Na Saleh Ally
TAYARI uongozi umefanya mazungumzo na Kocha Goran
Kopunovic raia wa Serbia amekubali kuja nchini, anatua leo asubuhi tayari kwa
ajili ya kuingia mkataba na mara moja kuanza kazi.
Kopunovic ni mmoja wa makocha wenye jina kubwa nchini
Rwanda, anatua Simba kuchukua nafasi ya Patrick Phiri ambaye kazi yake haijawa
nzuri tokea ametua kwani katika mechi nane za Ligi Kuu Bara, ameshinda moja,
sare sita na kupoteza moja.
Simba wanataka mabadiliko, Kopunovic hawezi kuwa kila
kitu lakini kuna mambo ambayo wachezaji, mashabiki na wadau wengine wa soka
wayatarajie mara baada ya kutua nchini na kuanza kazi.
Huenda kila kitu kisiwe bora katika kipindi kifupi,
lakini Kopunovic ni kocha mwenye mambo mengi, mazuri na mengine yanakera, yeye
ni binadamu pia.
Uchezaji:
Wakati anaingoza Polisi Rwanda kwa misimu miwili,
ilisifika kwa kucheza kwa kasi, wachezaji wake walikimbia muda wote na sifa
yake kubwa ni kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye pumzi ya kutosha.
Kutengeneza pumzi ya kutosha si jambo rahisi, lazima
mazoezi makali. Kopunovic ni kocha anayependa kikosi chake kiwe fiti kwa
kucheza kasi ya dakika 120 katika dakika 90, hivyo wachezaji wavivu wa mazoezi
Simba, watakiona.
Mafanikio:
Hakuwahi kubeba ubingwa wa Rwanda, lakini aliisaidia
Polisi kubadilika na kufikia kuwa tishio. Kwani kwa misimu mitatu
aliyoifundisha, mmoja alishika nafasi ya tatu ukiwa ni wa kwanza kwake na
miwili, yote alishika nafasi ya pili, nafasi ambayo ilikuwa ni aghalabu kwa
kikosi hicho kuipata.
Mara ya kwanza alishika nafasi ya pili nyuma ya APR
waliokuwa wakinolewa na Ernie Brandts ambaye baadaye alikuja kuinoa Yanga.
Msimu uliofuatia alishika tena nafasi hiyo nyuma ya Rayon Sports iliyokuwa
inanolewa Didier Gomez raia wa Ufaransa.
Kwa nafasi hizo mbili, ilikuwa ni mafanikio makubwa sana
kwa Polisi ambayo awali haikuwa kwenye hadhi ya vigogo wawili, yaani Rayon
Sports inayoongoza kwa mashabiki Rwanda na APR inayomilikiwa na jeshi.
Pia aliingia fainali ya Kombe la Amani mara mbili dhidi
ya APR, zote akapoteza kwa 4-2 na 2-1. Alipata nafasi ya kucheza Kombe la
Shirikisho, lakini wakaishia raundi ya kwanza.
Kubadili:
Pamoja na kuwa na uwezo wa kukibadili kikosi chake kama
atapewa nafasi ya kufanya kazi kwa uhakika, Kopunovic ana sifa ya kuwabadili wachezaji
hadi kuwa hatari.
Kwa wachezaji wasio wavivu ni rahisi kubadilika na
kupanda kiwango kama ilivyokuwa kwa Meddy Kagere, Mnyarwanda mwenye asili ya
Uganda ambaye alikuwa tishio hadi kufikia Yanga kumtaka kwa udi na uvumba,
lakini ikashindwa.
Jazba:
Hili ni tatizo lake kubwa, kuanzia kwa wachezaji wake
hasa wale ambao hawamuelewi, lakini Goran si mvumilivu sana kwa marefa ambao
wataonekana hawakitendei haki kikosi chake.
Wakati fulani ukiwa ni msimu wake wa pili kuinoa Polisi,
kidogo amtwange refa aliyekuwa akimtuhumu kuiuma Polisi katika mechi ya ligi ya
nchini humo. Amekuwa mwepesi kuomba radhi kila baada ya kuboronga.
Yanga:
Anaijua Yanga kwa mambo mawili, kwanza ilimfunga mabao
2-1 katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Nyamirambo mwaka 2012, baada ya
kuwa imetwaa Kombe la Kagame, halafu ikafanya ziara hadi Kigali na kulipeleka Ikulu
ya Rais Paul Kagame.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kasi ya juu, Yanga ikiwa
chini ya Tom Saintfiet ilishinda kwa mabao hayo yaliyofungwa na Stefano
Mwasyika na Hamis Kiiza.
Pili anaijua Yanga kwa kuwa ilikubaliana naye aje
kuifundisha, kila kitu kikawa kimeenda sawa, lakini katika hatua za mwisho
kabisa, uongozi ukamtosa na nafasi yake kuchukuliwa na Brandts.
Ingawa wajumbe wengi wa Yanga waliamini Kopunovic ni
bora zaidi ya Brandts, lakini hoja ya vipi timu yake imeshika nafasi ya pili na
Brandts amebeba ubingwa, ndiyo iliyoifanya Yanga ibadili mawazo hatua ya mwisho
na kumtosa Mserbia huyo ambaye aliishapaki mabegi tayari kuja Dar.
Kopunovic anatua nchini leo akitokea Hungary anakoishi,
amezaliwa Februari Mosi, 1967 na alicheza soka la kulipwa katika nchi za
Serbia, Hungary na Hispania.
Alikuwa mmoja wa washambuliaji wakali na inaelezwa ana
uwezo mkubwa wa kuwatengeneza washambuliaji na kuwa tishio.
0 COMMENTS:
Post a Comment