Inaonekana mshambuliaji nyota wa Yanga, Mrisho Ngassa amepoteza mvuto kutokana na mambo kadhaa.
Kwanza kabisa amekuwa hafungi mabao au kufanya kazi kama ile iliyozoeleka, kwamba anatoa krosi nyingi safi au kufunga mwenyewe.
Wakati kikosi cha Yanga kikitarajiwa kushuka
uwanjani leo hii kupambana na Simba katika mechi ya Mtani Jembe 2, kocha mkuu
wa timu hiyo, Mbrazili, Marcio Maximo, amekifanyia mabadiliko makubwa kikosi
chake huku akimtupa nje kiungo wake, Ngassa.
Katika mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa
na wapenzi wa soka hapa nchini, Ngassa anatarajiwa kuanzia benchi kutokana na
kuporomoka kwa kiwango chake katika siku za hivi karibuni.
Maximo anatarajia kumuanzisha Simoni Msuva
ambaye tangu Ligi Kuu Bara ilipoanza msimu huu, amekuwa akianzia benchi na
kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ngassa au Andrey Coutinho huku
akionyesha kiwango kikubwa cha kuwa kikosi cha kwanza.
Tangu kikosi cha Yanga kilipoingia kambini
kujiandaa na mechi hiyo, Ngassa amekuwa akipangwa mazoezini katika kikosi cha
pili ambacho kinaundwa na wachezaji wengi wa akiba, hali ambayo imekuwa
haimfurahishi mshambuliaji huyo.
Inawezekana Maximo alifanya hivyo kumpa ugumu ili leo aanze, kama kweli akianza lazima afanye kazi ya ziada.
Mechi ya leo itakuwa ni sehemu ya uamuzi, kwamba Ngassa bado wamo au ndiyo safari inamkuta, kazi kwake kuonyesha hasi au chanya ingawa hakuna ubishi uwezo anao, je, anautumiaje? tusubiri.
0 COMMENTS:
Post a Comment