ILIKUWA NI OKWI NA YEYE...YEYE NA OKWI.. |
Dakika 10 za kwanza za mechi ya Nani Mtani Jembe zilikuwa za hofu tupu huku wengi wakijiuliza kama mwamuzi mwanamama kweli angeuhimili mchezo huo kutokana na presha ilivyokuwa juu.
Mwanamama huyo anaitwa Jonesia Rukyaa, mwenyeji wa Kagera, amefunguka juu ya
mechi hiyo iliyomalizika kwa Simba kushinda kwa mabao 2-0.
Jonesia ambaye ana umri wa miaka 26, amemtaja
mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kuwa alihusika katika kuutesa moyo wake
mara baada ya mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi iliyopita huku akiitaja sababu.
Jonesia anasema taarifa kuwa alimpa Okwi kadi mbili za
njano kisha kuendelea kuwemo uwanjani, zilimuumiza kwa kuwa hazikuwa za ukweli
lakini anashangaa zilisambaa kwenye vyombo vya habari kwa kiwango cha juu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, juzi, Jonesia ambaye
kwa sasa yupo Kagera akiendeleza kazi zake za ujasiriamali, anafunguka kama
ifuatavyo:
“Namshukuru Mungu aliniongoza vema na kufanikiwa
kumaliza dakika 90 bila ya tatizo lolote, ila mechi hiyo ilikuwa si mchezo. Katika
dakika 10 za kipindi cha kwanza, nilitamani kuomba nifanyiwe mabadiliko kwani
mechi ilikuwa na kasi kubwa sana kupita maelezo.
“Nilikimbia huku na kule na kujikuta nikichoka ile mbaya
ukizingatia hali ya hewa ya Dar ni joto tofauti na ya Bukoba ambayo ndiyo
nimeizoea.
“Jambo zuri ni kuwa wachezaji wengi wa Yanga na Simba wanaelewa
sheria za soka, hivyo halikuwa jambo gumu kuwaelewesha.
“Jambo moja ndilo lililoniumiza na kunichanganya, zile
taarifa kuwa nilimpa Okwi kadi mara mbili zilinishangaza sana.
“Nilianza kupata mawazo na kuhisi familia yangu
itanionaje kama ni kweli, kama ingekuwa ni kweli basi ingehisi mtoto wao ni
mbumbumbu.
“Wengi walichanganya pale nilipompa kadi yule mchezaji
namba sita (Simon Sserunkuma) ambaye alijiangusha ndani ya eneo la penalti, kwa
kuwa Okwi ni nahodha alikuja kwangu kulalamika sasa wakadhani na kudhani kuwa
niliyempa kadi ni Okwi.
“Okwi nilikuja kumpa kadi kipindi cha pili kwa kosa la
kuvuta jezi ya mpinzani wake (Hussein Javu), hivyo nilimpa kadi ya njano moja
na siyo mbili.
“Zaidi ya hapo nashukuru Mungu sikupata vitisho
vyovyote, naamini watu wengi hivi sasa wanaufahamu mkubwa juu ya sheria 17 za
soka, tofauti na zamani, ndiyo maana sikuweza kukumbana na hali hiyo.”
Hiyo ilikuwa mechi ya pili kubwa kwa Jonesia, ya kwanza
ilikuwa ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro,
msimu uliopita.
Katika mechi ya Yanga, waamuzi wa pembeni walikuwa
Josephat Bulali na Mohamed Mono, wote wa Tanga.
“Mimi sijaolewa na bado ninaishi kwetu,” alisema Jonesia
huku akicheka.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment