MASAU BWIRE AKIWA DARASANI... |
Na
Saleh Ally
KUMEKUWA
na maswali mengi sana kuhusiana na Masau Kuliga Bwire mara tu baada ya
kuteremka daraja kwa kikosi cha Ruvu Shooting ambacho sasa kitapambana kikiwa
katika Ligi Daraja la Kwanza.
Sehemu
nyingi katika vijiwe wanavyojadili soka, wamekuwa wakijiuliza kama kweli Masau
atasikika tena na wapo ambao hata wamefikia kusema sasa ajira yake itakuwa
matatizoni kwani huenda kuteremka kwa Shooting, kukafanya ajira yake isitishwe.
Lakini
Masau licha ya kuwa mwandishi wa habari kitaaluma, pia ni mwalimu wa Shule ya
Msingi, kazi ambayo ameifanya kwa miaka 21 sasa.
Katika
mahojiano maalum na Championi Jumamosi, Masau ambaye ni mwalimu wa Shule ya
Msingi Makumbusho jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Chama cha
Soka Mkoa wa Pwani (Corefa), anasema wengi wamekuwa hawajui kuwa yeye ni
mtumishi wa serikali.
Kazi
hii ya ualimu, ulianza lini hasa?
Masau:
Nimeianza mwaka 1994 nikiwa mdogo sana, mimi ni mwalimu wa Daraja III A. Tokea
wakati huo nimefundisha shule tano ambazo ni Mburahati, Gilman Rutihinda,
Mapinduzi, Tandale na sasa nipo Makumbusho.
Hongera
kwa kazi hiyo muhimu kwa taifa. Je, unafundisha masomo yapi na kwa madarasa
yapi?
Masau:
Nafundisha hisabati na sayansi, pia ni mmoja wa walimu wa michezo. Zaidi
ninafundisha darasa la saba kwa asilimia zaidi ya 85 ya kazi yangu ya ualimu.
Miaka miwili tu nilifundisha darasa la sita.
Unawezaje
kupata muda wa kufundisha wakati pia unajihusisha na masuala ya soka?
Masau:
Kabisa, maana wengi wanafikiri sina muda. Licha ya kuwa naishi Kibaha, lakini
mara nyingi mimi ndiye mwalimu wa kwanza kufika hapa shuleni (anaonyesha
daftari la mahudhurio). Nafika saa 12 asubuhi au saa 12:30. Pia najua namna ya
kupangilia mambo yangu kwa uhakika.
Wanafunzi
wanajua timu yako ni Ruvu Shooting? Wanakusikia na kukusoma kwenye vyombo vya
habari?
Masau:
Wanajua sana, siku nikija nimefungwa wananipa pole. Nilipopata tatizo la
Shinyanga, wengi walinipa pole na kuniombea Mungu anisaidie nipone haraka.
Kawaida
mwalimu mzuri huwaweka vijana karibu yake katika mazingira ya kirafiki. Hii ni
njia pia ya kuwafanya wawe huru, kuwa mkali tu haiwezi kusaidia.
Turudi
katika taarifa za kutakiwa na timu kubwa katika usemaji. Je, uko tayari kuihama
Ruvu Shooting kama utapewa dau kubwa?
Masau:
Hili ni swali zuri, ningependa nilifafanue kila mara wanielewe kwamba
nitaendelea kubaki Ruvu Shooting hata kama itateremka hadi daraja la nane kama
lipo.
Kuna
timu zimenitaka na kutangaza kuniongezea dau, lakini nataka kubaki katika timu
yangu maana ni timu inayojali na kuthamini watu. Mimi ni muumini wa
kuheshimiana, bora nipate kidogo lakini nithaminike na kuheshimiwa.
Ulipata
matatizo Shinyanga, ulidai mmepuliziwa sumu vyumbani, ikafikia hadi ukalazwa.
Je, vipi hali yako kwa sasa?
Masau:
Naendelea vizuri, lakini bado siko sawa. Nimekuwa nikiishiwa nguvu na mapigo ya
moyo kwenda kasi. Sasa angalau nimerudi kazini.
Kiasi
fulani unaonekana kama umechanganyikiwa na timu yako kuteremka. Je, hivi si
visingizio?
Masau:
Wapo ambao wamekuwa wakiamini hivyo na hili ni jambo baya kabisa. Watu
wasifanye mzaha katika hili, iko siku litawatokea wao. Sisi si watu wa kwanza
kulalamika kuhusiana na Shinyanga.
Tulipuliziwa
dawa hiyo ya sumu. Kamisaa na Ofisa wa Bodi ya Ligi aitwaye Joel Balisidya pia
ni shahidi, niliwaita baada ya dawa ile kupuliziwa na wote walihakikisha hilo.
Stand
United na wachezaji wao walisikia nikisema mbele ya kamisaa wakiwa karibu na
chumba chetu, hakuna aliyekanusha maana walijua walichofanya.
Vipi
mmeomba lolote ili kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa kama itabanika ni
sahihi?
Masau:
Tumekata rufaa TFF, ndiyo tunaendelea kusubiri. Nimesikia wamekaa ila sijajua
uamuzi wao. Kikubwa watu wanaokataa hilo wanaweza kuwauliza hao niliowataja au
Hospitali ya Aga Khan jijini Mwanza ambako nilitibiwa.
Ulianzaje
kujua kama umeathirika na dawa hizi na kwa nini wewe tu?
Masau:
Hata Kocha (Tom) Olaba pia alikutwa na hili. Unajua sisi tulikuwa karibu na
vyumbani na baadaye tukaingia pamoja na wachezaji. Nilipata shida sana mimi
baada ya hali kuwa mbaya nikiwa chumbani peke yangu mjini Mwanza, hadi wahudumu
wa hoteli wakanisaidia kwenda kuingia kwenye gari nipelekwe hospitali.
Unafikiri
nini sahihi kifanyike kubaini ukweli ili kuondoa hisia za watu kuwa unazungumza
mambo ya kubahatisha?
Masau:
Kamisaa tulimuita akaona, Balisidya wa Bodi ya Ligi alikuwepo. Waamuzi
waliboronga, kila mtu aliona. Hivyo ni rahisi kupata uhakika wa kilichotokea.
Ila
kama adhabu ikitoka, isiwe kwa waamuzi tu ila na sisi tupewe nafasi ya kurudia
mechi hiyo katika uwanja huru.
Pia
niombe suala la ulinzi lidumishwe hasa mikoani, maana kunakuwa na kampeni
makusudi za kudhulumu pointi ambazo zinaonyesha kupangwa kwa makusudi.
Taarifa
zilieleza mlikuwa na ulinzi wa kutosha, mlipewa gari mbili za polisi?
Masau:
Kweli, lakini ni baada ya kuzungumza na Makao Makuu Dar es Salaam. Pale
Shinyanga ilishindikana, maana nilimpigia mkuu wa polisi pale kumuomba atupe
ulinzi baada ya vijana kuvamia na mapanga hotelini kwetu.
Lakini
alinikatia simu baada ya kusema maneno yasiyofaa. Nikapiga simu Makao Makuu Dar
es Salaam kuomba msaada. Hivyo hadi alipoamrishwa ndiyo akawatuma FFU wakiwa
kwenye gari mbili kutupa ulinzi. Haikuwa sahihi ingawa tunawashukuru mabosi
wake kwa kutusikiliza shida zetu.
MIAKA
21, SHULE 5:
Shule Mwaka
Mburahati 1994-97
Rutihinda 1997-2000
Mapinduzi 2002-2010
Tandale 2010-2010
Makumbusho 2010-sasa
0 COMMENTS:
Post a Comment