Kiungo mchezeshaji wa Yanga, Mnyarwanda,
Haruna Niyonzima, amesema hafurahii maisha anayoendelea nayo kwenye timu hiyo
na kufunguka kuwa hataongeza tena mkataba wa kuendelea kubaki Jangwani.
Mnyarwanda huyo anayeichezea timu ya
taifa ya Rwanda, alijiunga na klabu hiyo msimu wa 2012/2013 akitokea APR ya
nchini kwao.
Kiungo huyo, hivi sasa anaruhusiwa
kufanya mazungumzo na klabu nyingine anayotaka kwenda kuichezea kutokana na
mkataba wake kubakiza miezi sita.
Niyonzima amesema hajui sababu ya
kocha wake Mbrazili, Marcio Maximo kumtoa kwenye mechi nne mfululizo za ligi
kuu dhidi ya Simba, Stand United, Kagera Sugar na Mgambo JKT, zote katika
kipindi cha pili, bila kuambiwa sababu.
Niyonzima alisema, yeye ni mchezaji
mkubwa, ni vyema akaambiwa sababu ya kutolewa na kocha wake ili ajue tatizo ni
lipi kwa ajili ya kujirekebisha.
Aidha alisema, pia amechoshwa na uzushi
unaosambazwa na baadhi ya viongozi na makomandoo wa timu hiyo za yeye kushawishiwa
kusaini Simba na kipa namba mbili wa timu hiyo, Juma Kaseja.
Aliongeza kuwa, hali hiyo inamfanya akose
amani ya kubaki kuendelea kuichezea Yanga, hivyo amepanga kurejea kucheza ligi
kuu ya nchini kwao mara baada ya mkataba wake kumalizika.
“Kiukweli kabisa nimechoka kuichezea
Yanga kutokana na sababu mbalimbali. Kwa mfano kocha amenitoa kwenye mechi nne
mfululizo za ligi kuu dhidi ya Simba, Stand United, Kagera Sugar na Mgambo bila
kuniambia sababu ili nijue tatizo langu nijirekebishe, hali hiyo inanifanya
nichanganyikiwe kabisa.
“Mimi ujue ni mchezaji mkubwa
ninayeitumikia timu yangu ya taifa, pia ni tegemeo katika timu yangu,
ninayecheza dakika zote 90, sasa iweje Yanga niwe natolewa katika kipindi cha
pili?
“Kingine kikubwa kinachonichosha
kubaki Yanga ni uzushi ninaosambaziwa kutoka kwa baadhi ya makomandoo kuwa
Kaseja ananishawishi niende kusaini Simba, kwa kuwa ninalala chumba kimoja naye
kila tunapokuwa kambini,” alisema Niyonzima.
Ndio tatizo la wachezaji wenye ubinafi kama wewe,Ucheze wewe tu na wenzio wasipate nafasi ya kucheza?Sababu zako hazina msingi na unaonyesha umechoka kuitumikia yanga,ruksa kwenda unakojisikia kwenda,Ila asante sana.
ReplyDelete