December 8, 2014


Na Saleh Ally
MOJA ya ishu gumzo England kwa sasa ni kupoteza kwa Chelsea ambayo ilikuwa haijafungwa hata mechi moja katika michezo 14.


Michezo 14 bila ya kupoteza katika Ligi Kuu England si kitu kidogo. Ugumu wa ligi hiyo unajulikana, ndiyo maana rekodi ya Arsenal ya msimu wa 2003-04 ya kucheza bila ya kupoteza hata mchezo mmoja, inagombewa.

Kila timu imekuwa ikipambana kuifikia, Kocha Jose Mourinho alionekana yuko njiani, anakaribia kuifikia, lakini mwisho kipigo dhidi ya Newcastle kimefuta ndoto zake.

Newcastle imeipiga Chelsea kwa mabao 2-1, yaliyofungwa kwa ustadi mkubwa na Msenegali, Papiss Cisse katika ushindi ambao umekuwa na maana kubwa na mambo matatu muhimu yanaweza kuzungumziwa.

Hakuna ambaye alijua Chelsea ingeweza kupoteza dhidi ya Newcastle. Ilikuwa rahisi kufikiri siku wakikutana tena na timu kati ya Manchester United au Manchester City ingekuwa rahisi wao kukwama.

Sasa wamekwama kwa Newcastle ambayo imepanda hadi nafasi ya saba huku Chelsea ikibaki kileleni lakini tofauti yake ya pointi na Man City imepungua na kubaki tatu tu, hivyo kuzidi kuongeza ugumu wa ligi hiyo ambayo siku zote haina mwenyewe.

Mourinho hana raha kwa kuwa hesabu zake zilikuwa ni kuweka rekodi huku akibeba ubingwa. Sasa hofu ya kuwajenga upya wachezaji wake kisaikolojia ili waweze kwenda na mwendo walioanza nao, imeanza.

Unaweza kusema sasa kimeeleweka kwa kuwa hakuna anayeonekana hana mbabe kwenye ligi hiyo kwa kuwa kila timu imeshapoteza mchezo.

Chelsea inabaki kwenye rekodi nzuri ya kuwa timu pekee iliyopoteza mchezo mmoja. Man City wamepoteza mechi mbili na Man United waliokuwa wanaonekana hawana mwelekeo wakipoteza mechi tatu tu!

Vitu vitatu vikubwa vya kuzungumzia baada ya mechi hiyo ya Chelsea iliyolala kwa Newcastle ni ushindani au utamu wa Premier League, Papiss Cisse na kocha Alan Pardew.


Utamu:
Ligi Kuu England ina burudani ya juu kabisa, si vibaya kusema ligi tamu kuliko zote kutokana na ushindani uliopo.

Kufungwa kwa Chelsea maana yake timu yoyote inaweza kufungwa, timu yoyote kati ya tano inaweza kuwa bingwa kwa kuwa hata tofauti ya pointi si kubwa sana.

Vinara wanapishana pointi tatu na Man City walio nafasi ya pili lakini City hawezi kuidharau Southampton ingawa anaizidi pointi saba tu kama ilivyo Man United anayoizidi nane.

West Ham nao wana kasi kubwa msimu huu wakiwa na pointi 24 kabla ya mchezo wao wa jana, moja tofauti na Man United na Newcastle iliyopanda hadi nafasi ya saba ikiwa na pointi 23, ikilingana kwa pointi na Arsenal.

Cisse:
Papis Cisse ni kati ya wachezaji wa Newcastle waliokuwa tegemeo lakini msimu huu hakuuanza vizuri na kuanza kuonekana kama hana msaada na timu.

Kama si msimamo wa kocha Alan Perdew, basi angeweza kuondoka kwa kuwa alionekana hafai.

Taratibu akaacha kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza, akaanza kumrejesha taratibu naye akawa anaonyesha umuhimu wake.

Juzi alikuwa muuaji wa Chelsea iliyoonekana haifungiki. Nani anayekumbuka kwamba alisema amekwisha? Hakuna!

Kikubwa ukweli uko hivi; uvumilivu ni jambo muhimu hasa katika kipindi ambacho kinaonekana ni kigumu kazini au katika maisha ya kawaida.


Pardew:
Mashabiki wa Newcastle walikuwa wakiingia uwanjani wakitaka kocha Alan Perdew afukuzwe. Uongozi wake ukaendelea kushikilia msimamo wa kubaki naye, hadi ukaingia kwenye ugomvi mkubwa na mashabiki wake.

Mashabiki hao waliandamana hadi kwenye barabara wakitaka kocha huyo atupiwe virago na Newcastle iliendelea kupata matokeo mabaya. Uongozi ukaendelea kushikilia msimamo.

Sasa katika mechi nane zilizopita, zinaonyesha hivi, Newcastle imeshinda mechi sita, sare moja, imepoteza moja na ndiyo rekodi ya juu zaidi ya mechi nane.

Yaani katika mechi nane zilizopita, Newcastle ndiyo timu iliyofanya vizuri zaidi ya zote. Katika mechi zake nane zilizopita, Chelsea imeshinda tano, sare mbili na kupoteza moja.

Kwa upande wa Man City, iko sawa na ile ya Newcastle, imeshinda sita, sare moja na kupoteza moja. Sasa unaweza kuamini kikosi cha Pardew kina rekodi sawa na ile ya mabingwa watetezi?

Kama ilivyokuwa kwa Cisse, inaonyesha Pardew amekuwa mvumilivu zaidi, alionyesha kuwaamini wachezaji wake akijua mambo yatabadilika.

Pongezi kwa uongozi wa Newcastle ambao ulionyesha unamkubali na kuendelea kumuamini kocha wake katika wakati huo mgumu na ukazidi kumpa moyo ukimsisitiza aendelee kupambana.

Sasa Newcastle iko katika nafasi ya saba, ina pointi sawa na Arsenal iliyo katika nafasi ya sita. Usisahau, katika msimamo iko kwenye nafasi ya juu zaidi kuliko timu zilizopewa nafasi zaidi kama Liverpool yenye pointi 21 katika nafasi ya tisa, Tottenham nafasi ya 10 ikiwa na pointi 18 na Everton pointi 18 imetulia namba 11. Soka bana!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic