Kiwango ambacho amekuwa
akionyesha kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ kimewafanya wachezaji wenzake
kukubali kuwa sasa amekuwa “mtamu” kuliko hata Mcharo wa Airtel.
Barthez alionyesha kiwango
cha juu, juzi Alhamisi alipokuwa akiitumikia klabu yake ya Yanga katika Uwanja
wa Sokoine mkoani hapa kwa kupangua michomo mikali iliyokuwa ikipigwa na
washambuliaji wa Prisons.
Mpaka sasa, Barthez ameshacheza
mechi sita bila kufungwa, ambapo ni sawa na kusema ametumia dakika 540 bila
kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Hali hiyo iliwafanya baadhi
ya wachezaji wenzake wammwagie sifa kwa kazi yake hiyo kwa kudai kuwa kwa sasa
ndiye kipa bora hapa nchini kutokana na rekodi yake anayoishikilia.
Barthez anashikilia rekodi
ya kufungwa bao moja tu katika mechi nane alizoitumikia klabu hiyo tangu
alipoanza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo mwanzoni mwa
Januari katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Nahodha wa Yanga, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, amesema kwa sasa Barthez ndiye kipa bora hapa nchini kutokana
na kiwango chake cha juu anachoonyesha uwanjani tangu alipoanza kupata nafasi
katika kikosi cha kwanza.
“Barthez kwa sasa yupo
vizuri, anafanya kazi yake ipasavyo, hakika kwangu mimi hivi sasa ndiye kipa
bora kwangu.”
Yeyey Barthez alisema: “Namshukuru
Mungu kwani yeye ndiye anayeniongoza mimi kuwa katika kiwango hiki, lakini pia nawashukuru
viongozi wangu wote wa benchi la ufundi kwa kuniamini na kuamua kunipatia
nafasi hiyo, nitaendelea kujituma zaidi ili niweze kuwa bora zaidi siku zote.”







0 COMMENTS:
Post a Comment