April 18, 2015


Na Saleh Ally
KUMBUKUMBU inaonyesha, Etoile du Sahel iliipiga Esperance kwa mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tunisia mwaka 2011. Ikaifunga 3-1 msimu wa 2013.
Hauwezi kusema ni timu laini, huu ni mfano kuonyesha Yanga inakutana na timu ngumu sana katika mechi ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, leo.


Haitakuwa rahisi, Yanga wana kikosi kizuri lakini Waarabu ni wajanja na wazoefu wa michuano ya kimataifa.

Wanajua wacheze vipi mechi za nyumbani na wafanye nini katika mechi za ugenini. Kikubwa lazima Yanga wajiamini, wacheze kwa kasi ili kuwapa wakati mgumu Etoile kwa kuwa wengi wana maumbo makubwa.
Pia wanachotakiwa kubadilika Yanga ni kuhakikisha wanatumia nafasi zote wanazozipata kama itawezekana ili washinde kuanzia mabao matatu kwenda juu.

Pamoja na kuwa Yanga wana mipango yao, lazima wategemee mengi waliyoyatarajia na wasiyoyatarajia kutoka kwa Waarabu hao na haya saba, lazima utayaona leo Taifa, Etoile ikijaribu kuishinda Yanga. Hivyo lazima Yanga wawe imara kweli kupambana nayo na kuvunja au kuvuruga mipango hii ili wawamalize Waarabu hao wa Kaskazini.


Kupoozesha:
Lazima Etoile watafanya kila linalowezekana kucheza mpira wa taratibu kama vile wako mazoezini.
Watafanya hivyo ili kuwatoa Yanga mchezoni, wanajua wao watataka kucheza mchezo wa kasi ili kupata mabao wakiwa nyumbani.
Lakini Etoile watakuwa wakigonga pasi taratibu kama hawataki au wasiokuwa na haraka. Yanga wakiwafuata, wamekwisha:

Cha kufanya: Yanga ni kukaba kwa nguvu, kuwapa presha kuhakikisha mpira hawabaki nao ili wauchukue na kuwakimbiza.

Vichwa:
Etoile wanaweza wasifike mara nyingi langoni mwa Yanga. Lakini mara nyingi mipira yao ni krosi, wanafanya hivyo wakijua wana miili mikubwa na wazuri kwa vichwa.

Alkhail Bangoura raia wa Guinea na Baghdad Bounedjah pamoja na Kaddour Beldilali raia wa Algeria, ni kati ya wachezaji hatari wa mipira ya vichwa.
Yanga wanapaswa kuwa makini kwa kuwa wakiruhusu krosi kumi kwa kipindi kifupi na wakazubaa, wajue wataumia.

Cha kufanya: Lazima mabeki wa pembeni, viungo wa pembeni warudi mapema kukaba na ikiwezekana wazuie krosi zisipite au kupunguza wingi wa krosi zinazokwenda langoni mwao. Kingine, kila mpira wa krosi, mabeki wa Yanga lazima wawe wa kwanza kufika na kupiga.


Muda:
Kujiangusha kwa kuguswa kidogo tu ni kawaida ya Waarabu hao. Faida ya kujiangusha kwa Etoile ni kubwa kwa mambo mawili.
Moja; kupoteza muda kwa kuwa ndiyo nia yao. Pili; kuwavuruga Yanga kisaikolojia, wanajua wakiona Waarabu hao wanajiangusha, watapaniki na kuondoka mchezoni kutokana na kupandwa na jazba wakilaumu kwa nini wanapoteza muda.

Cha kufanya: Mapema nahodha amkumbushe mwamuzi jamaa wana tabia za kujiangusha. Wakifanya hivyo, wamkumbushe tena na ikiwezekana, wakubali kuwa watumwa, wawape mipira au kuwawekea katika eneo la goli ili wapige haraka.
Ingawa jambo sahihi kabisa kwa Yanga ili kumaliza tatizo hilo ni kuwatandika mabao mawili ndani ya dakika 30.
Hiyo itapunguza wao kupoteza muda, watafunguka na Yanga inaweza kupata nafasi zaidi.

10 nusu uwanja:
Sayansi ya soka inasema kila watu wengi wanapokuwa kwenye uwanja mdogo, ugumu kiuchezaji unaongezeka. Hii ni sayansi inayotumiwa sana na timu za Waarabu zinapokuwa ugenini.

Ukijumlisha na kipa, wachezaji wengine tisa, maana yake 10 watarudi na kukaa kwenye upande (zone) wao.
Kama Yanga itapandisha wachezaji 10 kushambulia, maana yake ile nusu uwanja moja itakuwa na wachezaji 20. Hii inaongeza ugumu kwa Yanga ambao watakuwa wakipambana kupata bao.

Utaona wachezaji wenye kasi kama Msuva na Ngassa wanakuwa si tatizo sana kwa Waarabu hao.

Cha kufanya: Lazima Yanga wawe wamejiandaa na pasi za haraka za chini, pia wawe wamejipanga kupiga mashuti ya kushtukiza yenye watu wanayoyafuatilia kama kipa ametema. Pia kama wamejiandaa na mipira ya adhabu au ‘mipira iliyokufa’, wana kila sababu ya kutafuta faulo karibu na eneo la 18, ikiwezekana ndani.

Kushtukiza:
Pamoja na kwamba wako ugenini, Waarabu hawawezi kuwa wajinga, kwamba wasubiri kujilinda tu hadi watakapokwenda kwao ndiyo watashambulia na kufunga.

Utawaona wakianza kwa kushambulia kwa kasi kidogo kutafuta mbinu ya kupata bao angalau moja, wakipata watataka la pili.

Wakiona Yanga wana mashambulizi makali, watarudi nyuma na kutumia plan B, kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Cha kufanya: Yanga lazima wawe makini, kwani wakifungwa tu, basi wameharibu mambo. Dawa ni kuwashambulia kwa kasi muda wote ili wawazuie Waarabu hao kushambulia sana na kushitukiza.

Dead balls:
Timu nyingi za Kiarabu kutoka Tunisia, Algeria, Misri na Morocco, zimekuwa na wapigaji wazuri wa mipira ya adhabu ndogo, maarufu kama “dead balls”.
Kwa kuwa wanajua wana wapigaji bomba wa mipira iliyokufa, kikubwa wanajitahidi sana kutafuta faulo nje ya 18. Unajua, wakiipata, wamewamaliza.

Cha kufanya: Yanga lazima wacheze kwa kuwasukuma, wahakikishe hawasogelei mara nyingi katika eneo la 18. Pia wajitahidi kucheza na kusababisha faulo kwa kuwa licha ya maumbo yao makubwa, Waarabu wakiingia karibu au ndani ya eneo la hatari, wanakuwa wepesi zaidi ya karatasi!




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic