Kiwango bora alichoonyesha Mrisho Ngassa katika mechi tatu zilizopita kinazidi kumshindilia mshambuliaji Mliberia,
Kpah Sherman katika benchi.
Hali hiyo inaweza sasa kumfanya straika huyo aliyesajiliwa
kutoka Klabu ya Centikaya TSK ya Cyprus barani Ulaya kutamani kuondoka baada ya
kupoteza nafasi yake katika kikosi hicho ambayo imechukuliwa Ngassa.
Ngassa alimpora Sherman nafasi hiyo tangu alipoingia
uwanjani akitokea benchi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar
na kuifungia Yanga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0.
Tangu siku hiyo, Ngassa amekuwa akianzishwa katika kikosi
cha kwanza cha timu hiyo na kumwacha Sherman, ambaye awali alikuwa tegemeo.
Katika mechi ya juzi Alhamisi dhidi ya Prisons, Sherman
alisugua benchi mwanzo mwisho ikiwa ni mara yake ya pili tangu ajiunge na
kikosi hicho kwenye usajili wa dirisha dogo la msimu huu.
Mara ya kwanza ilikuwa katika mechi ya kimataifa dhidi ya
BDF XI ya Botswana kwenye Kombe la Shirikisho Afrika lakini aliingia baadaye
kuchukua nafasi ya Andrey Coutinho kipindi cha pili huku Ngassa akimaliza
dakika zote 90.
Hali hiyo hakika inaonekana kumuumiza kichwa mchezaji huyo
kutokana na Ngassa hivi sasa kuwa katika kiwango cha juu.
Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwassa
'Master', alimtetea straika huyo kuwa mabadiliko waliyoyafanya ni ya kawaida
kwa timu yao ikiwa ni moja ya mbinu wanazofanya wakati wa kusaka ushindi.
“Unajua Sherman hakufunga katika michezo kadhaa aliyocheza
na hilo haliwezi kuondoa ubora wake, tulichokifanya ni kumpa nafasi mchezaji
mwingine katika mbinu zaidi za kusaka ushindi, ni mabadiliko ya kawaida,”
alisema Mkwassa.
Lakini katika michezo miwili ambayo Ngassa ameanza, Yanga
imevuna ushindi, iliilaza BDF kwa mabao 2-0, yote yakifungwa na raia wa
Burundi, Amissi Tambwe kabla ya juzi kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya
Prisons.







0 COMMENTS:
Post a Comment