Na Saleh Ally
MCHEZO wa soka hapa nchini
sasa unazidi kuingia kwenye njia ambazo si sahihi na hasa suala la uadui na
ubabe.
Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) ambalo linapaswa kuongoza mchezo wa soka katika njia sahihi, linaonekana
kushindwa na sasa ubabe unachukua nafasi kubwa.
Kumekuwa na wadau wengi wa
soka ambao wamekuwa wakilalama kutishiwa au kulazimishwa kufungwa midomo
wakitakiwa kutozungumza jambo lolote kuhusiana na TFF hasa inapoonekana kuna
tatizo katika shirikisho hilo.
Mmoja wao ni Dk Damas
Ndumbaro ambaye TFF imefanya kichekesho kwa kumfungia miaka saba, eti kwa kisa
cha kuzitetea klabu zilizokuwa zikipinga TFF kuzikata fedha zao za udhamini
kutoka Azam TV na Vodacom.
Achana na Dk Ndumbaro, hata
serikali kupitia Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma
Nkamia ilipinga jambo hilo ambalo lilionekana si sahihi. Lakini TFF
ikalifikisha haraka kwenye kamati ya nidhamu na kumfungia Dk Ndumbaro akiwa nje
ya Tanzania.
Kwa kuwa wadau wengi wa
soka wamekaa kimya, TFF inataka kutumia mwanya huo wa kuendesha kampeni za
kinyama, kunyanyasa watu, kuwafunga midomo kwa nguvu na anayesema anaonekana ni
adui. Mfano mzuri ni Fortunatus John Mang’wela ‘Photu’.
Mang’wela ndiye mwenyekiti
wa matawi ya Simba katika Wilaya ya Temeke na hivi karibuni alikutana na mkasa
wa kuzuiwa kuingia uwanjani kwa madai alizungumza redioni akitaka Rais wa TFF,
Jamal Malinzi ajibu hoja za Dk Ndumbaro kuhusiana na ubadhirifu wa fedha za TFF
na si kukaa kimya.
“Nimekutana na mkasa huo na
ulianza Jumamosi wakati Yanga wanacheza na Mgambo. Nilifika Uwanja wa Taifa
nikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Temeke (Tefa). Walinzi wakanizuia
kuingia na ilionekana walipangwa.
“Nikawaomba angalau niingie
nikamshushe mwenyekiti, wakaniruhusu, nikaingia na ‘eskoti’ hadi ndani,
nikamshusha mwenyekiti, halafu nikatolewa nje.
“Kawaida kwa kuwa mimi ni
mwenyekiti wa matawi, nina kitambulisho maalum. Nikaona ni bora nikate tiketi,
nikalipa shilingi elfu kumi na tano, nikaingia tena uwanjani na safari hii
niliona walinzi walivyokuwa wakiniangalia, nikajua kuna jambo.
“Yule (Wilfred) Kidau
(Kiongozi wa TFF), ndiye aliongoza zoezi la kunizuia. Nikawa nimefanikiwa
nimeangalia mpira. Baadaye nilimfuata na kumuuliza tatizo ni nini, maana ni mtu
tunayefahamiana. Wao TFF wamekuwa wakishangazwa na mimi kumsakama Malinzi na
uongozi wao wakati mimi ni mtu wao pia kama ndugu yao.
“Nikamueleza, sikuwa na
sababu ya kukaa kimya wakati naona kuna tatizo na hata mahojiano yangu katika
redio za Clouds, Magic na Times katika siku tofauti ilikuwa ni sehemu ya
kuonyesha mimi ni mdau na ninataka maendeleo na wala sina chuki na Malinzi.
Baadaye nikaachana na Kidau,” anasema Mang’wela.
“Jumapili mimi niliwahi
kufika uwanjani, Simba inapocheza Taifa, mwenyeji wake ninakuwa mimi, maana
ndiyo mwenyekiti wa matawi ya Temeke, lakini ajabu nikazuiwa tena. Kwangu
niliona sasa TFF imeingia hadi kwenye kuihujumu Simba, vipi mwenyeji ambaye ni
mimi nizuiwe?
“Kwa mara nyingine nikaamua
kukata tena tiketi, nikaingia kwa shida na kuangalia mechi. Imeisha tu akaja
askari mmoja anaitwa Muddy, ana nyota moja. Akaja kunikamata eti nimemtukana
Kidau, nikashangazwa sana.
“Sikufanya ubishi, nikasema
acha tulipeleke jambo hilo kituoni. Maana ningeanzisha mzozo, mashabiki wa
Simba pale ingekuwa shida. Nikatumia busara za kiutu-uzima. Ajabu nataka
tuondoke kwenda kituoni, askari akawa analazimisha nikapande Difenda wakati mimi
nina gari langu pale.
“Nikamuuliza Muddy, kwa kosa
la kumtukana mtu, unataka niache gari langu (Toyota) Prado la shilingi milioni
30 pale uwanjani! Likiibiwa? Nikamsisitiza achukue hata askari kumi wapande
kwenye gari langu twende kituoni.
“Ajabu sikufunguliwa mashtaka
na askari wengine wenye busara walipokuja pale wakaona ni mambo ya kitoto na
kutaka anayeing’ang’ania aachane nalo. Kwanza hakukuwa hata na ushahidi wa mtu
kutukanwa, halafu wanaume wanashitakiana eti mtu katukanwa, ajabu sana!”
“Nakuambia mpira wetu
unatumbukia pabaya, kama sasa imefikia hata viongozi wakizungumza lolote
kuhusiana na TFF basi wanazuiwa kuingia uwanjani au wanaonekana ni maadui!
“Tusipoangalia TFF
itakwenda kubaya, watu wataanza kuumizwa au kuingia ambako mpira haukufika.
Maana uadui huu utajenga chuki kwa wengine, halafu badala ya furaha na
maendeleo, itakuwa ni maumivu.
“Mchezo wa soka haujawahi
kuwa hivi hapa nchini, Tanzania si nchi ya watu kuzuia watu wasiwe huru
kuzungumza. TFF inataka watu waoga, wasio na uwezo wa kufikiri au kuchangia.
Mimi nasimama kidete na nitaendelea kwenda uwanjani ila wadau waamke,
tunakokwenda si kuzuri na huu si mpira wetu, maana viongozi wanaonekana kama
hawajui wanalofanya na badala ya maendeleo wanatengeneza uadui,” anasema Mang’wela
akionyesha kuwa na uchungu kutokana na unyanyasaji aliokumbana nao kutoka kwa
Kidau, kiongozi wa TFF ambaye ni swahiba mkubwa wa Malinzi.
0 COMMENTS:
Post a Comment