Na
Saleh Ally
UMEONA
wachambuzi na wadau wengi wa habari wameandika kuhusiana na tathimini ya namna
ulivyokuwa mwaka 2014 na matokeo yake kibao katika michezo mbalimbali.
Wamesema
kocha alivyofukuzwa, wameeleza makocha wapya walivyoajiriwa, namna timu
zilivyosajili wachezaji wapya, migogoro kwenye vyama vya riadha na kadhalika.
Mambo
ni mengi, unaweza kuyaita burudani ya kutosha lakini ukweli hasa ni yale
yanayoonyesha katika mwaka huu tunaoumaliza leo hakuna la maana ambalo
tulilifanya na tunaweza kujivunia.
Tumefanya
nini kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars? Tumefanya nini kwenye timu
ya taifa ya wanawake, Twiga Stars? Jibu litakuwa hakuna. Hata kama utauliza
kwenye ngumi za kulipwa, ridhaa, riadha, zaidi ya afadhali, hakuna cha
kujivunia kwamba kilikuwa kikubwa na kitakuwa dira au muongozo sahihi kwa mwaka
unaoanza kesho wa 2015.
Leo
ndiyo siku ya mwisho ya mwaka 2014, mwaka ambao haukuwa na tija hasa katika
soka na michezo mingine. Mimi niufunge kwa masikitizo makubwa na hasa katika
suala la Nani Mtani Jembe.
Nimekuwa
nikihoji mara kadhaa kuhusiana na klabu za Yanga na Simba, kwamba zilifaidika
nini wakati wa mechi ya kirafiki iliyopewa jina la Nani Mtani Jembe kwa kuwa
tuliona idadi kubwa ya watu iliyojaa uwanjani.
Hakuna
ubishi idadi ya mapato, unaweza kukadiria hadi Sh milioni 550 lakini
uchanganuzi wa mapato kuhusiana na mechi hiyo umekuwa ni kama kiza. Kimya
kutoka TBL ambao ndiyo wanaomiliki Bia ya Kilimanjaro inayozidhamini Yanga na
Simba.
Maswali
yote ya msingi hayajajibiwa, badala yake chuki na hasira kwa baadhi ya wahusika
kuwa kwa nini ninahoji! Lakini si suala la chuki, badala yake ni maswali ya
kawaida anayoweza kuuliza yeyote anayejiuliza na anayetaka kujifunza.
Najua
wako waliokaa kimya, watu wa hewala, wasiojali wapi tunakwenda kombo au
wasioona haja ya kurekebisha upepo mbaya kabla haujatengeneza dhoruba inayoweza
kuuvuruga kabisa mchezo wa soka ambao bado unasuasua.
Wapo
mashabiki wa soka ambao wamekuwa wakiniunga mkono tena sana kwa kuchangia
kupitia simu yangu ya maoni yenye namba 0658 939769.
Wengine
siwajibu, waniwie radhi kwa kuwa ujumbe unaoingia ni mwingi kupita kiasi,
nahitaji muda wa ziada hata kuwaambia nawashukuru kwa kuelewa nini
ninachokihoji, ni kwa ajili ya manufaa ya mchezo wa soka.
Hakuna
anayeweza kukataa fedha za viingilio siku hiyo zilitolewa na wapenda mpira
nchini ambao wangependa mpira uendelee kupitia fedha zinazotokana na mchezo
huo. Nisisitize, Simba na Yanga si mali ya viongozi wa klabu hizo, badala yake
wanachama, hivyo wana haki ya kujua.
Taarifa
zinaeleza Kilimanjaro ndiyo waliandaa pambano hilo, sawa. Ingawa mimi najua
kazi kubwa ya kampuni hiyo ni utengenezaji wa ‘udirinki’, vipi iingie hadi
kwenye kuandaa masuala ya mechi? Vipi wachukue hadi mapato wakati wao ni
wadhamini na walipaswa kufaidika na udhamini tu?
Ukimya
wao unazua maswali mengi sana. Kwanza niwaahidi sitachoka, nitaenda
nikiwashirikisha hadi mashabiki wa Yanga na Simba, siku watakayofunguka na
kuweka ukweli hadharani, nitakaa kimya.
Kikubwa
watueleze, wao TBL kama ni kweli walichukua fedha, kiasi gani na kwa nini? kama
si wao, aliyechukua ni nani, kiasi gani na kwa nini?
Ukimya
huu maana yake mapato hayo yamepotea hewani au kuna watu wamegawana. Je, kama
waliogawana hawaoni kama wataichafua TBL ambayo kiheshima iko juu kwa maana ya
moja ya makampuni makubwa nchini?
TBL
ikiendelea kukaa kimya, kumbe haijachukua haioni inajichafua? Kama yupo
aliyechukua na kuziacha Yanga na Simba zikiwa hazina kitu haoni ni kuzidi
kuzinyong’onyesha na kuzitumia mwisho kuziacha zikiendelea kuogelea umasikini?
Maswali
yako mengi, yanapaswa kujibiwa badala ya ukimya ambao hauna sababu. Safari
ijayo, nitakuja na maoni ya mashabiki wa soka ambao wamekuwa wakinitumia ujumbe
wao, nawasisitiza waweke tu majina yao na waniambie wako tayari nitumie
walichokiandika na namba zao za simu.
Naufunga
mwaka huu na maswali mengi ya kujiuliza. Bado nasisitiza hivi, kwa kuwa nina
haki ya kuhoji kama chombo cha habari, basi nitaufungua mwaka na maswali zaidi,
hadi kitakapoeleweka. Wadau kila la kheri na mwaka wa 2015.
ESCROW?
ReplyDelete