Na
Saleh Ally
MSHAMBULIAJI
wa Tottenham Hotspur, Emmanuel Adebayor, ameamua kufunguka kupitia mitandao na
kueleza matatizo kibao yanayowahusu ndugu zake.
Adebayor
ameamua kuweka mambo hadharani baada ya kuchoka kuandamwa mfululizo na ndugu
zake akiwemo mama yake mzazi.
Hadithi
aliyoitupia mtandaoni inasikitisha kusikia dada yake akiipangisha nyumba ya
Adebayor ambayo ameijenga kwa zaidi ya dola milioni 1.5 (Sh bilioni 3).
Akamuacha dada yake aishi hapo, siku aliporejea, akakuta wapangaji.
Alipojaribu
kumuuliza dada yake, akamporomoshea kashfa. Alipomshitakia kwa mama yake naye
akamshushia maneno makali!
Kaka
yake aliomba mtaji, alipompa hakuwahi kuanzisha biashara. Sasa anawasomesha
watoto wake nchini Ujerumani, kila kukicha amekuwa akimshutumu ikiwemo
kumzushia kuwa amechangia kifo cha kaka yake mkubwa, Peter.
Alimpa
mama yake mtaji wa kutengeneza biskuti huku akiruhusu watumie jina na picha
yake ili waweze kuuza. Wakashindwa.
Akachukua
uamuzi wa kumlipia mdogo wake katika ‘academy’ acheze soka nchini Ufaransa.
Miezi michache, akawa ameiba simu 21 kati ya wachezaji 27 aliokuwa akicheza
nao.
Mwaka
2005, akaitisha kikao cha wanandugu na kutaka wamalize tofauti. Alipoomba
ushauri wao, wakamueleza ingekuwa vizuri amnunulie nyumba kila mmoja wao na
kuwa anawalipa mshahara!
Adebayor
ameamua kufunguka. Ukweli huo ndiyo mfumo wa familia zetu nyingi za Kiafrika,
uko hivyo lakini inawezekana ukawa ni tatizo kubwa kiutendaji kwa kuwa sisi
wengi wetu ni wazembe na watu wa lawama.
Baada
ya ujumbe mzito wa Adebayor alioutupia kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook,
nilizungumza na wasanii na wachezaji mbalimbali ambao walikuwa wakielezea
machungu ya kuhusuana na ndugu ambao wanachangia hata wengine kukata tamaa.
Wapo
ambao wameacha muziki au kukwama kisoka kutokana na kuanza kuona kazi zao ni
kero. Wanaathirika kisaikolojia kwa kuanza kuona mafanikio ni kama sehemu ya
kuwaudhi ndugu zao, hivyo bora kuachana nayo.
Wanaofikia
uamuzi huo wakati mwingine hawajui kama wamefikia hivyo. Taratibu wanaanza
kuonekana wanayumba na kwisha kabisa kimchezo au kimuziki. Ndugu lawama
wasiojali mafanikio zaidi ya msaada, wanaweza kuwa kilevi ambacho kinachangia
wachezaji au wanamuziki kuporomoka kwa kiwango chao kiutendaji na mwisho kwisha
au ‘kufa’ kabisa.
Matatizo
ya Adebayor ndiyo matatizo yanayomkuta staa yeyote awe wa muziki au michezo.
Mfano kwa hapa nyumbani, Diamond Platinumz angekuwa muwazi, angeweza kukuambia
ndugu au watu wa karibu wanavyoweza kuwa tatizo.
Kiungo
kinda wa Simba, Jonas Mkude pia anaweza kuwa sehemu ya wale waliowahi kukutana
na “ndugu lawama” ambao ni wavivu na waliojaa lawama. Si unakumbuka hivi
karibuni aliingia mkataba mpya na Simba na kuingiza mamilioni ikiwa ni pamoja
na kupata gari?
Adebayor
ni shujaa zaidi, lakini hili liwe somo kwa wanamichezo, wasanii au hata
waandishi wa habari kwamba maisha ya Kiafrika yana mengi ambayo yanaweza
kuwakwamisha na ndugu wanaweza kuwa sehemu.
Ndugu
wa Kiafrika wanaweza kuwa kama kilevi na kumfanya mchezaji kushindwa kufanya
kazi yake katika kiwango ambacho ni sahihi.
Inawezekana
hata utendaji wa Adebayor umekuwa ukiyumba kutokana na matatizo lundo ambayo
yamekuwa yakimtokea. Ndiyo maana Didier Drogba akamshauri kuishi maisha
anayoona ni sahihi na kuachana na kila mtu anayeamini anamchanganya au kutaka
kumrudisha nyuma.
Kuna
rafiki yangu mmoja, amefanya kila juhudi, kawaleta ndugu zake jijini Dar.
Amekuwa akifanya juhudi ya kuwahudumia kila kitu. Mwisho anaambulia machungu
kila kukicha hali inayomfanya akate tamaa.
Lazima
tukubaliane kuwa ndugu wenye tabia ya kivivu na waliojaa lawama ni watu
wanaozorotesha maendeleo ya michezo, burudani na hata maisha ya kawaida.
Waathirika
wa ndugu wa aina hiyo ni wengi sana, lazima tukubali si Adebayor pekee. Uamuzi wa
ujasiri aliouonyesha, basi unapaswa kuigwa na wengi na kuamini wanaoweza
kukusaidia wanaweza kuwa wachache sana, hivyo hupaswi kuhofia wengi wasiokuwa
na msaada kwako.
Muundo
wa mifumo ya Kiafrika kweli ni tatizo, lakini wachezaji wa Kitanzania au
Kiafrika ambao wamekuwa na hofu kuu hata kutaja kiwango cha mishahara yao
kuwahofia ndugu, sasa wanapaswa kubadilika.
Ndugu
wote hawawezi kuwa wabaya, lakini ni vizuri kuepukana na wengi wasiokuwa na
faida, waache waishi maisha yao, hata kama kusaidia ni muhimu, ishi wewe
kwanza.








0 COMMENTS:
Post a Comment