Na Saleh Ally
NITAPISHANA
sana na nyie ndugu zangu, lakini hofu yangu mimi ni hofu yenu, kuwa watu waoga
utafikiri hapa kwetu ni sehemu mbaya sana ambayo inahitaji kupambwa na watu
fulani.
Watanzania
wengi sana hawajui ubora wa nchi yao, ndiyo maana kulaumu kumekuwa dira ya
wengi wakiamini huenda kila sehemu ni nzuri kuliko Tanzania.
Wakati
mwingine kuna haja ya kujionea wenyewe, acheni kuamini kila kinachozungumzwa na
wanasiasa, maana karibu kila mmoja anaponda tu Tanzania, hakuna anayesifia hata
kidogo.
Watu
kibao wangefurahia kuishi Tanzania bila ya kujali wanatokea wapi, iwe ni
Ujerumani, Uholanzi, Japan, Uingereza na kwingine kote.
Sisi
Watanzania ndiyo hatupaoni kwetu kama ni nchi nzuri ya kuishi. Kasoro
hazitaisha, kila nchi ina kasoro lakini leo niwe mtu mwingine ambaye si
mwanasiasa kuwa kwetu pazuri sana na tunapaswa kujiamini waungwana.
Samahani
sana, nilianza kama mwanasiasa vile, lakini lengo ni kuwakumbusha kwamba
tunaishi katika nchi bora kabisa ambayo unaweza kuishi maisha yako yote bila ya
hata kutamani kwenda nje, hivyo tusitoe nafasi kwa wajanjawajanja kutuchezea
wanavyotaka wao.
Mfano
wa watu wanaotaka kuleta utani nasi ni Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij
ambaye anaonekana kabisa anatuona kuwa bado tumelala.
Hizi
zimekuwa hisia za watu wengi kutoka Ulaya, wanadhani bado tumelala. Hata
Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania hudhani sisi tumelala, sasa ni tofauti,
wapo walioamka hata kuzidi wanaoishi Ulaya.
Huu
ni wakati mwafaka wa Nooij kubeba mabegi yake na kwenda kwao Uholanzi ili Taifa
Stars ifanyiwe mchakato mwingine mapema kabisa kabla ya kuingia kwenye kazi ya
kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika na pia Kombe la Dunia.
Stars
ni timu ya hovyo, si kwa kuwa tu imepoteza mechi zake za Kombe la Cosafa kwa
kufungwa na Swaziland na Madagascar lakini uliiona timu ilivyocheza?
Tungeweza
kusema timu ilifungwa tu kutokana na kushindwa kutumia nafasi nyingi ilizopata
lakini ilionyesha soka safi na la kuvutia.
Swaziland
ilitawala na kuizidi Stars, ikashinda 1-0. Ikaja Madagascar nayo ikashinda mabao
2-0 huku ikitunyanyasa pia, ikiwa na mashambulizi mengi, ilimiliki mpira zaidi
yetu.
Madudu
haya huenda TFF wanakuwa waoga kwa vile wanataka kuwa watu wa kungoja au
kuhofia kwamba wataambiwa walimtoa Kim Poulsen kwa kukurupuka lakini huu ndiyo
wakati mwafaka wa kumpa ruhusa yule babu anayependa sana bia aende zake.
Tayari
Nooij ameshasema soka letu ni maneno tu. Ameshaeleza namna anavyoondoka mapema
kwenda zake kunywa bia. Anaonyesha kiasi gani anavyotudharau, lakini sisi
tunataka tuendelee kukaa kimya.
Tukubali,
TFF ni mali ya umma. Si binafsi na inawakilisha Watanzania na hata kipato chake
kinatokana na Watanzania, iwe wamechangia kupitia viiingilio, wadhamini au hata
Fifa kwa kuwa inatoa ikijua ni shirikisho la Watanzania.
Hivyo,
TFF inapaswa kuonyesha ujasiri kwa kuwa kila dalili inaonyesha tutafeli mbele
na ndiyo imekuwa ndoto ya Watanzania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa Afrika.
Kwa Nooij, hakuna tutakachopata kwa kuwa anaonyesha wazi hayuko ‘siriaz’.
Tanzania
si sehemu ya Wazungu kuja kustaafu, tunahitaji watu wanaoweza kufanya kazi.
Kama ingekuwa Stars ni kwa ajili ya kuwapa watu nafasi ya kustaafu, basi
angalau tungewaachia wazawa kama akina Abdallah Kibadeni, Boniface Mkwasa na
wengine nao wastaafu hapo wakipata huo mshahara.
TFF
mnaweza kuwa mnahofia, basi mimi naweza kuwasaidia katika suala la kubeba
mabegi ya Nooij ili nimpelekee huko Afrika Kusini. Leo akimaliza mechi ya
‘kirafiki’ dhidi ya Lesotho ambayo hata akishinda ni kazi bure, abebe mabegi
akawasalimie kwao.
0 COMMENTS:
Post a Comment