Na Saleh Ally
KOCHA wa Yanga, Marcio Maximo, amekuwa akiwaingiza washambuliaji
Jerry Tegete na Hussein Javu kurekebisha mambo, hasa anapoona mambo hayaendi
vizuri.
Pia amekuwa akimuingiza kiungo wa pembeni, Simon Msuva kuongeza kasi
ya timu katika dakika za mwisho. Naye ameonyesha kweli ni chachu kwa kuwa
amefanikiwa kufunga mabao matatu akitokea benchi.
Kwanza akianza na mechi dhidi ya Tanzania Prisons aliyofunga bao
moja, lakini juzi amefunga mabao
mawili na kuibeba Yanga kuifunga Mgambo kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Tayari Tegete na Msuva wameonyesha kuwa wanaweza kuwa msaada kwa
plani za Maximo hasa anapoamua kutumia Plan B baada ya ile ya A kukwama. Wakati
Tegete anafunga mabao mawili dhidi ya Stand United, Yanga ilikuwa inaongoza kwa
bao moja lililofungwa na Jaja.
Bao hilo halikuwa linatosha na wenyeji walikuwa wanapiga presha
kubwa. Mabao mawili ya Tegete aliyeingia katika dakika ya 70, yakaihakikishia
Yanga ushindi na Plan B ya Maximo ikafanya kazi.
Wakati Msuva anaifungia Yanga mabao yote mawili dhidi ya Mgambo,
juzi, hakukuwa na bao lililokuwa limefungwa na huenda Yanga ilikuwa inakwenda
kwenye hatari ya suluhu au kupoteza.
Tayari wachezaji hao wawili wameonyesha wanastahili kuwa kwenye
kikosi kinachoanza cha wachezaji 11 na Maximo ana kila sababu ya kuliangalia
hilo.
Hata kama ni kitaalamu, inaruhusu mchezaji anayeingia kipindi cha
pili na kufanya majukumu yake sahihi, basi anatoka kwenye Plan B na kurudi Plan
A. Maximo hapaswi kuwa muoga.
Kuendelea kuwa mwoga kutowabadili Jaja na Coutinho kwa maana wawe
wanaingia wakitokea benchi, basi atakuwa anafanya hivyo kwa maslahi ya hofu au
kuangalia kuwa mchezaji wa kigeni ni lazima acheze kwa hofu ya kuona labda
viongozi wa Yanga, wanachama au mashabiki wanaweza kuona hana msaada.
Yote yanaweza kutokea, lakini kikubwa kuangalia maslahi ya timu kama
Yanga kwa kuwa ndiyo yanayotakiwa kuwa namba moja. Huenda Jaja au Coutinho
wanaweza kuwa bora zaidi katika Plan B, kitu ambacho Maximo hajajaribu na
hapaswi kuwa muoga.
Inawezekana Maximo kutokana na ugeni wake na kikosi cha Yanga,
alikuwa anajaribu kusaka kikosi sahihi. Wakati umefika mambo yako wazi kuwa
Msuva na Tegete wanastahili kuanza na baadaye Jaja na Coutinho waingie, hili
wala halitakuwa na maana kuwa hawana msaada.
Maana hata Msuva na Tegete wanaweza kuanza halafu ikaonekana
wameshindwa kuwa msaada katika dakika 60 za mwanzo, basi wanaweza kubadilishwa
pia na Jaja na Coutinho wakapewa nafasi tena. Hivyo hakuna haja ya kutanguliza
woga.
Msuva:
Inawezekana inahitaji muda kwa Maximo kumuamini mapema kijana Simon
Msuva. Analazimika kumuingiza kipindi cha pili kama timu inahitaji mabao ambayo
yamegoma au yanahitajika ya kuongeza.
Huenda Maximo anataka kumuingiza Msuva katika kipindi cha pili akiwa
‘fresh’ wakati safu za ulinzi za timu pinzani zinakuwa zimechoka, hivyo anakuwa
msaada zaidi, yote sawa.
Takwimu zinaonyesha anastahili kuanza katika kikosi cha kwanza na
Maximo hapaswi kuwa muoga au kuingia hofu ya Coutinho kukosa namba au kuingia
kikosi cha pili.
Asili ya Yanga kiuchezaji ni kasi, krosi na mashambulizi ya haraka
na pasi ndefu. Hiyo haitabadilika zaidi ya kuboreshwa, ndiyo maana mara nyingi
mawinga wakali ambao sasa wanajulikana kama viungo wa pembeni, zaidi wamekuwa ‘wakizaliwa’
Yanga.
Kusema Mrisho Ngassa akae nje, bado haitakuwa sahihi, badala yake
Yanga inataka viungo wa pembeni wenye kasi kutoka kushoto na kulia. Wale ambao
watakuwa wanapiga krosi kali na huenda Jaja, Tegete au Hussein Javu watakuwa na
nafasi ya kupata mipira mingi zaidi.
Tegete:
Aliingia katika mechi dhidi ya Stand United, Yanga ikiwa ugenini na
kufanikiwa kufunga mabao mawili ndani ya dakika 10.
Huwezi kumlaumu Maximo kwa Tegete kwa kuwa ndiye kocha anayejua
uwezo wake kwa kiasi kikubwa, lakini huenda anahitaji kukubali kwamba ili
Tegete ajiamini zaidi anahitaji kucheza muda zaidi.
Hakuna ubishi, Maximo anamuamini Jaja kuliko Tegete kwa kuwa ni
mshambuliaji huenda ana rekodi nzuri zaidi alikotoka, lakini kumuonyesha kuna
ushindani kwa Tegete, anaweza kubadilika haraka zaidi.
Jaja anakwenda anaimarika kwa maana ya uchezaji kwa kuwa anapata
muda mwingi wa kucheza na anaona tofauti ya soka la Brazil na hapa Bongo.
Tegete anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Maximo katika kipindi hiki kama atapata
muda wa kujenga hali ya kujiamini.
Si lazima wagawane 50-50 kwa maana ya muda, lakini angalau Jaja
acheze dakika 60 na mwisho amuachie Tegete amalize. Kwenye soka, mchezaji
anaweza kuongezewa uwezo kwa kupewa nafasi zaidi ya kucheza.
Dakika chache za mwisho hasa 15, timu nyingi zinakuwa zimebadili
aina ya uchezaji kutokana na kutaka ushindi yaani zinalinda bao au kutaka sare
kwa kupoteza muda, hivyo haimpi nafasi mchezaji kufanya vizuri.
Dakika 25 kwa mchezaji anayetakiwa kufanya
jambo ni bora zaidi, anaweza kuchemka au kuwa msaada kabla ya kipindi cha
mwisho. Hivyo Maximo anaweza kufikiria kuwapa muda zaidi.
Kwa kuwa Maximo ndiye kocha, anaweza kujua zaidi kuhusiana na
wachezaji wake. Mchezo wa soka una raha yake kwa kuwa unachezwa hadharani na
uwanjani hakuna mwembe wala mnazi wa kujificha, hivyo hakuna kificho, mambo
yote yanaonekana.
0 COMMENTS:
Post a Comment