Na Saleh Ally
KUWA mkweli ni tabu, lakini nianze na
kusimamia kuhusiana na mshambuliaji Geilson Santana ‘Jaja’ aliyekuwa akikipiga
Yanga.
Santana, raia wa Brazil, ameamua kubaki kwao
Brazil, kuna mengi yanasemwa kuhusiana naye kwamba yeye ameamua, wengine
uongozi umeona aende, familia yake imeona asirudi Tanzania lakini ukweli,
hataichezea Yanga.
Mipango ya kuziba pengo lake imeanza, kiungo
Mbrazil, Emerson De Oliveira Neves Rouqe,
anatua nchini kesho kuanza majaribio, akifuzu atapewa nafasi ya kuziba pengo la
Jaja, akionekana hawezi, basi safari imemkuta na Yanga itasaka straika DC Congo
au Zambia.
Nilimsikia mmoja wa wazee wa Yanga, Ibrahim
Akilimali, akisema kuwa wamefurahishwa na kuondoka kwa Jaja kwa kuwa katika
mechi saba za ligi alifunga bao moja. Tena alikuwa mshambuliaji asiyegombea
mpira.
Kauli hiyo ya Akilimali imekuwa ikizungumzwa
na mashabiki wengi wa soka ambao huenda wamekuwa wakikubali kusikiliza tu
wanachoelezwa bila ya kufanya tathmini.
Usimlaumu mzee Akilimali, wala usiwashangae
wanaosema Jaja alikuwa anaweza. Ishu ya msingi tujifunze kuwa, baada ya
kuondoka tuliona nini kwake.
Hakuweza kupambana kugombea mpira, hilo
alifeli. Lakini alikuwa bora kwenye kufunga na mabao yake matatu yanajibu
maswali zaidi ya mia aliyotuachia. Nani amejifunza ambaye anaweza kufaidika na
walichopatia na kukosea Yanga kwa kumleta Jaja?
Je, Jaja angepewa ushindani zaidi, mfano Kocha
Marcio Maximo akawa anawapanga akina Jerry Tegete au Hussein Javu, halafu yeye
akaingia baadaye ingekuwaje?
Wanaosema alikuwa ni mbovu, takwimu
zinaonyesha vipi? Kwamba kweli alifeli kupita wote na hakuwa ni mwenye viwango?
Huenda ni hisia, lakini ukisema mechi
zinazotambulika, achana na zile za kirafiki, Jaja aliichezea Yanga mechi nane.
Moja ya Ngao ya Jamii na saba za ligi.
Amefunga mabao matatu katika mechi saba.
Akianza na kufunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Azam FC, Yanga ikabeba
ngao.
Katika ligi, mambo yalikuwa magumu hadi
alipofunga dhidi ya Stand United mjini Shinyanga wakati Yanga ikishinda kwa
mabao 3-0, mawili yakiwa yamefungwa na Jerry Tegete.
Kukimbia:
Huenda mashabiki wengi hawakufurahishwa na
Jaja kutokuwa na mbio, kutopambana au kuonekana mshambuliaji mwenye mikiki na
vurugu.
Huenda naweza kuungana na mashabiki au watoa
tathmini, kuwa Jaja hakuwa akipambana, jambo ambalo niliamini angeweza
kubadilika kama angetaka na kucheza soka bora baadaye.
Lengo si kuwalaumu Yanga au mtu mwingine, ila
kupitia mshambuliaji huyo, licha ya kuondoka, bado tunaweza kumtumia kama somo.
Mabao:
Alifunga mabao matatu katika mechi
zinazotambulika na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Angalia mabao yake matatu, mawili katika mechi
dhidi ya Azam. La kwanza akifunga katikati ya mabeki wawili na kipa, akajirusha
na kuuguza mpira kiufundi.
Bao la pili, hii itabaki zawadi ya muda mrefu
kwa mashabiki wa soka. Baada ya kupewa pasi, alitulia na kumuangalia kipa, kwa
ujasiri mkubwa akauchota mpira, ukajaa wavuni.
Bao la tatu, mechi dhidi ya Stand kwenye
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Jaja huku akiwa anaangalia upande wa lango
lake, akageuka kama mshale na kuachia shuti lililojaa wavuni.
