BAHANUZI |
Uongozi wa Stand United ya mkoani
Shinyanga, bado unazidi kuonyesha mapenzi yake kwa straika wa Yanga, Said
Bahanuzi na umesisitiza upo tayari kutoa kitita cha Sh milioni 10 ili kumnasa
katika usajili huu wa dirisha dogo.
Bahanuzi kwa sasa hana nafasi katika
kikosi cha kwanza cha Yanga, huku wakitumika zaidi akina Geilson Santana Santos
‘Jaja’ na Jerry Tegete katika nafasi moja ya ushambuliaji.
Stand inamhitaji Bahanuzi kwa udi na
uvumba, ili iweze kuimarisha safu yake ya ushambuliaji ambayo bado haijakaa
sawa tangu kuanza kwa michuano ya ligi kuu msimu huu.
Hii ni mara ya pili kwa Stand kuitaka
Yanga iwapatie mchezaji huyo, baada ya kumkosa katika usajili wa dirisha kubwa kabla
ya kuanza kwa msimu huu.
Kocha Msaidizi wa Stand, Athumani
Bilali, amesema uongozi wa timu yao hivi sasa upo katika harakati kabambe za
kuhakikisha wanampata Bahanuzi ambaye mwaka 2012 aliibuka mfungaji bora wa
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame) na kuongeza kuwa
tayari wamemtengea kiasi cha fedha kisichozidi milioni 10.
“Siku ya Jumanne (kesho) tunatarajia kukutana na viongozi
wetu kwa ajili ya kupanga mikakati yetu ya raundi ijayo ya ligi kuu, ikiwa ni
pamoja na suala zima la usajili.
“Hata hivyo, kwa sasa uongozi wetu
unaendelea na harakati za kuhakikisha safari hii Yanga inatupatia Bahanuzi
baada ya kumkosa hapo awali,” alisema Bilali.
0 COMMENTS:
Post a Comment