Na Saleh Ally
KOCHA Marcio Maximo aliyetupiwa virago vyake
Yanga na Hans van der Pluijm ambaye anachukua nafasi, kila mmoja unaweza
kumzungumzia ndani ya miezi sita akiwa Jangwani.
Pluijm ndiye alianza kuifundisha timu hiyo
kabla ya Maximo, aliingia mkataba wa miezi sita, mwishoni akaona hakuna dalili
za kuongeza wakati timu ilikuwa inafanya vziuri, akaondoka zake na kujiunga na
Al Shaolah FC ya Saudi Arabia, ambayo hakudumu nayo.
Pluijm anaonekana kuwa na rekodi nzuri na
Yanga kwani hakufukuzwa katika miezi hiyo sita, pia uongozi ulijaribu
kumrudisha baada ya kuwa ameingia mkataba na Al Shaolah ikashindikana.
Maximo pia alisaini mkataba wa miaka miwili
kutokana na rekodi yake akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars. Lakini ameutumikia
mkataba huo kwa miezi sita tu, sawa na ile ya Pluijm.
Ndani ya kipindi hicho, bila ya kujali huyu
alifukuzwa na yule aliondoka, jambo la kutazama hapa ni mambo mbalimbali ya
uwanjani na kiuongozi ili kuangalia tofauti za makocha hao, mmoja kutoka Bara
la Amerika Kusini, mwingine Ulaya.
Uoga:
Hakuna kocha asiye muoga kufungwa, lakini
Maximo imezidi na hili lilianza kujionyesha zaidi wakati alipokuwa katika
kikosi cha Taifa Stars.
Lakini alipokuja Yanga, hali hiyo
ilijionyesha mapema.
Alikataa katakata kucheza mechi za kirafiki ikiwemo ile
dhidi ya Azam FC na baadaye Mtibwa Sugar.
Kiasi fulani, mambo ya Maximo
yanachanganyika na siasa, kwa kuwa ni mtu wa maneno mengi na ikiwezekana kama
ataharibu, kamwe huwa hakubali.
Misimamo:
Wote ni makocha wenye msimamo, wasumbufu kwa
waandishi wa habari. Hawatoi nafasi kubwa ya kueleza mambo mengi wanayofanya
kama ambavyo mafunzo mengi ya kisasa ya makocha yanavyoagiza kushirikiana na
vyombo vya habari kwa ukaribu zaidi.
Maximo alijipangia kuzungumza kila Ijumaa,
hata hivyo mara kadhaa amekuwa akichagua sana kuzungumzia mambo fulani na
mengine kuyaacha.
Pluijm kwenye kuzungumza ni uwazi kwa kiasi
kikubwa. Si mtu anayetaka kubania maneno, lakini kumpata azungumze pia ni kazi
lakini akiamua kuzungumza, anaeleza kila kinachotakiwa kujibiwa.
Timu:
Timu ya Maximo inakuwa na mchanganyiko,
vijana na wakongwe. Lakini wakati anaanza ni muoga kubadili kikosi chake, wengi
ambao anawakuta huendelea kuwatumia na baadaye anaanza kutoa nafasi.
Alitoa nafasi kwa kina Jerry Tegete na Kiggi
Makasi akiwa Taifa Stars. Lakini Yanga ni Hamis Thabiti pekee alimrudisha na
hakucheza zaidi ya mechi tano katika kipindi chote cha miezi sita aliyokaa.
Si lahisi kutoa nafasi kwa wachezaji walio
nje ya kikosi kilichozoeleka na wakati mwingine ni mtu anayejikinga sana na
lawama, hivyo huhakikisha anajaza nyota wote ili kujiondoa kwenye kulaumiwa.
Mholanzi Pluijim si muoga, anapenda kujaribu
na anapenda kutoa nafasi kwa wachezaji wengi zaidi. Utaona katika mechi za
majaribio anaweza kubadili kikosi mara kadhaa kama alivyofanya wakati
alipoifundisha Yanga kwa miezi sita kabla ya kuondoka kwenda Al Shaolah FC.
Kasi:
Kikosi cha Maximo kinajaza watu wengi zaidi
nyuma. Kawaida mabeki wanne hubaki kabisa nyuma na mabeki wa pembeni huenda upande
mmoja au kubaki wote kabisa. Mfano Oscar Joshua na Juma Abdul, walipiga krosi
chache zaidi wakati wa kipindi cha miezi sita cha Mbrazil huyo.
Inawezekana Pluijm akamfuatia Ernie Brandts
ambaye alitaka vijana wake wapande zaidi kutokea pembeni na kupiga krosi nyingi
zaidi.
Lakini ukimlinganidha Brandts na Maximo,
utaona Mholanzi huyo kikosi chake kinacheza kwa kasi zaidi kwa kuwa anataka
timu ‘inayotembea’. Pluijm amekuwa akisisitiza timu yenye kasi kwa maana ya
kuwachosha na kuwachanganya wapinzani wao.
Mazoezi:
Katika mazoezi, mwanzoni hakukuwa na tofauti
kubwa sana. Lakini ufundishaji wa Maximo ulionekana una ulaini kidogo kwa maana
ya ‘loading’, yaani mzigo mkubwa. Unapoanza mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.
Basi yatanakiwa mazoezi magumu sana.
Angalia tofauti yao hapa, Maximo anaamini
zaidi makocha kutoka nchini kwake Brazil, ndiyo maana alisisitiza kuja na
Leonardo Neiva. Lakini Pluijm kwa kuwa ni mkazi wa bara la Afrika, anajua nini
cha kufanya katika timu za Kiafrika.
Alisisitiza kuwa na msaidizi kutoka Brazil,
lakini msisitizo wa Pluijm ni kuwa na msaidizi wa hapa Tanzania na anayemvutia
zaidi ni Charles Boniface Mkwasa na ndiye anajua mazingira ya wachezaji wa
Kibongo.
Hivyo anapofanya maandalizi ya mwanzoni mwa
msimu, anajua dozi ya kuwapa wachezaji ili wawe fiti. Kocha wa Express ya
Uganda aliwataja wachezaji wa Yanga kutokuwa na stamina ya kutosha wakati
walipowafunga katika mechi ya kirafiki.
Lakini kwa Pluijm, utaona Yanga inabadilika,
timu yenye kasi na nguvu na wachezaji wanajua shuruba ya mazoezi ya mwanzo
ingawa kwa sasa, hakutakuwa na mazoezi makali sana labda kujaziajazia maana
mechi za ligi, ziko karibu.
Upendeleo:
Maximo alikuwa hawaamini zaidi makocha wa
Kitanzania. Hata alipokubaliana na Yanga kuja nchini, uongozi ulimsisitiza
tayari una kocha msaidizi ambaye ni Mkwasa, yeye akakataa katakata.
Kwa nini? kumbuka hata akiwa Stars
alisisitiza kuja na Itamar Amorim. Hadi alipoondoka kwenda Azam FC, yeye ndiyo
akaanza kuonyesha imani kwa Ali Bushiri.
Lakini Pluijm ni tofauti, si kwa kuwa
tu ameoa mwanamke raia wa Ghana, hivyo anaweza kuwa ‘shemeji’ wa Afrika, lakini
anawaamini makocha wa Kiafrika na hata akiwa Ghana, alikuwa na wasaidizi
kutokea nchi husika na si kwao Ulaya.
0 COMMENTS:
Post a Comment