MASAU AKIWA OFISINI KWAKE KATIKA SHULE YA MSINGI YA MAKUMBUSHO JIJINI DAR ES SALAAM. |
Na Saleh Ally
UKIKUTANA na Masau Kuliga Bwire, kamwe hauwezi kujisikia
mchovu au mpweke. Ni mcheshi, mtu mwenye stori nyingi.
Masau Bwire ambaye sasa inawezekana ndiye msemaji
maarufu zaidi katika tasnia ya michezo nchini ni mwalimu wa Shule ya Msingi
Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mwalimu huyo ambaye ni rafiki mkubwa wa wanafunzi
shuleni hapo kama ilivyo kwa walimu wengine, amezungumza na Championi Ijumaa na
kueleza jambo ambalo hajawahi kuliweka hadharani.
Ruvu Shooting imeporomoka hadi Ligi Daraja la Kwanza.
Masau amesisitiza kwamba hatahama kamwe na hiyo ndiyo timu yake hata ikishuka hadi
daraja la nane (kama lipo), lakini yeye ni shabiki wa timu gani?
Kwa mfumo wa ushabiki wa soka nchini, inajulikana kama
mtu si Yanga basi atakuwa Simba ingawa wako wachache wamekuwa wakiendelea
kusisitiza kwamba wao si mashabiki wa klabu hizo kongwe zaidi nchini
zilizoanzishwa mwaka 1935 na 1936.
Masau anasema licha ya watu kuamini yeye ni Simba damu,
wamekuwa wakifanya makosa makubwa kwa kuwa kuna kitu kuhusu yeye hawakuwahi
kukijua.
“Kwanza wanapaswa kujua mimi nimewahi kuwa shabiki wa
Simba, halafu nikawa shabiki wa Yanga. Nimewahi kuwa shabiki wa timu zote
mbili.
“Baadaye nikaamua kuachana nazo zote. Hadi sasa mimi si
shabiki wa Simba wala Yanga, watu hawaamini hilo lakini ndiyo hali halisi,”
anasema Masau.
Kama yeye si shabiki wa Simba au Yanga ambazo aliwahi
kuzishabikia! Je, ilikuwaje akazishabikia halafu akazitosa zote?
Simba:
“Nikiwa mdogo, kaka yangu ambaye sasa ni askari pale
Kibaha alikuwa anapenda sana Simba. Akaondoka nyumbani kwenda shule kwa muda
mrefu.
“Aliporudi nyumbani akaja na picha kubwa za wachezaji
mbalimbali wa Simba na kuzibandika chumbani. Mimi pia nilikuwa nikipenda Simba
kwa ajili yake, sasa mambo ya kitoto si nikazitoboa zile picha machoni mwa
wachezaji kwa kalamu.
“Aisee, jamaa alinikimbiza bila kuchoka karibu kijiji kizima.
Kila nikigeuka, yupo, naongeza mbio. Nikigeuka tena huyu, aah! Akanikamata,
alinipiga vibaya. Kuanzia siku hiyo nikaanza kuichukia Simba, nikaachana nayo
na kuhamia Yanga,” anasema.
Kama aliondoka Simba, kipi kilisababisha ahamie Yanga
ambayo hakuwa akiishabikia?
Yanga:
“Kawaida pale kijijini tulikuwa tukicheza soka tena
mechi kali kati ya Yanga dhidi ya Simba. Mimi nilikuwa staa wa soka katika
kijiji chetu, lakini ni ule mpira wa makaratasi ‘chandimu’.
“Kwa kuwa nilikuwa sichezei tena Simba, basi nikatua
Yanga na ndiyo ikawa timu yangu. Nikawa nawasumbua sana Simba, nakumbuka
kipindi kile nilikuwa najulikana kwa jina la utani la Amasha.
“Siku moja, nilitakiwa kwenda shule lakini kwa kuwa
tulikuwa na mechi, pia ni tegemeo. Sikukubali kuwaangusha Yanga. Nikatoroka na
kwenda kucheza, kumbe mwalimu alishitukia ile hali.
“Basi nilipofika shule, aisee alinikamata na kunichapa
sana kwa uzembe ule. Hasira zikanishika, nikaona Yanga ndiyo imeniponza, aaah!
Nikaachana nayo pia,” anasema Masau na kusisitiza.
“Kuanzia wakati ule sijawahi kuzishangilia na badala
yake nimebaki kama mwanamichezo hadi nilipotua Ruvu Shooting.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment