Baada ya kuzingua kwa muda mrefu, hatimaye
nyota wawili wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima na kiraka Mbuyu Twite,
wamekubali yaishe kwa kuanguka saini Jangwani.
Nyota hao ambao wamekuwa viungo muhimu klabuni
hapo kwa misimu mitatu mfululizo, hivi karibuni walikuwa wakihusishwa kutaka
kuondoka Jangwani kutokana na mikataba yao kufika kikomo baada ya kumalizika
kwa ligi kuu msimu huu.
Mbuyu alikuwa akitajwa kuhitajika nchini Kenya
na Tunisia lakini kwa Niyonzima ilikuwa tofauti, alikuwa akidengua kusaini
mkataba mpya akitaka cha juu zaidi, lakini suala hilo rasmi limefutwa baada ya
nyota hao kumwaga wino juzi na jana.
Taarifa zimeeleza kwamba, Mbuyu amepewa mkataba wa mwaka mmoja wakati
Niyonzima amekubali kubaki kwa kupewa miaka miwili, pia akiongezwa mshahara kwa
asilimia kadhaa.
“Mbuyu tumemalizana naye tangu jana (juzi
Jumamosi), tumeamua kumpa mkataba wa mwaka mmoja tu, kikubwa tumezingatia
kigezo cha umri (inatajwa ana miaka 34), kwa hiyo kumpa muda mrefu tunaweza
kujikuta tunaingia hasara.
“Niyonzima yeye amekubali kuendelea klabuni na
leo (jana) tumemalizana naye. Kikubwa ni kwamba kilichokuwa kinakwamisha ni
suala la maslahi lakini tunashukuru katika hilo tumeelewana,” kilisema chanzo
hicho cha habari na kuongeza:
“Kikwazo kikubwa katika usajili wa Niyonzima
kilikuwa ni juu ya mshahara, hivyo ili kuondoa malumbano, ilibidi tumpandishie
robo ya ule wa awali.”
Aliposakwa Niyonzima, hakuwa tayari kuweka
wazi suala hilo lakini alionyesha kushtushwa sana. “Nani kakwambia jambo hilo?
Bado sijasaini ila muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi.
“Kwa sasa nipo bize na familia yangu, hivyo
sipendi kujihusisha na mambo mengine, kwani muda wa usajili bado ni mrefu na
Yanga wanalijua hilo,” alisema Niyonzima.
Katika hatua nyingine chanzo hicho kiliongeza
kuwa, mchezaji mwingine kati ya nane waliokuwa wamemaliza mikataba yao klabuni
hapo, kipa Deogratius Munishi “Dida’, naye ameongeza mkataba wa miaka miwili.
0 COMMENTS:
Post a Comment