Mshambuliaji nyota wa Simba, Mrundi, Amissi
Tambwe, anatarajia kuondoka nchini leo na kwenda kwao Burundi kwa ajili ya
mapumziko lakini amepanga kuondoka na mizigo yake yote.
Tambwe ambaye hivi sasa hana raha katika
kikosi cha Simba kutokana na kuwepo kwa tetesi za kutaka kuachwa, amefikia
hatua hiyo akihofia kukutwa na balaa kama lililomkuta Mrundi mwenzake aliyewahi
kuitumikia klabu hiyo msimu uliopita, Gilbert Kaze.
Kaze ambaye alikuwa akicheza nafasi ya beki wa
kati katika kikosi cha Simba, alifungashiwa virago bila ya yeye kujua wakati
alipokuwa Burundi kwa mapumziko hali inayomfanya naye ahofie kukutwa na balaa
hilo.
Tambwe
amesema kuwa, mpaka sasa hajui hatma yake katika kikosi cha timu hiyo, hivyo
anaenda kwao Burundi akiwa amejiandaa kwa jambo lolote litakalotokea hapo
baadaye, ndiyo maana anatarajia kuondoka na mabegi yake yote.
Alisema pamoja na kupewa moyo na viongozi wa
timu hiyo, bado ana wasiwasi kwa sababu hajafanya mambo makubwa msimu huu kama
ilivyokuwa ule uliopita.
“Jambo jingine linalonipa wasiwasi ni
kuhusiana na mkataba wangu, kwani nimebakiza miezi michache tu, hiyo nayo
inaweza kuwa sababu lakini ngoja tuone itakavyokuwa.
“Natarajia kuondoka Jumatano (leo), kwenda
nyumbani kwa mapumziko lakini itabidi niondoke nikiwa nimejiandaa kwa kila kitu
na kama ikitokea nikaachwa basi nisihangaike tena,” alisema Tambwe ambaye msimu
uliopita ailiibuka mfungaji bora wa ligi kuu baada ya kufunga mabao 19.
0 COMMENTS:
Post a Comment