JUMAPILI
saa 10 jioni, watani wa jadi Yanga na Simba wanakutana tena kwa mara nyingine
msimu huu. Kwa hesabu za kawaida watakuwa wanakutana kwa mara ya tatu katika
msimu mmoja na mara ya kwanza kwa mwaka huu.
Nimesema
mara tatu kwa kuwa naunganisha mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika
kwa sare ya bila mabao, ilipigwa Oktoba 18, 2014.
Katikati
kuna mechi moja ni ya kirafiki lakini maarufu kama Nani Mtani Jembe ambayo
ilipigwa Desemba 13, 2014 na Simba wakaibuka na ushindi wa mabao 2-0 na
kuchukua kikombe.
Sasa
wanarudi kwenye ligi na hesabu za kitaalamu zinaonyesha kwa msimu huu hakuna
mbabe kwa kuwa mechi ya kwanza ilikuwa na sare ya bila bao. Hivyo kila timu
pamoja na kuwa inatafuta pointi tatu muhimu lazima ijue hakuna ambayo imeifunga
nyingine au kushinda katika msimu wa 2014-15.
Ndiyo,
hakuna ubishi kwamba Yanga na Simba wanasaka pointi tatu muhimu, Simba wanataka
kujikomboa kutoka katika hali ya kusuasua na Yanga wanataka kuendeleza hali yao
ya kasi ambayo imeanza kuonekana.
Ushindi
ndiyo furaha na faraja ya kila upande lakini ukirudi katika hesabu, kila upande
unazitaka pointi tatu zake ili kujiongezea katika msimamo. Yanga ndiyo vinara,
inajua kila timu yaani 13 zilizobaki Ligi Kuu Bara zinaifukuza, lakini Simba
pia inataka kupanda hadi ‘Top 2’ ikitokea nafasi ya nne.
Yanga
ina pointi 31 kileleni, Simba ina 23. Ingawa pengo la pointi ni kubwa lakini
kila upande unataka kupata pointi hizo tatu ili kujiimarisha kutokana na
malengo zilizojiwekea. Yes! Kila upande unataka uzipate pointi tatu tamu kuliko
zote za ligi kwa Yanga na Simba.
Wakati
Yanga na Simba wanawaza kila wanalotaka, mfano ujiko, furaha, kupoza presha
upande wa viongozi, makocha na wachezaji au umuhimu wa pointi tatu, bado
tukubaliane mechi hiyo inapaswa kuwa mfano kwa kuwa ndiyo taswira ya soka
nchini.
Tunajua
kuna Azam FC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na timu nyingine ambazo zimekuwa mfano
wa kuigwa kutokana na mambo kadhaa mazuri zinayofanya, lakini pia tukubaliane,
wakongwe hao wanapaswa kupewa nafasi yao na hilo halipingiki hata kidogo.
Wakikutana
watani hao, mambo mengi yanasimama kwa lengo la kuwashuhudia wakifanya mambo
yao. Sasa wanachofanya nini, hapa ndiyo ninaposisitiza kwamba taswira iwe kweli
wakongwe au baba wa mpira wa Tanzania wanakutana.
Kuanzia
uwanjani, soka liwe la uhakika, mechi ichezwe kwa kiwango ambacho yeyote awe wa
Tanzania au nje, aamini kweli wakongwe wa mpira wa Tanzania wamekutana na si
kupaniana, ugomvi, kuzozana au kuchezeana rafu za mchangani.
Wachezaji
wanapocheza mechi hizo za watani wamekuwa wakicheza katika kiwango duni
kutokana na uoga, kwamba wana hofu ya kuonekana wamehujumu hasa kama wakipoteza
mpira.
Hilo
si sahihi na kama timu itacheza kwa woga kila mmoja akitaka kumpa mpira
mwenzake kioga na si kwa mipango, soka ya Tanzania itakuwa ni kwa ajili ya
kuchekesha tu.
Hivyo
wachezaji lazima waonyeshe uwezo na kuthibitisha kweli wanastahili kucheza
katika timu hizo kongwe zilizobeba mioyo ya watu wengi wanaopenda soka nchini,
hivyo kiwango ni jambo namba moja.
Wachezaji
na viongozi, kumbukeni Watanzania wengi na hasa mashabiki wa soka hawana
kiwango cha juu cha kipato.
Wanapojipinda
na kuja kushuhudia mechi yenu, basi wanakuwa wamejichanga kupita kiasi na
wengine wanasafiri kutokea mikoa mbalimbali ya Tanzania, basi wapeni burudani
wanayostahili na si vituko ambavyo wakivihitaji, wataangalia runinga hasa
vipindi vya wachekeshaji kama Kingwendu au King Majuto.
0 COMMENTS:
Post a Comment