SIKU ambayo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
lilijitutumua na kutangaza kuufungia Uwanja wa Karume mjini Musoma kutumika
katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza, ndiyo siku ambayo wachezaji wa Polisi
Tabora walimtwanga mwamuzi.
TFF iliamua kuufungia uwanja huo baada ya vurugu kubwa
zilizozuka wakati timu ya Polisi Mara ikicheza na Mwadui FC, wikiendi
iliyopita.
Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alipigwa
jiwe la mgongo, mshambuliaji Bakari Kigodeko kwa kuwa alitoa pasi ya bao la
kusawazisha naye alipigwa huku Mwenyekiti wa Chama cha Soka Shinyanga, Kangi
Rugola naye akipigwa na kuchaniwa nguo hadi kubaki uchi!
Saa chache zilitofautisha vurugu za Musoma na zile za
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati wachezaji wa Polisi Dodoma
walipompiga mwamuzi wa kati na yule wa akiba.
Tena mchezaji mmoja wa Polisi Dodoma yeye alidiriki
kumkimbiza mwamuzi hadi jukwaani ambako aliambulia kipigo kutoka kwa mashabiki
wa Toto. Jiulize yule mchezaji alijiamini vipi hadi akapanda jukwaani?
Sasa TFF imetoa adhabu, huenda bado inaendelea
kuchunguza. Jana wachezaji wa Polisi Tabora nao walimpiga mwamuzi wa kati na
msaidizi wake.
Wachezaji hao wa timu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora,
wamempiga mwamuzi huyo baada ya Toto African kusawazisha bao na kufunga la
pili. Waliendelea kuwapiga waamuzi na mmoja alipokimbilia jukwaani walijaribu
kumfuata.
Mashabiki walionyesha kukasirishwa na kutaka kuwaadhibu,
hali iliyosababisha askari polisi waingilie. Baadaye mwamuzi akarudishwa chini
ya ulinzi mkali na kumaliza mpira, Polisi Tabora wakiwa wameshatoa timu yao
uwanjani!
Kiongozi wa soka kapigwa na mashabiki wa Polisi Mara,
wachezaji na kocha wa Mwadui FC wakapigwa na mashabiki wa Polisi Mara.
Siku iliyofuata wachezaji wa Polisi Dodoma wakampiga
mwamuzi huku akikimbizwa kama kibaka. Siku moja baadaye waamuzi wamepigwa na
wachezaji wa timu ya Polisi Tabora.
Maana yake timu za Polisi ndizo zinazoongoza kwa kujichukua
sheria mkononi katika mchezo wa soka. Hii ni sehemu ya picha mbaya kwa jeshi
hilo kwa kuwa lina timu zinazoendeshwa au kutumikiwa na watu wasiokuwa waelewa.
Hatuwezi kukwepa kwamba timu za soka zipo kwenye jamii,
wanajua kuhusiana na wananchi kukatazwa kuchukua sheria mkononi. Sasa vipi timu
za Polisi zinachukua sheria mkononi kwa kuwapiga waamuzi eti kwa kuwa wao ndiyo
polisi?
Jeuri hiyo ya kudharau mamlaka husika katika soka kama
TFF wanaipata wapi? Wanamtegemea nani? Kwa nini wanafanya hivyo?
Ndiyo maana nasisitiza, uamuzi wa TFF kufungia uwanja
pekee bado hautamaliza tatizo hili, badala yake kuwe na juhudi za kuwanasa
wahusika na adhabu yao iwe kali kupindukia ili iwe mfano kwa wengine.
Kama kweli kuna mwamuzi anaboronga, basi naye apewe
adhabu kali ambayo itakuwa mfano kwa wengine.
Lengo langu si kuwatetea waamuzi wafanye maovu, lakini
tukubaliane hatuwezi kuwa na waamuzi wanaofuata sheria kwa kupigwa kama ngoma
karibu kila mechi inayohusisha timu za Jeshi la Polisi au jeshi jingine lolote.
Si wanajeshi wala askari walio juu ya sheria, kwa kuwa
siku ya mwisho wote ni wananchi. Hivyo lazima wakubali kuna mamlaka zitakazoshughulikia
matatizo kama hayo.
Hata mamlaka hizo pia bado zinaweza kukosolewa kama
zitachukua uamuzi ambao si sahihi katika mambo ya msingi na haki.
Ndiyo maana nasisitiza, timu za majeshi lazima zionyeshe
kuwa zinatokea katika taasisi zinazoheshimika na nidhamu ndiyo uti wa mgongo,
badala ya kufanya mambo ya kihuni kama zinavyofanya sasa!









0 COMMENTS:
Post a Comment