UKINIKATAZA kusema ukweli utakuwa unapoteza
muda kwa kuwa lazima nitasema bila ya hofu yoyote.
Wote mnajua, katika michezo, hasa upande wa
wadau wa soka kuna msiba mzito wa Kocha Sylvester Marsh ambaye amefariki dunia
juzi akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Kifo cha Marsh ni pigo jingine katika mchezo
wa soka nchini kwa kuwa amekuwa mmoja wa makocha wazalendo wachapakazi na wenye
juhudi za makusudi za kuendeleza mchezo huo.
Unakumbuka alifanya kazi chini ya makocha
Jan Poulsen na baadaye Kim Poulsen, wote wakiwa wanatokea nchini Denmark na
kuvinoa vikosi vya Taifa Stars na Kilimanjaro Stars.
Hakuna kocha kati ya hao aliyewahi
kulalamika kuhusiana na utendaji wake kwamba ni wa kiwango cha chini.
Marsh alikuwa anaipenda kazi yake,
alionyesha anaipenda nchini yake na alitaka mabadiliko. Hakuna ubishi,
ameondoka akiwa na ndoto lukuki za kuleta maendeleo katika mchezo wa soka.
Uthibitisho kwamba alikuwa ana ndoto kibao
ni kile kituo chake cha kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto wa Kitanzania
kilichopo jijini Mwanza.
Alifanikiwa hadi kupata baadhi ya wafadhili
kutoka nchini Ujerumani ambao walijitolea kufanya kazi naye. Lakini ameondoka.
Kifo hakina mwenyewe, hakikwepeki, ni amri
ya Mwenyezi Mungu na haina makosa. Lakini narudia leo baada ya kuwa nimeandika
Ijumaa kuhusiana na kuugua kwake, kuwa tumepata funzo.
Ugonjwa wa Marsh ulitupa somo, kifo chake
kimetupa somo zaidi kwamba mchezo umejaa lundo la wanafiki ambao sasa wataanza
kusema pengo lake halitazibika.
Mchezo wa soka umejaa wadau lundo wanafiki
wanaoweza kuonyesha upendo kupitia macho yao, midomo yao kwa kuwa watatengeneza
matabasamu ya uongozi lakini katika mioyo yao, kamwe si wakweli na hawana
upendo hata kidogo.
Wakati wa ugonjwa wa Marsh wachache
waliojitokeza kumuona, wachache walioona anastahili kusaidiwa. Lakini leo
ameondoka duniani, wengi watajitokeza kusifia mambo yake, kusifia ukaribu wake
na ikiwezekana juhudi zake.
Unafiki ni jadi katika soka? Ujanja ujanja
na ubabaishaji wa wadau wengi wa soka upo hata katika afya au mambo ya msingi
kama vile alivyougua Marsh? Sasa kaondoka, ndiyo wakati mzuri wa kuonyesha sura
zenu na kumsifia?
Ni vema kusubiri hadi mtu apoteze maisha ili
kuanza kumsifia kwa alichokifanya? Au vema kupambana kuokoa maisha yake?
Jamani, lazima tuone aibu, tuwe waungwana wa dhati na si maneno tu mdomoni.
Marsh ameondoka kwa ugonjwa wa kansa, nani
kati yetu ana uhakika ni mzima? Yupi anajua ataondoka lini na kwa nini
tunashindwa kuwa wakweli?
Wakweli wachache wanaonekana wabaya! Mchezo
wa soka una sura ya kinafiki, umejaza watu wengi wabinafsi na wenye nafasi za
uongozi katika klabu, vyama na hata shirikisho la soka wanaonekana wazi
wanajiangalia wao na si maendelo ya mchezo huo na lazima mkubali bila ya
upendo, kamwe maendeleo hayatapatikana.
Lengo langu si kutaja watu, unajijua,
utajipima mwenyewe. Lakini yaliyomkuta Marsh kuanzia ugonjwa, kusumbuka fedha
ya matibabu yalikuwa maumivu ambayo jibu lake ni kilichotokea. Kumbuka, hata
wewe siku moja yanaweza kukuta.
Mwache Marsh atangulie, kwa kuwa njia yetu
ni moja nasi tutamfuata siku yoyote Mwenyezi Mungu akiidhinisha lakini kati
yetu, hakuna anayejua kifo chake kitakuwaje.
Ndiyo maana nilitamani kuona wote mnapeleka
mioyo yenu katika matengenezo upya ili muweze kutambua maana ya upendo wa dhati
kuliko sasa mnavyotambua kwa dhati maana ya unafiki wa dhati.
that was great man
ReplyDelete