SISI ni binadamu, kila mmoja anaweza kuwa na ufahamu wake tofauti kuhusiana na jambo fulani, hali kadhalika katika utafsiri wa mambo pia.
Jambo linaweza kuonekana zuri upande mmoja, likaonekana ni baya upande mwingine na kila sehemu wakashikilia msimamo wao wakiamini hiyo ilikuwa ni sahihi na kusiwe na mabadiliko.
Dunia ya watu wanaopishana mawazo, halafu wakajadili na kufikia kuungana pamoja, ndiyo yenye nafasi ya kupiga hatua kwa kuwa kunakuwa na muunganiko wa mawazo na kila baada ya mjadala watu wanajifunza na kuimarika zaidi kiuelewa.
Ijumaa iliyopita, Gazeti la Championi lilichapisha picha za mechi ya Simba dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam zikionyesha beki Juma Nyosso wa Mbeya City akifanya vitendo visivyo vya kiungwana kwa mshambuliaji Elius Maguri wa Simba.
Picha hiyo ilizua mjadala mkubwa, wako wakiwemo wanahabari ambao walipiga simu na kutuma ujumbe mfupi wakipongeza sana kuhusiana na picha hiyo.
Lakini wako walifanya hivyo na kulaumu sana kuhusiana na hilo.
Waliopongeza, walisema imesaidia kuonyesha wachezaji wengine wasivyojitambua, badala ya kucheza soka kwa ujuzi, wanaendekeza upuuzi kama ule wa Nyosso. Lakini wako walilaumu na kudai, gazeti ndiyo lilimdhalilisha Maguri!
Haya ni makundi mawili ya wasomaji wa gazeti hili, kwangu yote niliyachukulia kama maoni sahihi kwa kuwa kila mtu ana haki ya kufikiri anachoona sahihi lakini pia akawa anakosea.
Mwandishi wa gazeti hili, alifanya mahojiano na Maguri, mara tu baada ya gazeti kutoka Ijumaa. Mshambuliaji huyo alielezwa wazi kutokana na kukerwa na picha hiyo lakini akasema aliona bora itoke ili watu na wadau wa michezo waone namna watu wasivyo waungwana na hawachezi soka badala yake mambo ya kijinga.
Maguri aliuliza swali: “Mfano kama vile nisingeshikwa, nikaenda na kumfikia Nyosso, halafu ningempiga ngumi. Lazima waandishi mgesema mimi ni mtukutu, sijitambui au vinginevyo, sasa mmeona wenyewe.”
Kweli tumeona wenyewe, hakuna anayeweza kubisha kwamba jambo hilo ameliona kwenye Championi. Sasa kama isingetolewa na gazeti lako hili bora la michezo, ungeliona wapi suala hilo? ungejuaje kama kwenye soka huo upuuzi bado unaendelea?
Msomaji mmoja alituma maoni yake na kusema katika soka hayo ni mambo ya kawaida kabisa, hivyo hakukuwa na haja ya kuonyesha. Hivyo anaunga mkono tabia za kipuuzi kama hizo? Basi, tukaheshimu maoni yake, hata kama yanashangaza na kushitua kabisa.
Kwenye swali la Maguri kuhusiana na kama angempiga Nyosso ngumi tungemuona ni mjeuri, asiye mstaarabu na hata angesema amefanyiwa hivyo hakuna ambaye angemwamini, hilo halina ubishi.
Kabla Maguri hajaingia matatizo, gazeti lako bora la michezo limekuonyesha kwamba kuna tatizo, hupaswi kuamini Maguri kadhalilisha, unapaswa kufikiri na kuamini aliyedhalilishwa ni Nyosso kwa kuwa alichokifanya kwa mchezaji kama yeye mkongwe tena aliyewahi kuitumikia Simba, yenye mashabiki wanaomthamini, hakupaswa kufanya hivyo.
Kama ni mtu atakuwa amedhalilika basi ni Nyosso kwa kuwa familia yake itajiuliza vipi anaweza akafanya vitendo vya kijinga katika umri huo.
Pia ukitaka kujua kwamba picha hiyo itakuwa ni mapinduzi, Rais wa Simba, Evans Aveva amesema wamefungua mashitaka TFF, wasingefanya hivyo bila hiyo picha.
Nahodha wa Simba, Hassan Isihaka akihojiwa na Azam TV mara tu baada ya mechi dhidi ya Ruvu JKT, pia alilaani kitendo hicho. Hii ni sehemu ya kuonyesha msaada wa picha hiyo.
Championi hawakuwa waoga na kuingia kwenye msemo wa mficha maradhi kifo kitamuumbua.
Kusubiri kifo kituumbue ni makosa wakati ni lahisi kukiweka hadharani na mwisho kikatafutiwa dawa.
NIMESHANGAA NA JINSI mAGURI ALIVYOTULIA NA KUJIULIZA KAMA KWELI KILINASIA
ReplyDelete