June 27, 2015



Na Saleh Ally
KATI ya vitu ambavyo vimekuwa havizungumzwi sana ni kuhusiana na Kocha Alex Ferguson alivyomchapa kibao Ryan Giggs mbele ya mpenziwe pamoja na wachezaji wengine makinda wa Manchester United.


Giggs ni kati ya wachezaji wachache walioichezea Manchester City na Manchester United ingawa yeye aliichezea City akiwa mtoto mdogo.

Baada ya Ferguson kugundua ubora wake akahakikisha anajiunga na timu yake, mama yake akamkabidhi Ferguson awe kama mzazi wake.

Baadaye Ferguson alianza kumuamini Giggs kama kaka wa akina David Beckham, Garry na Phil Neville, Paul Scholes na Nicky Butt. Mara nyingi alitaka afanye kazi ya kuwasimamia katika mambo kadhaa.

Siku moja akiwa nyumbani, alipigiwa simu usiku na mtu aliyejitambulisha ni jirani wa nyumba aliyokuwa akiishi Giggs kwamba kuna kelele kubwa ya muziki hadi anashindwa kulala.

Ferguson alichofanya ni kufunga safari hadi eneo hilo, baada ya kuegesha gari lake aliingia ndani ya nyumba hiyo kama askari. Akazima muziki na mara moja, akamchapa kibao Giggs kibao kikali mbele ya kina Beckham, wageni wake wengine pamoja na mpenzi wake.


Baada ya tukio hilo, disco likawa limeisha na Scholes, Beckham na wenzake wakajua kuwa wanafanya kazi na mtu wa aina gani, hakuna utani.

Lakini huenda lilikuwa somo kubwa na kali zaidi kwa Giggs ambaye hajawahi kuonekana hana nidhamu uwanjani kwa kuongoza kiutendaji na mara zote amekuwa mmoja wa wachezaji bora na wenye nidhamu ya juu.

Giggs ameichezea Manchester United kwa miaka 18 tangu mwaka 1987 alipojiunga na timu ya watoto, lakini sasa ana rekodi ambayo inaonekana huenda ni miaka kumi au zaidi ijayo ndiyo inaweza kuvunjwa kwenye Ligi Kuu England.

Kofi alilochapwa na Ferguson, leo ni zaidi ya miaka 10 na limemsaidia kuongeza nidhamu, kujitambua na kumfanya aweke rekodi ya kucheza mechi 632 katika Ligi Kuu England.


Rekodi hiyo inamfanya Giggs raia wa Wales kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika Premier League.

Hakuna ubishi, bila nidhamu uwezo wa mchezaji hauwezi kuwa bora. Nidhamu ndiyo inayompa nafasi mchezaji kuwa na mwili ulio fiti, ulio tayari kwa mapambano na akili ya kufanya ubunifu uwanjani.

Kwa mujibu wa Giggs mwenye ambaye Kiasili ni Mwafrika, anasema tangu alipopigwa kofi hilo na Ferguson, alitumia siku zaidi ya mia akijifunza mengi.

“Kwanza niliona amenionea na kunidhalilisha sana, nilitamani kuondoka siku hiyohiyo. Baada ya hapo, nilijikuta nimebadilika mwenyewe na kuanza kuchambua makosa yangu.

“Kweli nilikuwa mkubwa zaidi ya kina Beckham, lakini niliwaandalia mazingira mabaya, nikawabugudhi majirani na kweli nilikuwa sina nidhamu,” anasema Giggs.


Nikaona vizuri kujifunza kuliko kuchukizwa. Ndiyo maana nilifanya vema zaidi kadiri siku zinavyosonga. Pia nilitaka kumuonyesha Ferguson mimi ni mtu ninayeweza kubadilika, nikaongeza juhudi sana.

Ukiangalia wachezaji 10 waliocheza Ligi Kuu England mechi nyingi zaidi, wawili ndiyo wanacheza hadi leo na wazi hakuna nafasi ya kufikia rekodi hiyo.

Gareth Barry wa Everton amecheza mechi 562, ana misimu hadi mitatu kufikia mechi hizo za Giggs. Tayari ana miaka 34 na swali ataweza kuendelea kucheza zaidi ya misimu miwili?

Kipa Mark Schwarzer ana mechi 514 katika nafasi ya saba. Tayari ana miaka zaidi ya 40, hana nafasi ya kucheza zaidi ya mechi 50 za Premier League.


Kilichomfikisha Giggs hapa ni hicho kibao cha Ferguson, kikambadili na kujitambua kwamba wapi alikosea na kipi cha kufanya.

Mafunzo yanapatikana kwa njia mbalimbali, huenda kwa mdomo, kwa utaratibu au hasira lakini wangapi wanakubali na kujifunza hadi kufikia kujitambua kama ilivyokuwa kwa Giggs?

Kucheza kwake mechi nyingi lazima kuliongozwa na mengi. Mfano kujituma, kutaka kushinda na kuuepuka uvivu. Msingi wa yote hayo, ulikuwa ni nidhamu.

Nidhamu ndiyo msingi wa kila kitu katika maisha. Nidhamu ndiyo inaweza kuwa muongozo wa kila unachofanya kwenda kwenye mafanikio.


Giggs kacheza mechi nyingi zaidi kwa kuwa alikuwa na nidhamu ya juu baada ya adhabu ya Ferguson. Mchezaji mwenye kipaji wa Tanzania angechapwa kibao na kocha, angejifunza kama ilivyokuwa kwa Giggs alipochapwa na Ferguson?


         Mchezaji                Nchi                     Mechi
1. Ryan Giggs                   (Wales)                     632
2. Frank Lampard          (England)                609
3. David James                (England)                 572
4. Gareth Barry               (England)                 562
5. Gary Speed                   (Wales)                     535
6. Emile Heskey              (England)                 516
7. Mark Schwarzer         (Australia)               514
8. Jamie Carragher        (England)                 508
9. Phil Neville                   (England)                 505
10. Steven Gerrard         (England)                505


1 COMMENTS:

  1. Mbona makala haijazungumzia nidhamu yake ya kumchabanga shemejiye (mke wa kaka yake)?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic