TANZANIA yetu ni nchi yenye kila kitu,
lakini utamaduni wa mambo kadhaa ndiyo umekuwa unachangia kutuangusha na hasa
suala la uoga, watu kuhofia kusemwa, kukosolewa na hata kuumizwa!
Jiulize kama ikiwa ni nchi iliyojaza waoga,
wasiopenda shida wala karaha, wasiotaka kuulizwa wala kusumbuka na hata kama
kitu kinaharibika, basi acha kiharibike tu kuliko kusemwa au kulaumiwa bure!
Lazima nijitenge, lazima niseme ukweli na
ninatoa shukurani kwa wote ambao wamekuwa wakiniunga mkono kutokana na suala la
fedha za Bonanza la Nani Mtani Jembe, kwamba lengo tujue, mgawo wake ulikuwaje.
Tukijua mgawo uliwaje, basi itakuwa ni
lahisi kujua fedha hizo zimekwenda wapi na wapi na zimesaidia vipi mchezo wa
soka yetu ambayo ni changa, inaendelea kupigania kupata ahueni.
Kuna mtu msomaji mmoja alijiuliza, kwamba
hauoni kama Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro
inayozidhamini Yanga na Simba ikiona inaandamwa, basi itajitoa na kuwa shida kwa
klabu hizo.
Jibu langu: “Simba na Yanga ni kubwa kuliko
bia ya Kilimanjaro hapa nyumbani, hata unapozungumzia udhamini, naweza kusema
zinapewa fedha kidogo, badala yake zingeongezewa kwa kuwa Kilimanjaro inatapa
nafasi pana ya kujitangaza kupitia klabu hizo kongwe.”
Jibu la msomaji: “Kweli naungana na wewe,
pia Kilimanjaro si mdhamini wa kwanza, akienda, wako watajitokeza, hizi timu
zinauzika kweli.”
Nimekuwa na mijadala mingi na wasomaji wengi
kupitia namba yangu ya 0658 939769, wanaungana na mimi, sasa wanaamini TBL
imepata faida kubwa kujitangaza.
Lakini kumbe nao wanashangazwa kama ilivyokuwa
kwangu, vipi inachukua mapato ya mlangoni?
Kama TBL haijachukua, nani kachukua,
kapeleka wapi, kwa nini na kwa faida ya nani? Lakini pia nataka kujua, mpira
umefaidika kwa kiasi gani?
Fedha za soka, lazima zifaidishe mchezo wa
soka. Hilo halina mjadala na ningependa kama TBL wangelieza hili suala kuliko
kukaa kimya. Najua kama wataendelea kukaa kimya,nitapiga hodi ofisini kwao ili
kwenda kupata uhakika wa mambo.
Najua huenda nikapata sapoti ndogo kutoka
kwa wanahabari wenzangu kwa hofu kuwa watakosa kitu fulani kama urafiki wao na
watu wa TBL. Lakini sasa ni wakati wa kuusaidia mpira wa Tanzania, tuwe wazi
bila ya uadui wala hofu hata kidogo.
Bado naendelea kukadiria kwamba ni Sh
milioni 500 hadi 580 zinaweza kuwa zilipatikana siku ile katika mechi ya Nani
Mtani Jembe 2. Nani aliisimamia, nani alichukua fedha zote hizo na zimeusaidia
vipi mpira wetu.
Nilitaka tutajiwe mapato nilipoandika Hoja
Yangu, Ijumaa. Hilo bado nalisisitiza, lakini nauliza tena, nani alichukua
fedha hizo na ziliufaidishaje mpira wetu kwa kuwa naona si sahihi kama fedha
zinatokana mpira zinakwenda kutengeneza tasnia nyingine au matumbo ya watu
wachache halafu mpira unaendelea kudidimia.
Vizuri waandaaji wa mechi hiyo wakatuambia,
wakafafanua ili mien aye nipunguze maswali mengi kuhusiana na hilo. kama
hakutakuwa na majibu, basi nitalazimika kutaka kujua, sidhani kama nitafikia
kuhamasisha maandamano.
Swali la msomaji mmoja, lilikuwa hivi: “Saleh
Ally, kwani wewe umepata hasara gani, hata wasiposema ni kiasi gani wameingiza
wewe unakosa nini?”
Jibu langu: “Ninacho cha kukosa, mimi ni
mdau michezo, soka ni moja wapo. Kama fedha zake, zitafaidisha wachache, halafu
kila mmoja akakaa kimya eti hakupata hasara yoyote, basi ndiyo mpira wetu
unaangamia. Tusiache watu wachukue fedha za soka na kuweka mifukoni mwao
wanavyotaka, usisahau Yanga, Simba ni za wananchi kama mimi na wewe na si mali
ya viongozi wala TBL. Je, unajua TBL kazi yao ni kuuza bia na si kuandaa mechi
na kuchukua mabao?”
Msomaji hakujinibu, huenda alikuwa busy au
aliishiwa credit. Nitasubiri jibu lake, lakini wakati hajanijibu, nakumbushia
tena. Mgawo wa Nani Mtani Jembe ukoje? Nani na nani kachukua na unafaidishaje
soka nchini? Nitarudi.
0 COMMENTS:
Post a Comment