Katika harakati za kuhakikisha kuwa
wanaendelea kuwa na timu ya mapambano msimu ujao, imebainika kuwa Azam FC
wamemjaza manoti ya Sh milioni 20 taslimu beki wao shupavu, Said Morad kwa
ajili ya kumbakiza kundini.
Mpaka sasa Azam imefanikiwa kuwaongezea
mikataba wachezaji wake wanne, akiwemo Mrundi, Didier Kavumbagu, wazawa Erasto
Nyoni, Gaudence Mwaikimba na Morad.
Kavumbagu aliyeifungia mabao 10 msimu huu
pamoja na Erasto na Morad, wamepewa mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja huku
mkongwe Mwaikimba akichukua wa miezi sita.
Chanzo kutoka ndani ya Azam, kimeeleza kuwa pamoja na fedha hizo, beki huyo ameongezewa mshahara ambao utakuwa mnono.
“Viongozi wanaendelea na mipango ya usajili
lakini ndiyo hivyo, kwanza wamewatuliza hawa wengine mapema, Morad pia alikuwa
anadhaniwa anaweza kuwahiwa na timu nyingine baada ya kumaliza mkataba wake,
ndiyo maana wakamuwahi na kumpa milioni 20 na mshahara wake wa milioni mbili
aliokuwa anachukua hata msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Morad kuthibitisha taarifa
alisema kwa kifupi: “Yaani usajili wangu huu hauna mabadiliko makubwa sana,
siwezi kuweka wazi sana lakini vingi ni vilevile kama ilivyokuwa msimu
uliopita.”
0 COMMENTS:
Post a Comment