March 30, 2015


Uongozi wa klabu ya Yanga umesema kiungo wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, anawachezea akili kutokana na madai yake ya kutaka kuondoka katika klabu hiyo huku akiwa tayari ameshafanya mazungumzo ya awali na timu hiyo.

Hivi karibuni Ngassa kupitia gazeti hili alieleza kuwa ana asilimia 3 pekee za kubaki katika klabu hiyo kwa madai kuwa tayari ameshapata klabu nyingine anazofanya nazo mazungumzo katika nchi za Qatar, DR Congo na Afrika Kusini.

Sakata hilo la Ngassa na klabu yake hiyo liliibuka kufuatia madai ya kukataliwa kusaidiwa kulipiwa deni lake kiasi cha shilingi milioni 45 anazodaiwa na benki ikiwa ni kama adhabu ya TFF kutokana na kusaini timu mbili.

Kiongozi mmoja mkubwa wa Yanga ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema wanashangazwa na kauli za mchezaji huyo kutoa malalamiko kwenye vyombo vya habari kuwa hafanyiwi haki katika kulipa deni lake hilo na kudai anataka kuondoka klabuni hapo akiwa yupo ndani ya mazungumzo na uongozi huo kwa ajili ya kuongeza mkataba.

“Mazungumzo kati ya Ngassa na Yanga yalianza tangu Oktoba ambapo kwa sasa ana mkataba wa awali wa kuongeza mkataba mwingine na mazungumzo bado yanaendelea baina yetu na yeye, tunashangaa kuona anazungumza ovyo.

“Tunazungumza naye kwa ajili ya kuongeza mkataba wa miaka miwili, kama amepanga kuondoka basi anaweza kuondoka hata leo, kitendo anachokifanya siyo cha ki-professional kabisa na ndiyo maana Ulaya klabu zimekuwa haziongei na wachezaji na badala yake wanazungumza mawakala.

“Kama kuna kitu anakihitaji kiongezwe kwenye mkataba wake basi ni vyema angekaa na uongozi na kulizungumzia suala lake kwani tayari tuna mazungumzo naye ya awali na anachokifanya yeye hivi sasa ni uswahili tu.

“Yanga imekuwa na desturi ya kuwajali wachezaji wake ambapo kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa wakineemeka na Yanga, mfano mzuri kapteni, ‘Cannavaro’ (Nadir Haroub) amekuwa ni miongoni mwa wachezaji wanaotakiwa kuigwa kwani amekuwa hana matatizo yoyote na klabu na uongozi unampa kipaumbele kutokana na nidhamu anayoionyesha na haumsikii akisema suala lake hata siku moja.

“Wachezaji wanadhani kuchezea klabu nyingi katika ligi ndiyo usupastaa, hilo si sawa, mchezaji anatakiwa atulie katika timu moja ili awe ‘elected’ na hatimaye kuwa vizuri na si kama hivyo ilivyo,” alisema bosi huyo wa Yanga.


1 COMMENTS:

  1. Million 45 mlizomuahidi ( CRDB ) mmemlipia?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic