UONGOZI
wa Azam FC umeamua kumrejesha kocha Stewart Hall kwa mara nyingine kuongoza
benchi la ufundi la kikosi hicho.
Hall
anarejea Azam FC, hii itakuwa ni mara ya tatu baada ya kuondoka au kuondolewa
mara mbili huko nyuma.
Taarifa
nilizozipata ni kwamba, Hall, raia wa England, atasaini mkataba wa kufanya kazi
Azam FC, leo na mara moja ataanza kupiga mzigo. Ninaamini hawatabadili hilo.
Kabla
ya kufikia makubaliano, Hall ameuomba uongozi wa Azam FC kwamba kama unamtaka
afanye nao kazi, basi lazima akubaliane nao kuhusiana na suala la timu ya
benchi la ufundi.
Uongozi
umekubaliana naye na sasa Hall anatua na kikosi chake kizima, akiwemo kocha
bora wa makipa pamoja na mtaalamu wa chakula.
Uhakika
wa hayo tutasubiri leo, tutajua kila kitu. Ninataka kuzungumzia ujio wa Hall
kwa mara nyingine, maana nililazimika kuuliza ili kupata uhakika.
Kwamba
vipi kocha huyo amekubali kurejea tena, lakini anatoa masharti ya kutaka kuwa
na wasaidizi wake mwenyewe? Je, hawaamini waliopo?
Jibu
nililopewa ni kwamba ilikuwa kazi ngumu kwa kocha huyo kufanya kazi zake
kiufasaha na mara kadhaa alikuwa akizozana au kugombana na waliokuwa wakifanya
naye kazi.
Rafiki
wa kocha huyo alinieleza kwamba kulikuwa na mambo mengi ya “Kiswahili”. Watu
walitaka kupeleka mambo ili mradi tu, kitu ambacho Hall hakukubaliana nacho
hata kidogo.
Kitendo
cha kukataa walichokuwa wakitaka, yaani aliotakiwa kufanya nao kazi,
kilisababisha wamuanzishie zengwe na siku ya mwisho uongozi uliamini yeye ni
tatizo, mwisho akaondolewa halafu akarudishwa tena.
Sasa
amekubali kurejea, tena anarejea akiwa na timu ya watu anaowaamini kwamba
watafanya kazi vizuri. Hapa ndiyo nimekuwa nikisema mara kadhaa, ingawa
zinafanyika juhudi kubwa za kuyapinga kwa kuwatumia watu walaini wa fikra ambao
wanakubali kirahisi kuandika lolote.
Kinachoonekana
wanachotaka viongozi wakuu wa Klabu ya Azam FC na wanachokilenga waajiriwa
wengi, kinaweza kuwa ni tofauti, hali inayosababisha wao kama timu kushindwa
pamoja.
Inaonekana
uongozi wa juu wa Azam FC unataka kuwekeza kweli. Unataka mambo yaende
kitaalamu na ndoto walizonazo zifikiwe kwa kuifanya Azam FC kuwa mahiri, kubwa,
gumzo Tanzania na Afrika nzima.
Wafanyakazi
wake wengi wanaweza wakawa na mawazo hayo, lakini shida kubwa yamechanganyika
na mengine ya umimi kwa kuwa wapo wanaotaka kufaidika kwa maisha yao binafsi.
Penye
rikizi hapakosi fitna. Wafanyakazi wao kwa wao badala ya kuungana kama timu,
wamekuwa wakipigana fitina na kusababisha kuifanya Azam FC itumbukie katika
mifumo ileile ya Yanga na Simba, maana yake wanakuwa hawana tofauti tena.
Shida
nyingine unaiona kwamba viongozi wa juu wa Azam FC, wako tayari kusikiliza
maoni, wako tayari kujifunza ili kubadili mambo. Lakini waliopewa majukumu ya
kuendesha klabu hawataki lolote kwa kuwa “wanajua sana!”
Kama
malengo ni kufanikisha mafanikio ya Azam FC, suala la “hii ni rikizi ya nani”
na kila mmoja anaitaka hadi kuingiza “fitna” kila mmoja akimpiga vita mwenzake,
basi klabu hiyo itaishia katika umaarufu walionao Yanga na Simba ambao wao
wanaweza kusema ni timu au klabu za wananchi.
Azam
FC inamilikiwa na familia binafsi, tena wenye fedha na ndoto ya mafanikio,
hivyo wanaofanya kazi hapo, lazima pia wajue bosi au mwajiri wao amelenga nini.
Kama kweli wanapewa kila kitu kufanikiwa maendeleo, basi lazima wakubali
kuachana na tabia zao walizokuwa nazo, halafu wabadilike na kutimiza ndoto
hiyo.
Nasisitiza,
mara kadhaa nimesema kuhusu hili. Mmepinga sana bila ya hoja ya msingi. Sasa
Hall anarudi na kauli ya fitna au chuki inajirudia mara nyingine. Vizuri
mkawasaidia hao waajiri wenu kutimiza ndoto zao kuliko kuangalia zaidi ndoto
zenu za riziki!
Unajua lazima tujue dunia inakwenda wapi, ajira ni tatizo duniani na wenzetu wamekuwa tofauti na sisi. Wanajua kitafutiana ajira!! Hall mara ya mwisho abaondoka wasaidizi wake walikuwa ni K. Ongara na muhindi ambao hakuna mswahili hata mmoja japo Kally amewahi cheza bongo na baba yake ni mbongo lakini ametumia muda mwingi uingereza na ni mwingereza. Kama ni viongozi atawakuta wale wale ukiondoa jemedari ambaye yuko TFF. Kwahiyo akisema majungu ni lazima atwambie yalikuwa wapi!! Alikuja maximo na msaidizi na wachezaji bado hakuwa na jipya zaidi ya kuwatafutia ajira ndugu zake. Tuache kuamini fikra za mzungu ni sawa hata kama anakosea, huo ni ukoloni wa akili. Aliondoka Mourinho chelsea na kurudi mara tatu, na yeye kuna majungu!? Kuna wakati ambao club inahitaji mabadiliko hata kama ya muda mfupi ili kurefresh na kuanza upya
ReplyDelete