Na Saleh Ally
GUMZO la ujenzi wa viwanja kwa klabu mbili
kongwe la Yanga na Simba, sasa linaonekana ni kama hadithi isiyokuwa na jipya,
imezoeleka.
Hadithi ileile, kuanzia aliyepita, aliyepo,
huenda hata tunayemtarajia, huenda akaingia na kuzungumza yaleyale.
Big G ukiitafuna sana, kawaida inaisha
utamu. Lakini inavyoonekana si hii inayozihusu Simba na Yanga, ni tamu tu kila
kukicha.
Yanga na Simba, wangekuwa wawekezaji, basi
ungewaita ni wale wasio na uwezo wa kujenga kiwanda licha ya kuwa na maeneo
yao.
Jiulize, Yanga na Simba, kweli kwa historia
yao, sehemu walizopita, ukubwa wao. Wanashindwa kujenga hata uwanja wa mazoezi?
Yanga na Simba ndiyo timu zinazoongoza kwa
kuhangaika kwa uwanja wa kufanyia mazoezi kuliko timu nyingine yoyote nchini!
Najua utabisha, hauna haja ya kuzifananisha
na Azam FC yenye uwanja wake au Stand United, yenye uhakika wa kujifua
Kambarage. Mfano mzuri ni Ajabalo FC ‘Mnyama Mkubwa’ ya Sinza.
Ingawa inatumia Uwanja wa Shule ya Msingi
Mashujaa, ukiuliza kila mtu eneo hilo atakueleza ni uwanja wa Abajalo, hata
kama haiumiliki.
Nikikuuliza leo, Yanga au Simba, uwanja wao
wa nyumbani ni upi? Naamini utakuwa hauna jibu.
Hata kama Yanga na Simba, zote ni Sports
Club, yaani zinazoshirikisha michezo mbalimbali si soka tu. Vipi hazina viwanja
vilivyo tayari kutumika angalau kwa ajili ya mazoezi tu?
Kuna hoja nataka niiweke mezani, tujaribu
kuijadili na kuangalia mwendo au kipimo cha safu mbili za uongozi za klabu hizo
zinazoongozwa na Yusuf Manji na Evans Aveva kama kweli wako makini na wanataka
mabadiliko hasa katia suala la uwanja.
Yanga au Simba, zinapofanya mazoezi kwenye
Uwanja wa Boko Veterani, zinalipa Sh 300,000 kwa wakati mmoja. Labda asubuhi,
zikifanya mara mbili kwa siku, ni Sh 600,000.
Yanga inalipa Sh 100,000 kila siku kwenye
Uwanja wa Shule ya Sekondary ya Loyola ya Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kwa mazoezi pekee, kwa mwaka Yanga na Simba
zinaweza kutumia hadi Sh milioni 27 kwa timu moja. Piga hesabu ya miezi mitatu
tu!
Hadi Boko Veterani, imeweza kutengeneza
uwanja. Hii ni timu ya watu wanaotaka kujifurahisha tu! Vipi taasisi kubwa kama
Simba na Yanga ambazo mpira ndiyo biashara namba moja?
Yanga inakwenda kwenye michuano ya
Shirikisho, imepangiwa kukipiga na BDF. Huenda ikawa ndiyo timu pekee ambayo
haina hata uwanja wa mazoezi?
Ni kichekesho na maajabu. Inaonekana ni
kawaida kwa kuwa imezoeleka, lakini ukiiangalia kwa kina ni kitu kinachotia
aibu, kinyaa na hakifai kuendelea kujadiliwa bila vitendo.
Yanga walishaonyesha ramani na thamani ya
uwanja wao inajulikana. Simba wamesema wameishapata ramani. Sasa hiyo ya michoro
inatosha, vizuri tuanze kuona tingatinga likianza kazi.
Kutokuwa na uwanja wa uhakika, unazifanya
Simba na Yanga kutokuwa na programu za uhakika. Mfano Yanga haiwezi kutumia
uwanja wa Loyola kwa jioni. Viwanja vyenye wenyewe, wakati fulani wanakuwa na
ratiba zao.
Shule za Msingi, Shule za Sekondary
zinamiliki viwanja. Klabu kongwe ambazo kazi tao ni soka, hazina viwanja!
Ajabu zaidi, kila upande una eneo angalau la
kujenga ‘pitch’ tu. Nani kajaribu angalau kuanza? Imefikia kwa wachezaji wa
kigeni, kuwasajili, kuwaacha, kuwalipa fidia. Yanga na Simba zingekuwa
zimekamilisha uwanja kwa msimu mmoha tu.
Hii ni sehemu ya kuonyesha asilimia kubwa ya
vingozi wanaioingia kuongoza Yanga na Simba ni waoga, wanachojaribu ni kupata
ushindi ambao ni wamuda.
Bora Yanga kumfunga Simba au Simba kushinda dhidi ya
mtani, yaani mambo ya muda. Lakini uwanja ni mipango endelevu. Sasa mbona
hawafanyi?
Wakati mwafaka wa viongozi kuona aibu. Kwa
kuwa hawana sababu ya eneo, badala yake ni suala la ujenzi tu. Jengeni basi
acheni blah blah, hamchoki kuulizwa!
0 COMMENTS:
Post a Comment