Simba na Yanga wiki hii zinatarajia
kuingia kambini kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe utakaopigwa Desemba 13,
mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa. Ikumbukwe Simba ndiyo wenye kombe hilo,
ambalo walilitwaa msimu uliopita baada ya kuwanyuka wapinzani wao mabao 3-1,
huku straika Amissi Tambwe akitupia mawili.
Hata hivyo, wakati Kocha wa Yanga,
Marcio Maximo akitarajia kutia guu nchini leo Jumatatu akitokea kwao Brazil, Tambwe
naye anatua Bongo leo akitokea kwao Burundi ambapo alikwenda kwa ajili ya
mapumziko mafupi.
Tambwe hapendwi na mashabiki wa Yanga
kutokana na mabao yake ya Nani Mtani Jembe iliyopita, kufukuzisha benchi zima
la ufundi, lililokuwa chini ya Mholanzi Ernie Brandts pamoja na Fred Felix ‘Minziro’.
Akizungumza na kutoka mjini Bujumbura, Tambwe alisema kuwa ameamua kurejea mapema kwa
ajili ya kuwahi mazoezi, tayari kuwavaa Yanga hiyo Desemba 13.
“Mpaka sasa (jana) bado nipo Bujumbura
nimepumzika, ila natarajia kuja huko (Dar) Jumatatu (leo) kwa ajili ya kujifua
kujiandaa na mchezo unaotukabili,” alisema.
Aidha Ofisa Habari wa Simba, Humphrey
Nyasio, alisema wachezaji walitarajiwa kuanza kurejea kuanzia jana kwa
wachezaji wote wa kitaifa na kimataifa.
Licha ya Simba kuonekana kutofanya
vema, hata hivyo imekuwa na matokeo ya kuridhisha mbele ya Yanga, ambapo mara
ya mwisho kwa Yanga kushinda ilikuwa msimu wa 2012/13 huku Simba ikiigaragaza
kwenye Mtani Jembe kabla ya kutoa sare kwenye michezo mitatu iliyofuatia ya
Ligi Kuu Tanzania Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment