Kocha
Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, ameamua kuweka wazi kuhusiana na suala la kuondoka kwa mshambuliaji Amissi
Tambwe ambaye amejiunga na Yanga.
Amesema Tambwe raia wa Burundi alikosa nafasi kwenye kikosi chake, kwa kile alichosema hakuwa na uwezo wa
kupambana na mabeki wenye nguvu ukimlinganisha na Elias Maguli.
Kauli ya Phiri imekuja siku
chache baada ya Tambwe kusitishiwa mkataba wake Msimbazi, akidaiwa kushuka
kiwango wakati alifanya vyema enzi
za Mcroatia, Zdravko Logarusic na Abdallah Kibadeni, hadi kufanikiwa kuwa
mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Phiri amechambua kitaalamu
na kusema Tambwe ni mchezaji mzuri, lakini kilichomfanya asiwe na furaha Simba
ni kukaa benchi, hivyo kuvurugika kisaikolojia na kujikuta akishindwa kutimiza
majukumu yake kwa ufanisi akiwa uwanjani.
“Ukiangalia nilikuwa
nikimpanga Maguli katika mechi ambazo niliamini zina mabeki wagumu kupitika,
kitu ambacho Tambwe hakuweza kufanya, lakini alikuwa mzuri katika mechi zisizo
na beki ngumu.
“Jambo hilo lilimfanya
apoteze kujiamini na kukosa nafasi, hivyo kuathirika kisaikolojia na kujikuta
akishindwa kufanya vizuri ndani ya uwanja,” alisema Phiri.
Phiri ni kati ya makocha wakongwe barani Afrika ambao wamewahi kung'ara kwenye ngazi za klabu na timu za taifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment