Na
Saleh Ally
MJI wa Freiburg uko Kusini mwa nchi ya Ujerumani, sifa yake ni
utulivu na mji wenye watu wataratibu na wanaojiamini kwa kiasi kikubwa.
Mwaka
juzi nilihudhuria michuano ya vijana iliyofanyika kwenye mji mdogo wa Hausen
ambao uko takribani kilomita sita kutoka Mji wa Freiburg.
Baadhi
ya wachezaji waliokuwa kwenye michuano hiyo bila ya kujali walicheza au la ni
Said Ndemla (sasa yuko Simba) na Mudathir Yahaya (anaitumikia Azam FC) na Frank
Sekule, yuko Majimaji.
Watu
wa eneo hilo, wanasapoti kubwa kwa timu yao inayoshiriki Bundesliga. Hiyo ni FC
Freiburg ambayo kamwe hawajawahi kuwaza iwe bingwa na hawataki ishuke daraja,
shida yao kubwa ibaki Bundesliga ili iwape burudani.
Mmoja
wa wachezaji waliowahi kung’ara na timu hiyo ni Papis Cisse ambaye sasa yuko
Newcastle. Mmoja wa mashujaa na magwiji wa FC Freiburg ni Joachim Low, pia
anatokea eneo hilo na ndipo yalipo makazi yake.
Low
ndiye kocha mkuu wa kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani alichokifundisha kwa
mafanikio makubwa.
Kocha
huyo ni kati ya mashujaa wa eneo hilo, watu wa Freiburg wanajisifia kwa kusema
ukweli na wasio na hofu wakitaka jambo. Wanaotaka haki walio tayari kuiomba au
kushauri bila ya woga.
Kwa
sasa Low ni Kocha Bora wa Dunia 2014. Ameitwaa tuzo hiyo akiwabwaga Muitaliano
Carlo Ancelotti na Muargentina Diego Simeone.
Hata
kabla ya kutwaa tuzo hiyo juzi, Low alionyesha kweli anatokea Freiburg
alipozungumza jambo ambalo litasababisha mapinduzi katika mchezo wa soka.
Substitute
ya nne, yaani badala ya timu kufanya mabadiliko ya wachezaji watatu katika
mechi moja. Basi Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lifanye utaratibu wa
kuboresha kwa kuiangalia upya sheria hiyo ya mabadiliko.
Alichokisema
Low nakiunga mkono kwa asilimia mia moja kwa kuwa ndiyo uboresha mpya wa mambo
ya soka.
Soka
haliwezi kubaki palepale. Lazima kuna mambo mapya yatakuja kama ambavyo tumeona
Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini amependekeza iwepo
kadi nyeupe.
Kadi
nyeupe inapendekezwa kuwa itakuwa hivi; mchezaji anayelambwa kadi hiyo anaweza
kurejea baada ya muda fulani.
Sikuwahi
kuunga mkono wazo hilo la Platini kama ambavyo ninaunga hili la Low. Huu ni
mtazamo wa kila mmoja lakini ni hatua ya kutengeneza njia sahihi ya mchezo wa
soka ambao pia unaihusu Afrika na Tanzania kwa jumla.
Hakuna
ubishi Low hajasema kwa maslahi ya Tanzania, Yanga, Simba, Mtibwa au Azam FC,
anaangalia timu yake ya taifa ya Ujerumani, klabu za Ujerumani na Ulaya kwa
jumla, lakini anajua sheria itagusa dunia nzima kama kweli kutakuwa na
mabadiliko.
Ninaunga
mkono pendekezo hilo la Low kwa kuwa naona litawapa makocha hata wa hapa
nyumbani kubwa na wigo mkubwa wa kuwatumia wachezaji zaidi.
Wachezaji
watapata fursa ya kucheza zaidi hasa kama kocha anaona anahitaji kubadilisha
wachezaji lakini amekuwa akibanwa na mabadiliko mara tatu tu.
Yote
yanawezekana, alichoanzisha Low kinaweza kuwa mjadala lakini hata Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) linaweza kukifanyia tathmini na kuangalia kama kina
manufaa, basi nao wamuunge mkono Low.









0 COMMENTS:
Post a Comment