Na Saleh Ally
BAADA ya African Sports
kupata uhakika wa kurejea Ligi Kuu Bara, haraka nilipiga hodi kwenye ofisi za
Bin Slum Tyres Ltd, nikitaka kujua mikakati hasa ya uongozi wa wadhamini hao.
Nilitaka kujua wadhamini
hao watafanya nini baada ya kufanikiwa kuipandisha African Sports ‘Wana
Kimanumanu’, moja ya timu kongwe kabisa katika soka nchini.
Kurejea kwa African Sports
katika Ligi Kuu Bara, maana yake Mkoa wa Tanga unakuwa na timu tatu, nyingine
ni Coastal Union na Mgambo FC.
Lengo la kuwahi kuzungumza
na uongozi wa Bin Slum ilikuwa ni kutaka kujua baada ya kuipandisha African
Sports sasa wanafanya nini kuhakikisha wakiingia ligi kuu, basi wanakuwa sawa
kweli.
Majibu ya Mkurugenzi
Mtendaji Mkuu wa Bin Slum, Nassor bin Slum, yalinishtua baada ya kusema ameiacha
African Sports iendelee na mambo yake.
Bin Slum alisema haya: “Kweli
nikueleze kidogo tunaweza kuwa na mtazamo utakaowashtua wengi. African Sports
tumekuwa nao bega kwa bega tangu madaraja ya chini, sasa wapo Ligi Kuu Bara.
“Mdogo wangu (Mohammed)
ambaye ni mmoja wa wakurugenzi ndiye alikuwa akihusika na udhamini wa African
Sports kwa kuwa yeye ni mwanachama huko. Mimi ni Coastal Union.
“Ila tulichoamua ni
kuwaacha African Sports wapate wasaa wa kuingiza fedha sasa. Unajua hatukuwa
tukifanya vile (kuwasaidia) kwa lengo la kufanya biashara.
“Sisi wote kwetu ni Tanga,
leo kama kampuni tumeonyesha upendo wetu kwa Coastal Union na baadaye African
Sports. Sasa timu zote kongwe zimerudi ligi kuu.
“Tunawaachia African Sports
vifua vyao (upande wa mbele wa jezi), ili wapate wadhamini ambao wataweza
kuwekeza na kutoa fedha.
“Unajua wakati Coastal
ikiwa inapigania kupanda daraja, hakuna aliyesema lolote zaidi ya kutuachia
tupambane.
“Lakini ilipopanda, maneno
yakaanza na ajabu wengi wanaodai wanaipenda timu wakajitokeza na kuanza kulaumu.
Sasa hatutaki hilo lijirudie tena kwa African Sports halafu tuingie kwenye
malumbano.
“Kama ni upendo wetu wa
kutafuta na tulichopata tumekirudisha mkoani kwetu kwa kupambana kuhakikisha soka
linarejea na kuzirudisha timu zote kongwe, tunaona ni jambo jema kabisa na vema
tuishie hapo,” anasema Bin Slum.
Umeyasikia maneno ya bosi mkubwa wa Bin Slum? Huenda ingekuwa
jambo zuri kama angeendelea, lakini hofu ya kugeukwa na watu kutokuwa waungwana
inamuondoa.
Pamoja na yote, bado
hauwezi kuipongeza familia ya Bin Slum kutokana na ilivyoweza kujitolea kwa
mkoa ambao imetokea. Kweli wapo kwa ajili ya kuchuma katika Jiji la Dar es
Salaam.
Kwetu sote, mimi wewe na
wengine, tunaisaidia mikoa yetu kuinuka kimichezo? Kila mmoja anapaswa
kujitathmini kupitia mtihani huo wa Bin Slum.
Leo wamechangia kuifanya
Tanga kufikisha timu tatu, heshima ya kisoka katika mkoa huo sasa imerejea na
wana timu zinazotoa ushindani sahihi.
Wangapi wanatokea Rukwa,
Kigoma, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora na kwingineko ambako mikoa yao imedorora
kisoka na haina hata timu?
Si kila mkoa lazima utakuwa
na timu, lakini bado msaada kwa soka hata kupitia vijana bado unaweza kuwa
sehemu ya kuonyesha mnaijali mikoa mliyozaliwa, mikoa yenu ya asili.
Unaweza kujitangaza Dar es
Salaam na Tanzania nzima huku ukiusaidia Mkoa wa Mwanza, Shinyanga au Tabora.
Kampuni ya Bin Slum Tyres
Ltd imeonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa Mkoa wa Tanga. Lakini uzalendo wake
upo juu hata katika mikoa mingine na hii inaonyesha ni biashara yenye upendo
ndani yake, hivyo wengi wanapaswa kuiga na inawezekana, kikubwa kuamua na
kuondoa hofu.
Watanzania pekee kupitia wadau
na kampuni kama hiyo ya Bin Slum Tyres Ltd, ndiyo wanaoweza kuubeba mpira wa
Tanzania. Tukisubiri watu watoke nje ya mipaka yetu, tutajidanganya.
0 COMMENTS:
Post a Comment