July 22, 2015


Na Saleh Ally
KUNA jambo wamelifanya Manchester United unaweza kuliona ni dogo sana, lakini sasa wanakwenda rasmi katika kutatua kilichokuwa kikiwaumiza kwa muda mrefu sasa.


Kocha Mkuu, Louis van Gaal ameamua kumsajili kiungo wa Bayern Munich, Bastan Schweinsteiger, anayejulikana kwa majina mengi yanayomaanisha ubora.

Ukiachana na majina mawili yakiwa ni ufupisho wa jina lake, Schweini na Basti. Majina yaliyobaki ni “Midfield Motor’, ‘Brain’ na ‘Heart’. Yeye ndiye mota ya timu, yaani ndiyo anayeizungusha, moyo pia roho ya timu.


Van Gaal anaijua habari yake kwa kuwa alifanya naye kazi alipokuwa kocha wa Bayern Munich.

Schweinsteiger ni kati ya viungo bora kabisa duniani kwa mambo mengi na uthibitisho kuwa katika miaka 17 aliyoichezea Bayern Munich kikosi cha pili, huku akiwa tegemeo katika kikosi cha kwanza kwa miaka 13, mafanikio yanaonekana.

Akiwa na Bayern Munich amechukua makombe zaidi ya 20, yeye akiwa ‘dereva’ wa timu. Bundesliga mara 8, Kombe la DFB mara 7, Kombe la Ligi, mara mbili kama ilivyo kwa Super Cup.


Ukienda Ulaya, kabeba Ligi ya Mabingwa mara moja, pia Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu.

Ujerumani imechukua ubingwa wa dunia akiwa ‘dereva’ pia, hii ni mwaka jana walipochukua ubingwa huku wakionyesha Ujerumani ni hatari kwa kuichapa Brazil mabao 7-1, kwao.

Usisahau michuano miwili iliyopita ya Kombe la Dunia, 2006 na 2010, Ujerumani mara zote ilishika nafasi ya tatu, yeye alikuwa ‘dereva’ pia.

Kwa aina ya uchezaji wake, uzoefu wa mechi 535 na kufunga mabao 69, unaweza kusema Manchester wamepata bando la bila kikomo kwa kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kuongoza ulinzi, lakini kusaidia mashambulizi ya timu, pia anafunga.


Schweinsteiger ana uwezo mkubwa wa kukaba na kwa uchezaji wake, lazima Manchester ina winga wenye kasi kama ilivyo kwa Frank Ribery na Arjen Robben ili awapigie yale mapasi ‘marefu’ ya uhakika.

Tangu ameondoka Roy Keane, Manchester haikuwa na mtu sahihi katika nafasi hiyo zaidi ya Paul Scholes ambaye wakati fulani Kocha Alex Ferguson alilazimika kumrudisha licha ya kuwa amestaafu na kuonyesha kiasi, lilikuwa tatizo sugu.

Michael Carrick hakuwa ‘mbaya’, lakini hakufikia kiwango cha juu kiasi cha kumfananisha na Keane, Scholes kama unavyoweza kusema Schweinsteiger, huenda ni zaidi yao kwa mujibu wa rekodi na takwimu zake.

Achana na ushabiki wa Kiingereza, Schweinsteiger anaonekana kuwa na rekodi ya juu zaidi kuliko Scholes na Keane kwa maana ya mafanikio kwenye ligi, Ulaya na pia timu ya taifa kama vile kuchukua ubingwa wa dunia tofauti na wao.

Inaonyesha sasa ni wakati wa United kuwa na uhakika katika ulinzi, pia uhakika wa mawinga wake kucheza vizuri lakini mabeki wakizubaa, tayari United wana mfungaji wa mashuti ya mbali.

Kwa msimu huu, pamoja na Manchester usajili wa aina mbalimbali, huenda usajili bora zaidi utakuwa wa Schweinsteiger na kama atakuwa katika kiwango chake bila ya kuumia, kuna kila sababu ya United kurejea tena kwenye fomu na kuwa kati ya wale watatu au wawili wanaowania ubingwa wa Ligi Kuu England na si kutaka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya tu!


Dondoo:
*Alikuwa na uhusiano na mwanamitindo Sarah Brandner aliyeishi naye tangu mwaka 2007 hadi 2014 walipotosana.

*Alipotosana na Sarah, Schweinsteiger hakukaa kimya kwa muda mrefu kabla ya kuibukia kwenye uhusiano wa mcheza tenisi nyota wa Serbia, Ana Ivanovic.

* Schweinsteiger ni muumini mzuri katika dini anayoamini ya Ukristo, anatokea madhehebu ya Roman Catholic.

*Ndoto yake ilikuwa ni bingwa wa Ulaya na duniani kote katika michezo ya mashindano ya kwenye barafu, akaangukia kwenye soka.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic