Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal ameamua kuweka wazi
mipango yake ya kustaafu kufundisha soka ambapo amesema klabu hiyo ndiyo ya
mwisho na baada ya hapo ataachana na kazi ya ukocha.
Van Gaal, 63, amesema hayo muda mfupi kabla ya mechi dhidi ya Liverpool
ambayo inatarajiwa kupiga kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Anfield.
Kocha huyo raia wa Uholanzi ameweka wazi kuwa nia yake kwanza ni
kuhakikisha United ambayo inamiliki Uwanja wa Old Trafford inapata mataji kisha
ndiyo atang’atuka.
“Umri umesogea, hii itakuwa kazi yangu ya mwisho, nahitaji kuwa
karibu na watoto wangu, wajukuu wangu na mke wangu.
“Wanastahili kuwa karibu yangu, sasa hivi siwezi kuwa karibu nao
mfano nilikosa sherehe ya kuzaliwa ya mjukuu wangu, sikupenda,” alisema kocha
huyo.
Kuhusu mwelekeo wa timu yake, alisema: “Tunao ubora wa kucheza Ligi
ya Mabingwa, kuna maendeleo ya timu kadiri siku zinavyosogea.
“Nahodha wangu, Wayne Rooney ni mwepesi wa kuelewa, sijui kama huwa
anazungumza na mkewe kuhusu soka, ninachomaanisha ni kuwa wachezaji wangu wengi
ni watu waelewa.
“Mfano mwingine ni Michael Carrick naye ni zaidi ya mchezaji, anajua
vitu vingi na anapenda kuzungumza kuhusu mbinu, nafurahi kufanya kazi na
wachezaji waelewa.”
0 COMMENTS:
Post a Comment