Hakuna anayeweza kubisha kwamba Jaja alifunga
mabao matatu, yote yakiwa kwenye kiwango cha “yanayoweza kufungwa na straika
anayejua tu.”
Viwanja:
Kingine ni kwa viongozi, kwamba wanaweza
kujadili na kuangalia kwamba kwa wachezaji kutoka mabara ya Ulaya, Asia na
Amerika Kusini wanaweza kupata kazi kutamba hapa nyumbani.
Ukiachana na viwanja vya Taifa na Azam
Complex, Chamazi vyote vya jijini Dar es Salaam, uwanja pekee wenye ubora mzuri
ni Kambarage, Shinyanga.
Jaja amefunga mabao kwenye viwanja vyote
vyenye kiwango kizuri. Ingawa Taifa alifunga mabao mawili tu, lakini hakuna
ubishi alifunga. Hivyo kuna tabu na viwanja vyetu na Jaja ameondoka akituachia
somo kwamba lazima TFF na Bodi ya Ligi wasimamie ubora wa viwanja ili timu
zisajili wachezaji kutoka kwingine ikiwezekana Ulaya, la sivyo, watakuja hapa
kuchekesha tu.
Suala la kusimamia viwanja vikawa bora
linawezekana, tumeona Shinyanga hawakuwa kwenye ligi. Wamerejea na uwanja wao
tayari uko bora kuchezewa. Vipi kwingineko washindwe?
Wanaomzidi Yanga:
Simon Msuva mwenye mabao matatu na Jerry
Tegete mwenye mabao mawili. Wachache wana bao moja kama Jaja (kwenye ligi),
hivyo hakuwa mbali na kujirekebisha na huenda kama angepewa changamoto,
angeweza kufunga zaidi.
Wageni wenzake:
Ukizungumzia wachezaji wa kigeni, anza na
mfungaji bora wa msimu uliopita, Amissi Tambwe kutoka Burundi, hadi ligi
imesimama alikuwa na bao moja kama ilivyo kwa Jaja.
Wageni wengine ambao walikuwa wana bao moja
hadi mechi saba zimepigwa kwa kila timu ni Kipre Tchetche (Azam FC-Ivory
Coast), Haruna Niyonzima (Yanga-Rwanda), Andrey Coutinho (Yanga-Brazil), Yayo
Lutimba (Uganda) na Itubu Imbemu (Coastal-DR Congo).
Kwa kuwa hata wageni hawa wana bao moja,
huenda wanaweza kujirekebisha na kufunga mabao zaidi katika mechi sita
zilizobaki za mzunguko wa kwanza na 13 za mzunguko wa pili.
Wanaoongoza:
Wanaoongoza ni wale wenye mabao manne kila
mmoja ambao ni Danny Mrwanda (Polisi Moro), Didier Kavumbagu (Azam FC), Rashid
Mandawa (Kagera), Rama Salim (Coastal) na Ame Ali (Mtibwa Sugar).
Bado hakuna tofauti kubwa kutoka bao moja hadi
manne. Utaona katika wafungaji watano wa mabao manne kila mmoja, kuna wageni
wawili na wenyeji watatu.
Kavumbagu kutoka Burundi, huu ni msimu wake wa
tatu Ligi Kuu Bara, Salim anayetokea Kenya, amefanikiwa kwa msimu wa kwanza
kuanza vizuri lakini utaona hakuna tofauti kubwa Kenya na Tanzania kiuchezaji.
Mwache aende:
Mwisho mwache Jaja aende, lakini bado
alihitaji muda kuzoea mazingira ya soka ya Bongo. Maana hata Coutinho pamoja na
kasi, chenga, bado amefunga bao moja tu la mkwaju wa faulo, hii inathibitisha
muda ulitakiwa.
Wakati anakwenda Jaja, vizuri kujifunza kama
nilivyoeleza awali. Lakini Mbrazil huyo kama tukikubali kujifunza kupitia kwake
bila ya kujali Uyanga, Usimba basi kuna faida hapo baadaye. Tukipuuza, basi
tutaendelea kubaki kama jana.
0 COMMENTS:
Post a Comment