Uongozi wa Yanga umesema mkataba wao na mshambuliaji Mbrazili, Geilson Santana ‘Jaja’ hauonekani kwenye makabrasha yao.
Jaja alisaini kuitumikia Yanga kwa miaka miwili, mwanzoni mwa msimu
huu lakini alidumu kikosini hapo kwa miezi mitatu tu ambapo klabu hiyo
ikatangaza kumshitaki na kutaka fidia ya shilingi bilioni 3.6.
Dk Jonas Tiboroha ambaye ni katibu wa Yanga, amesema kuwa nakala za
mkataba wa mchezaji huyo ambazo zinatakiwa kutumika kwenye kesi ya kumshitaki,
hazijulikani zilipo.
Dk Tiboroha amesema suala la Jaja linahitaji uchunguzi zaidi lakini
mkataba wake haupo na kuwatupia lawama viongozi waliopita kwa utendaji wao.
“Bahati mbaya sana, mkataba wa Jaja haupo, zaidi tunapata A, B, C
kuhusu Jaja, ninapata taarifa za kudodosa kuhusu hilo, labda nitatakiwa
kulifuatilia zaidi nikiingia ofisini na mbaya zaidi sijaingia ofisini.
“Lakini yote kwa yote sisi ndiyo wa kujilaumu kama viongozi kutokana
na kutenda mambo kienyeji zaidi,” alisema Dk Tiboroha.
Yanga inamdai Mbrazili huyo dola 36,000 kama fidia ya mshahara, dola
20,000 za usajili na dola milioni mbili kama fidia ya kuvunja mkataba wa miaka
miwili, jumla ni dola milioni 2.1 (zaidi ya shilingi bilioni 3.6)








0 COMMENTS:
Post a Comment