Na Saleh Ally
KOCHA Mart Nooij ameondoka Tanzania akiwa ameweka
rekodi ya aina yake. Kwamba katika mechi zaidi ya 15, alikuwa ameiongoza Taifa
Stars kushinda mechi tatu tu!
Kocha huyo Mholanzi alionekana ndiyo tatizo
kubwa, hakika hakustahili na kumuondoa ilikuwa sahihi kabisa.
Huenda kuchelewa kwake kuondoka kumekuwa
tatizo kubwa zaidi kwa TFF kwa kuwa amejikuta akilazimika kusindikizwa na
askari utafikiri ni kiongozi wa serikali.
Watanzania walionekana kumchoka Nooij kuliko
TFF ambao ndiyo walikuwa wakifanya naye kazi. Huenda walitaka kujaribu tena na
tena, lakini imeshindikana.
Taarifa nyingine zilieleza TFF walishindwa
kumng’oa Nooij mapema kwa kuwa fedha za kuvunja mkataba zilikuwa nyingi sana.
Huenda ni wakati mwingine wanapaswa kujifunza kuwa na mikataba bora ambayo ina
urahisi wakati wa kuvunja.
Lakini kulikuwa na taarifa nyingine kwamba
si Jamal Malinzi, lakini kuna kiongozi mwingine ndani ya TFF mwenye sauti hata
kuliko rais huyo wa shirikisho ndiye alikuwa akizuia kocha huyo asiondoke.
Alikuwa akizuia kutokana na maslahi yake
binafsi, kwamba yeye ana urafiki wa karibu na kocha huyo. Hivyo aliendelea
kushawishi asiondoke.
Yote hayo yanaweza kuwa kweli au la, lakini
ambacho TFF wanapaswa kusisitiziwa na kukumbushwa ni kwamba mabadiliko
waliyoyafanya kwa kumng’oa Nooij na kuvunja benchi lake la ufundi, lazima
wakumbuke wamemshusha konda na kumuacha dereva.
Kama kweli imeonekana mwendo wa daladala
haukuwa sahihi, halafu wameamua kumuondoa konda na kumuacha dereva, basi mwendo
utaendelea kuwa uleule hata kama atajirekebisha kwa muda, mwisho atajisahau tu.
Nasisitiza, uamuzi wa kumuondoa Nooij
ulikuwa sahihi kabisa lakini ukweli kuvunja benchi la ufundi bila ya kumuondoa
mshauri wa ufundi wa Rais wa TFF katika masuala ya ufundi, Pelegrinus Rutayuga
ni kutwanga maji kwenye kinu.
Rutayuga ameshiriki katika mechi, ushauri
wake umeifanya TFF kupotea katika mengi. Hivyo ni lazima naye alipaswa kuondoka
kwa kuwa ndiye dereva wa masuala ya ufundi.
Kama anamshauri Rais wa TFF, Jamal Malinzi,
basi ndiye alihusika na ujio wa Nooij, ndiye alishiriki katika vitu vingi
vilivyohusiana na ufundi ambao umefeli.
Rutayuga ndiye amekuwa dereva wa ufundi wa
Taifa Stars ambao umefeli. Hivyo kuondoa mkono na kuacha kiwiliwili chote na
kichwa ni kazi bure kujisifia kuwa kuna mabadiliko.
Kuna baadhi ya wachezaji wa Stars
waliniletea malalamiko kuhusiana na Rutayuga, lakini tatizo likawa moja kwamba
hawataki kutajwa, pili hawataki kufafanua kwa undani zaidi, jambo ambalo niliona
si sahihi.
Lengo si kumshambulia Rutayuga, hivyo lazima
kama ni shutuma, ziwe zenye uhakika na ukweli. Huenda wao waliona kuna hofu ya
kumuogopa kama ambavyo wachezaji wamekuwa na hofu. Hapa hilo halipo.
Msisitizo ilikuwa ni lazima wao wawe wazi.
Matatizo hayo tunaweza tukawa tumeshindwa kuyajua kwa kuwa wao wanaficha,
lakini hili la Rutayuga kufeli na Stars kufanya vibaya zaidi katika kipindi
yeye akiwa mshauri, wala halina majadala.
Inawezekana kuna matatizo mengi ambayo
yamejificha, kama wachezaji hao wangekuwa jasiri kusema tungeweza kujua ukweli.
Ukimya wao, unatufanya tubaki na maswali kwamba tatizo ni nini!
Pamoja na woga wao, bado tunaweza kunusa harufu
ya tatizo pia kwamba uwepo wa washauri wasiokuwa na uwezo pia ni tatizo kubwa.
Tusizungushe mambo, Rutayuga si mshauri
ambaye anaweza kuisaidia Tanzania kutokana na rekodi zake kiuwezo. Ndiyo maana
hata siku ile nilipokutana naye, zaidi alijisifia mafunzo yake ya fitna kutoka
kwa Mwenyekiti wa zamani wa TFF, Muhidini Ndolanga.
Taifa Stars haihitaji fitna kama za Ndolanga
ambaye wakati wake alishindwa kuisaidia na kuwa moja ya timu za hovyo kabisa.
Sasa huyu aliyechukua mafunzo kwake ataisaidia vipi timu hiyo?
Malinzi lazima akubali kwamba mshauri wake
hakuwa na msaada na hana msaada sasa kama ataendelea kuwa hapo kwa masuala ya
ufundi. Hivyo asichelewe kwa mara nyingine kama ilivyokuwa kwa Nooij, amuondoe.
Vizuri atafutwe mshauri mwenye taaluma ya
ukocha tena mwenye uwezo na rekodi za juu kabisa. Mshauri ambaye ana uwezo wa
masuala ya kiufundi kwa ajili ya kusaidia timu yetu. Kama ni suala la kulipa
fadhila, inatosha na mkumbuke Stars ni timu ya Watanzania na wao wanapoona kuna
tatizo, wakati mwingine ni vizuri kuwasikiliza.
Saleh Ally Metodo na Pelegrinus Rutayuga ni chatu na mbuzi,teh teh teh teh teh!
ReplyDeleteYetu macho na masikio,Saleh soma sana surat yassin maana huyo jamaa inasemekana kwa kutuma chatu hajambo!
Hapa ni jembe na soka la Tanzania,ipo siku Jembe atakuwa mmoja wa mashujaa wa ukombozi wa soka letu hao Akina nani sijui bora wajitambue mapema
Delete