Timu ya Coastal Union ya Tanga,
inaweza kuwa imeingia kwenye mtihani mzito baada ya kudaiwa kuwa kipa wake
namba moja, Shabaan Kado, kagoma na kaondoka klabuni hapo kutokana na sababu
mbalimbali.
Imeelezwa kuwa chanzo kikubwa cha
yote hiyo ni kwamba kipa huyo hajafurahishwa na hali ya maisha yake ya sasa
klabuni hapo ikiwemo kushutumiwa kwa baadhi ya mambo yanayoenda kombo klabuni
hapo kwa sasa ikiwa ni pamoja na kutupwa benchi katika mechi mbili za mwisho za
timu hiyo dhidi ya Ruvu Shooting na Azam FC na nafasi akapewa Fikirini Mapala.
Mtu wa karibu na Kado kutoka kikosini
hapo alilijuza blogu hii kuhusiana na tukio hilo na kueleza ukweli
kwamba Kado hajafurahishwa na vitendo hivyo, ndiyo maana ameamua kuondoka Tanga
kwa siku ya tatu sasa na kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kutuliza akili.
“Huku mambo si shwari sana, Kado
ameamua kuondoka hapa na amekwenda Dar kutuliza akili, anadai kwamba amechoshwa
na baadhi ya maneno yanayoelekezwa juu yake kutokana na hali ya timu ilivyo
sasa, mechi za Ruvu na Azam pia hakudaka na akajaribiwa kipa mwingine, hivyo
hayo yote anaona bora ajitenge kwanza kwa sasa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Kado mwenyewe
kuzungumzia suala hilo, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi
kutokuwa hewani lakini Meneja wa Coastal, Akida Machai alisema:
“Hapana, Kado hajaondoka kwa
ubaya wowote hapa, alinitumia meseji kwenye simu yangu kwamba anaondoka kwenda
Dar kumuangalia bibi yake anaumwa na kisha atarudi mapema kuja kuendelea na
timu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment