Baada ya kuibanjua Mgambo JKT mabao 2-0, Kocha
Mkuu wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, amefunguka kuwa Yanga ndiyo timu
bora kwa sasa kutokana na matokeo mazuri wanayoyapata.
Yanga juzi Jumamosi iliwaadhiri Mgambo JKT kwenye Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga kwa kuwafunga mabao 2-0 yaliyofungwa kwa vichwa na Mrundi,
Amissi Tambwe pamoja na kiungo mshambuliaji, Simon Msuva.
Yanga chini ya kocha huyo imefanikiwa kushinda
michezo yote mitano ya Ligi Kuu Bara iliyocheza nje ya Jiji la Dar es Salaam na
kuweka rekodi ya kipekee.
Ilishinda dhidi ya Mbeya City na Prisons kwenye Uwanja wa
Sokoine, Mbeya kabla ya kuitungua Polisi Moro katika Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro, kisha kuzifunga Mgambo na Coastal kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya
Ghana, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, Yanga ndiyo timu bora kwa sasa
kutokana na kucheza vizuri katika kila mchezo.
“Tumecheza
vizuri katika mchezo huu, mara zote huwa tunacheza hivyo, ndiyo maana tunapata
matokeo chanya, Yanga ndiyo timu bora, sisemi kwa sababu ni timu yangu bali
matokeo yanathibitisha hilo.
“Mechi inayokuja tutacheza na Ruvu, ni timu
ngumu lakini tunachotaka ni kushinda kila mchezo ili kusafisha njia ya ubingwa
mwishoni mwa msimu na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa,” alisema
Pluijm.
Yanga ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobaki
katika michuano ya kimataifa ambapo inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho na
wikendi ijayo itapambana na FC Platinum nchini Zimbabwe. Awali, Yanga iliifunga
timu hiyo mabao 5-1 jijini Dar.







0 COMMENTS:
Post a Comment