Baada ya kukamilisha siku nne akiwa kazini anainoa Yanga, Kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm tayari amepata kikosi cha
kwanza atakachoanza nacho kuivaa Azam FC.
Timu hizo, zinatarajiwa kuvaana katika mechi
ya Ligi Kuu Bara, itakayopigwa Desemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa
jijini, Dar es Salaam.
Pluijm alianza kibarua cha kukinoa kikosi
hicho Jumamosi ya wikiendi iliyopita mara baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu
hiyo Mbrazili, Marcio Maximo kutimuliwa.
Katika mazoezi yake hayo ya siku nne, kocha
huyo alionekana akikiandaa kikosi hicho kwa kuwapanga pamoja na kuwapa mbinu
mbalimbali za ndani ya uwanja kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji.
Kocha huyo, katika kikosi hicho cha kwanza
kinatarajiwa kuwa na sura mpya nne zitakazoanza kuonekana kwenye mechi dhidi ya
Azam FC, ambazo ni Salum Telela aliyekuwa anaanzia benchi, Danny Mrwanda,
Amissi Tambwe na Akpah Sherman waliotua kuichezea timu hiyo katika usajili wa
dirisha dogo.
Wakati hawa wanaingia Andrey Coutinho, Jaja
ambaye ameshatimka, Hassan Dilunga na
Juma Abdul ambao walikuwa na nafasi ya kuanza kwenye mechi nyingi
kipindi cha Maximo hawapo kwenye kikosi hiki cha Pluijm.
Kikosi hicho cha kwanza kinatarajiwa kuundwa
na Deogratius Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Kelvin Yondani, Salum Telela, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima, Tambwe, Sherman
na Mrwanda.
Wakati kikosi hicho kikiandaliwa, kwenye mechi
ya Azam FC huenda kukawepo na mabadiliko kidogo kutokana na Cannavaro kutumikia
adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata wakati timu yake ilipocheza na Kagera Sugar.
Hivyo, kutokana na Cannavaro kutumikia adhabu
hiyo, nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Twite atakayecheza pamoja na
Yondani huku Telela akicheza namba mbili huku Saidi Juma akicheza namba sita ya
Twite.
“Baada ya siku tano nitakuwa nimeshajua kabisa
nani atakuwa wapi na nani wapi nimeanza kazi hivi karibuni sidhani kama
mnatakiwa kuwa hofu sana,” alisema Pluijm.
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye ligi kuu
ikiwa na pointi 13, baada ya kucheza michezo saba, ushindi hapa unamaana kuwa
Yanga watafikisha pointi 16 ambazo ni moja zaidi ya kinara Mtibwa Sugar.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment