![]() |
| WACHEZAJI WA POLISI DODOMA WAKIMSHAMBULIA MWAMUZI WA AKIBA KATIKA MECHI YAO YA DARAJA LA KWANZA DHIDI TOTO AFRICAN KWENYE UWANJA WA CCM KIRUMBA, MWANZA. |
Na Saleh Ally
WAKATI mwingine nachelea kusema
Watanzania tumekuwa na uoga usiokuwa na sababu za msingi hadi kufikia kuwapa
watu nafasi ya kuvunja sheria, pia bila ya sababu za msingi.
Kweli kila mmoja wetu anajua nguvu
ya jeshi, maana wanatumia silaha, wana mafunzo ya kupambana, hivyo ni watu
ambao wameiva kwa mapambano.
Ninajua majeshi yote, wanapewa
elimu hiyo kwa ajili ya usalama wa raia na hakuna ubishi wote ni waajiriwa wa
wananchi ambao kodi zao ndizo zinazowalipa mishahara na kuendesha mambo mengi
ya majeshi hayo.
Leo nitazungumzia Jeshi la Polisi
Tanzania bila ya woga hata chembe, kwa kuwa sasa naona wanataka kugeuka sehemu
ya waharibifu wa amani na nidhamu katika mchezo wa soka.
Imekuwa ni hali ya kawaida, timu
zinazomilikiwa na Jeshi la Polisi kufanya vurugu bila ya woga wakijua hakuna wa
kuwagusa.
Timu hizo zinaundwa na baadhi
wakiwa maaskari na wengine raia, lakini wanafanya vurugu waziwazi wakijua wao
ndio wenye uwezo wa kuwaadhibu wengine wakifanya hivyo, kwa kuwa ni wao,
watalindwa wafanye vurugu.
Mechi lukuki zimetokea hivyo, tokea
wakati huo daraja la nne na wakati mwingine hadi Ligi Kuu Bara, mara kadhaa
tuliona mambo hayo na tukayakemea kwa nguvu kubwa.
Sasa naona yanaanza kurejea kwa
kasi kubwa huku kama ilivyo kawaida, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) na wengine wa ngazi za mikoa wakiwa kimya kwa ileile hofu kuwa hili ni
jeshi, mimi naifuta.
Naona yanayofanyika ni mambo ya
kijinga tena hadharani. Angalia namna timu ya Polisi Mara walivyowashambulia
kwa mawe kwa kuwapiga na kuwaumiza wachezaji wa Mwadui FC pamoja na Kocha,
Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Mshambuliaji Bakari Kigodeko
alipigwa jiwe kwenye goti kwa kuwa alitoa pasi ya kusawazisha bao. Julio
alipigwa jiwe la mgongo katika vurugu hizo.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka
Shinyanga (Shirefa), Kangi Lugola alipigwa na mashabiki hao, akachaniwa nguo,
hakika huyu mtu mzima ameaibishwa. Yote haya yametokea mjini Musoma.
Julio alilazimika kupiga simu Dar
es Salaam kwa kuwa baadhi ya waliokuwa wakishiriki ni rafiki wa askari na
hakuna anayeweza kuwazuia.
Siku hiyohiyo kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza, wachezaji wa Polisi Dodoma licha ya kuwa ugenini,
walikuwa ‘busy’ wakipiga waamuzi, wakianza na wa akiba, halafu yule wa
katikati.
Mmoja wa wachezaji bila ya aibu,
alimkimbiza mwamuzi huyo hadi jukwaani. Kufika huko mashabiki wakamtolea uvivu
na kumchakaza makonde na makofi. Lakini hivi karibuni timu nyingine ya Polisi
hukO Tabora ilifanya tena vurugu.
Hawa wachezaji na mashabiki wa
Polisi, jeuri wanaitoa wapi? Kwa nini wanafanya mambo haya ya kipuuzi na
kulichafua jeshi hilo ambalo lina watu wengi makini?
Hata hao makini, hawawezi kukwepa
kuchafuka kama watakuwa kwenye dimba la wapuuzi wachache ambao hawaelewi kazi
ya polisi ni kudumisha amani na utulivu badala ya kusababisha vurugu za
makusudi, huu ni upuuzi wa kupindukia!
Siku moja nikiwa kwenye Uwanja wa
CCM Kirumba, Mwanza, mwishoni mwa mwaka jana, nilishuhudia shabiki mmoja wa
Toto African akishuka jukwaani na kwenda kumuondoa mwandishi wa Championi
aliyekuwa akipiga picha karibu na kibendera.
Sababu za msingi, eti mganga wao
alisema mtu yeyote asikae eneo hilo. Mwandishi akakimbilia kwa askari waliokuwa
pale kushitaki, lakini kwa kuwa askari wale jamaa ni washkaji zao,
wakamsisitiza mwandishi aache kupiga picha eti wenye mechi hawataki! Angalia
maajabu haya!
Kuna sababu ya Jeshi la Polisi
Tanzania pia kuanzisha mafunzo maalum kwa wanaokwenda viwanja vya michezo ili
kuondoa hofu ya askari kutojua haki za wahusika walio uwanjani, mpigapicha
anatakiwa akae wapi, shabiki ashangilie namna gani na kadhalika.
Msisitizo ni kwamba, timu za soka
zilizo chini ya Jeshi la Polisi, zimekuwa zikilipaka matope jeshi hilo
kuonyesha kwamba hawana nidhamu.
Ajabu askari polisi wanataka
nidhamu na watu wafuate sheria wakati wao wanaonyesha ni mbumbumbu wa sheria za soka kwani wanaowapiga watu,
hawafuati sheria za soka. Wanawaachia rafiki zao wawaonee watu, wawaumize kwa
kuwa wanaamini wanatetea timu za polisi!
Hiyo inatokana na kujumuisha watu
wasio waelewa, wanaoamini kuwa askari ni kufanya unavyotaka huku wakiwa
wamesahau hata mchezo wa soka una sheria na kanuni zake na hakuna hata sehemu
moja inayoruhusu kupiga au kumshambulia binadamu badala yake ni kupiga mpira au
kushambulia kwa mpira pekee!










0 COMMENTS:
Post a Comment