Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles
Boniface Mkwasa ameonyesha kuumizwa na maneno yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Wakati akilifunga Bunge la Jamhuri ya
Muungano. Kikwete aliamua kuwa wazi na kusema aliamua kuacha kwenda uwanjani
kuiunga mkono Taifa Stars kutokana na kupoteza michezo mfululizo.
Kikwete alisema mara kadhaa alipokuwa
akienda uwanjani, Stars ilikuwa ikipoteza hadi kufikia kuona watu wanaweza
kuona yeye ana bahati mbaya ndiyo maana timu inafungwa kila mara.
Hali hiyo ilimfanya Mkwasa ajitokeze na
katika maneno yake alisisitiza kuwa ni wakati mwafaka kwa Kikwete kurudisha
imani yake kwa Stars kwa kuwa imebadilika.
Mkwasa anakuwa kati ya Watanzania walioguswa
na maneno ya Kikwete ambaye amekuwa mkweli na kujiweka wazi kwamba anakerwa na
mwenendo wa Stars.
MKWASA. |
Hakika unakera na hata baada ya kuingia
kwa Mkwasa, katika mechi yake ya kwanza ambayo ilikuwa dhidi ya Uganda, Stars
ilipata sare.
Maana yake, hakuna chochote cha kujivunia
hadi sasa. Kama ni mabadiliko anayoyasema Mkwasa, si thabiti au yanayoweza
kuonekana na kusema kweli yamepatikana.
Bado, ndiyo safari inaanza. Kikubwa ni
kumuunga mkono yeye na kikosi chake na yeye na wenzake wajitume kuwaonyesha Watanzania
kwamba hawajakosea kuwaunga mkono.
Kikubwa wakumbuke, mafanikio yatakuwa
sehemu ya kurudisha imani yao kwa Watanzania. Lakini kama watafeli katika hilo,
basi mwisho uvumilivu utawaisha wale wanaowaunga mkono.
Pamoja na Mkwasa, wadau wengine nao
wanapaswa kuumizwa na jambo hilo. Hakika ni gumu kuendelea kulibakiza moyoni
huku ukiona timu ya taifa lako ikigeuzwa kichwa cha mwendawazimu.
Kufeli kwa Stars hakujaanzia kwenye kikosi
pekee, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lazima wawe kitu kimoja
pia.
TAIFA STARS |
Huenda wale wa juu wanaweza kuwa
wanatamani kuona mafanikio yanapatikana na wakafanya kila linalowezekana.
Lakini wengine ambao wako ndani ya
shirikisho hilo kwa ajili ya maslahi yao binafsi wakawa tayari kuiona timu
ikifeli ilimradi wao wanafaidika.
Lazima tukubali, Stars si ya TFF, ni ya
Watanzania wote wapenda maendeleo wa mchezo wa soka. Lakini haiwezi kupiga
hatua kama waliopewa dhamana wako kwa ajili ya matumbo na mioyo yao.
Kuna kila sababu ya kila mmoja kuwa
mkweli, kuipigania Taifa Stars na kama tabia za ubinafsi, ujivuni, kujiamini
kwa kipuuzi kutaendelea. Basi Stars haitapiga hatua hata kidogo.
Mwisho itakuwa hivi, Rais Kikwete amekuwa
wa kwanza kuacha kwenda uwanjani, baadaye atafuatia Saleh Ally, halafu wewe,
yule na mwingine na siku moja, timu hiyo itacheza uwanjani bila ya mashabiki!
Kikosi
0 COMMENTS:
Post a Comment