December 28, 2014


Yanga inashuka uwanjani ndani ya muda mchache ujao kuwavaa Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam inasubiriwa kwa hamu kubwa na Yanga wakiwa na rekodi ya kuifunga Azam FC mabao 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii. Je, leo wataendeleza ubabe au Azam FC watalipa kisasi?

Kunaweza kukawa na maswali mengi sana, lakini burudani kubwa ni ile kati ya mafowadi wakali wa Yanga dhidi ya mabeki wa Azam FC.

Hakuna ubishi Azam FC ni moja ya timu zenye mabeki bora katika Ligi Kuu Bara na sasa wameongezewa nguvu mpya.

Kwanza walikuwa na watu hawa watatu imara kama chuma. Nahodha Aggrey Morris, David Mwantika na Said Morad. Kati ya hao wawili wakicheza, basi ujue kazi ipo.
Lakini sasa Serge Wawa kutoka Ivory Coast ambaye ni mzoefu, ameongeza nguvu zaidi na kuifanya Azam FC kuwa na ukuta chuma kabisa.

Yanga wanaweza kujivunia washambuliaji wao wawili wapya kabla ya kujumlisha wale wa awali.

Amissi Tambwe, huyu alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kabla ya Simba kumtema msimu huu. Lakini Yanga ina Kpah Sherman raia wa Liberia.

Huyu jamaa yuko sawa kweli kwa mujibu wa takwimu za mechi ya Bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba.
Ingawa hakumaliza, lakini alionyesha ni ‘shoka’. Swali, leo ataweza kuendeleza alichokifanya siku ile?

Je, Azam FC wataweza kuwazuia wawili hao ukijumlisha na Mrisho Ngassa, Simon Msuva na wageni wengine wawili, Haruna Niyonzima  raia wa Rwanda na Andrey Coutinho wa Brazil?

Lazima burudani itakuwa tamu na si hapo, hata washambuliaji wawili wa Azam FC, Didier Kavumbagu raia wa Burundi ataungana na Kipre Tchetche wa Ivory Coast.

Kazi itakuwa kwa safu ya ulinzi ya Yanga itakayoongozwa na Kelvin Yondani ‘Cotton’.

Lazima itakuwa ni mechi yenye burudani kuanzia kwenye ulinzi, kiungo na ushambulizi. Vizuri kuiangalia kitaalamu na kupumzisha ushabiki.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic