November 17, 2014


NISEME bila ya kukwepesha mambo kuwa mimi ni mzalendo ninayesikia raha kuona vijana wa Kitanzania wanafanikiwa. Hakuna asiyejua sisi Watanzania hatuna mafanikio kabisa kimichezo nje ya mipaka, sasa hata nyumbani!


Katika soka mambo yanabadilika na utasikia gumzo la usajili la dirisha dogo, mapemaa limeanzia kwa wazawa. Simba gumzo kubwa lilikuwa ni Jonas Mkude, kiungo kinda ambaye Msimbazi wamefanya kila linalowezekana kumbakiza.

Simba imemwaga Sh milioni 60 kumbakiza Mkude, hakuna anayeona Msimbazi wametoa fedha nyingi, labda atakayejitokeza aone chache. Mwisho, kiungo huyo Mtanzania atalazimika kufanya kazi kwa ubora ili aendane na thamani yake.

Ukiachana na Mkude, Mtanzania mwingine kinda naye amekuwa gumzo, huyo ni Simon Msuva. Simba imeeleza nia yake ya kumpata na imesema itatuma barua Yanga kuuliza kama itampata.

Ingawa Simba ilitangaza dau dogo la Sh 500,000, lakini hiyo inaweza kuwa moja ya mbinu za kutaka kumnasa Msuva. Iwapo Yanga itakubali kukaa meza moja na Msimbazi ili wajadili, hakuna ubishi Simba itakuwa tayari kutoa dau kubwa kumpata kiungo huyo wa pembeni mwenye kasi ya kimondo.

Wapo wanaojaribu kuweka thamani kwamba Msuva anaweza kufikia hata Sh milioni 100, yaani thamani yake ya usajili na inawezekana ikazidi. Hii ni faraja kuu kuona wachezaji wa Tanzania wakigombewa.

Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji vya juu kuliko hata wale wa Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, DR Congo na kwingineko, lakini wamekuwa wakiangushwa na mambo mawili makuu.


Kwanza ni viongozi kutoamini kuwa wana uwezo, lakini wakati mwingine viongozi wanakuwa sahihi. Halafu wachezaji hao ndiyo wanakuwa tatizo kutokana na kutojiamini, hilo ni tatizo jingine.

Kwa kuwa Msuva na Mkude wameaminika, kitu wanachotakiwa kukiangalia ni kutolala au kujisahau katika kipindi hiki ambacho wamepata heshima au sifa ya juu. Tunajua wapo wengi ambao waliporomoka mapema kutokana na kuvimba vichwa.

Msuva na Mkude wote watakuwa na mapumziko mafupi baada ya kusimama kwa Ligi Kuu Bara kwa muda hadi mwezi ujao mwishoni. Hiki si kipindi cha wao kulala au kuanza kufanya starehe kwa kuona sasa hakuna kama wao.
Wawili hao ni wachezaji makinda ambao safari yao ya kuanza kupata mafanikio ndiyo imefika gia namba mbili. Wana gia nyingi za kuongeza mbele ili kufikia mafanikio sahihi.

Mafanikio ya mwanzo humchanganya karibu kila anayeyapata, ili Msuva na Mkude waone kuwa wanakwenda katika njia sahihi lazima waamini wana deni kubwa kwa kuwa imani ya watu wa Yanga na Simba kwao imekuwa kubwa.

Wanachotakiwa ni kuwaonyesha walipatia kuwaamini, mfano Msuva, wengi wamekuwa wakitaka apewe nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza. Hivyo asiwaangushe wanaomuamini.
Kutowaangusha wanaomwamini ni lazima ajitume kwa juhudi kubwa ili kufikia mafanikio ya juu, pia kuwa msaada katika kikosi cha Yanga. Anaweza kuwa msaada tu kama atafuata mambo muhimu kama mazoezi ya kutosha, kujituma pia juhudi.
Kizazi cha kina Msuva, Mkude ndiyo njia sahihi ya mabadiliko. Kwani sasa ni tegemeo kwenye vikosi vyao wakiwa makinda, baadaye watakuwa tegemeo kwenye timu yetu ya taifa. Tayari klabu zao zimewaamini, basi wao pia wanapaswa kudhihirisha hilo.

Msisitizo wangu ni kwamba wakati wa likizo, wachezaji hao na wengine wanaweza kuutumia kwa kupumzika lakini lazima wajitunze ili wahakikishe wakirejea kuzitumikia katika ligi, basi wawe na kiwango cha kutosha ili kuongeza ushindani kama ambao umejitokeza katika mechi saba zilizopita ambazo zilionekana hazina mwenyewe.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic