July 10, 2015


Na Saleh Ally
MASWALI mengi sana yamekaa kichwani, lakini kubwa ni kiasi gani namna Watanzania wamekuwa wakichezewa akili na kulaghaiwa waziwazi na wakaendelea kukaa kimya bila ya kusema lolote.


Watanzania kweli ni wapole sana, lakini siamini kwamba ni watu wanaoweza kuchezewa sharubu na mtu au kundi la watu halafu wakabaki kimya huku wengine wakiendelea kusifia kilichofanyika ni bora kabisa.

Mfano mzuri ni lile suala la kufungiwa miaka saba kwa Dk Damas Ndumbaro. Alifungiwa na Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilitoa adhabu hiyo ya ajabu kabisa, Watanzania, wapenda soka na michezo kwa jumla wakakaa kimya!

Dk Ndumbaro alikuwa akizitetea klabu kuhusiana na maslahi yao. Hadi leo zimefaidika na alichokifanya, lakini zimekaa kimya na kuacha aendelee kubaki nje ya mpira kwa maslahi ya wachache.

Kwa mara nyingine, tumeona namna sakata la kiungo mshambuliaji Ramadhani Singano ‘Messi’ na Klabu ya Simba kuhusiana na ipi ni kandarasi sahihi. Kila mpenda soka na mwanamichezo alitaka kujua ukweli wa hilo.


Kilichokuwa kinazungumzwa kuhusiana na hilo, Simba walisema wana mkataba wa miaka mitatu na mchezaji, Messi akasema ana mkataba wa miaka miwili tu. Mchakato wa kupata mwafaka katika hilo ukaanza na Simba wakawa tayari kutoa vielelezo, halikadhalika mchezaji pia akafanya hivyo.

Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza) kiliingia kumsaidia Messi, hilo ni jambo zuri kabisa. Baadaye TFF wakaziita pande zote na kukaa pamoja, mwisho wakajadiliana na baada ya hapo sekretarieti ikiongozwa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine walizungumza na waandishi na kulivuruga kabisa.

Hapa ishu ilikuwa ni kusema maneno mawili tu, “mkataba wa Messi wa miaka miwili ndiyo ulio sahihi” au “mkataba wa miaka mitatu wa Simba, ndiyo sahihi.”

Hilo likawa gumu na majibu yakawa hivi; “Hapa hatukuja kutafuta nani atakuwa ni mshindi, badala yake tumetaka wakae na kumalizana.” Hii ilikuwa ni sehemu ya zile zilizoonyesha kuna jambo linakwenda chinichini na huenda Simba, haikutakiwa kushinda.

Baadaye Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji ilikutana na pande hizo, ikapangwa tarehe nyingine na katika kikao cha pili, uamuzi umesema Messi ni mchezaji huru.


Unapomuambia kila mmoja kwamba Messi ni huru, jibu linakuwa ni kwamba Simba ilichakachukua mkataba kutoka wa miaka miwili na kuweka wa miaka mitatu. Jibu la Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Richard Sinamtwa liko hivi: ”Hapana!”

Sinamtwa ambaye kitaalamu ni mwanasheria anaeleza kwamba madai yaliyokuwa mezani ni kwamba mambo kadhaa ndani ya mkataba kutotimizwa kwa Simba kama vile kutolipa kodi ya pango la Messi.

Madai mengine yalikuwa ni kutolipa bima na huduma za afya. Simba ikashinda zote, likabaki hilo la kodi lakini swali kwani hii ndiyo ile ishu iliyoanzisha mjadala ya mkataba upi sahihi? Na vipi suala la upi mkataba sahihi liendelee kuwa siri?

Hivi hiyo kamati imeshindwa kusema kwamba Simba walichakachua au Messi ndiye alikuwa na mkataba wenye tatizo! Haohao wameingia kwenye kuvunja mkataba wa Messi kwa madai hakulipiwa pango la nyumba!

Simba wamesisitiza kwamba katika mkataba Messi alikuwa akilipwa mshahara wa Sh 700,000 kwa mwezi. Wao walikuwa wakimpa Sh 800,000, yaani lile ongezeko la Sh 100,000 ndiyo hiyo kodi.

Kamati ya Sinamtwa imekubali kweli Messi alikuwa akilipwa Sh 800,000 ingawa kwenye mkataba inaonekana ni Sh 700,000. Hawakutaka kuhoji ongezeko la Sh 100,000 ni la nini na mwisho wamesema hazina maelezo. Simba wamezitolea lakini bado hukumu imewamaliza.


Je, kama ilionekana Simba hawakulipa fedha hizo, kwa nini kamati isiwaagize kulipa mara moja. Mfano, “baada ya siku 7 muwe mmelipa la sivyo mkataba utavunjika.” Kwa sasa mkataba umevunjwa na Messi hajalipwa, sasa hapo ameifaidika nini kwa maana ya haki?

Kazi ya kamati si lazima tu kuvunja na kusambaza. Lengo ni kuweka mambo sawa panapowezekana. Sasa kipi kilikuwa kinashindikana na Simba imethibitisha ilikuwa ikilipa?

Inaonyesha ilikuwa lazima mkataba uvunjwe kwa kila namna ili timu inayomtaka impate. Huenda ungevunjwa mwanzo kabisa, lakini kwa kuwa Simba haikuwa na makosa, kukawa na ugumu. Kosa likaendelea kutafutwa.

Hauhitaji kujifunza sana kupata majibu ya hili. Hakika ilionekana tangu mwanzo, zilikuwa zikifanyika juhudi za kuvunja mkataba wa Messi na Simba kwa hila ili aende sehemu nyingine ambao watampata kwa bei rahisi kuliko akibaki mikononi mwa Simba ambao wamesumbuka kumkuza na kumpa nafasi hadi kaonekana na kujulikana lakini leo wanadhulumiwa na wajanja.

Hili lilifanyika tangu siku ya kwanza, ndiyo maana hata baada ya ule mkutano wa kwanza, Messi cha kwanza alikimbilia kuhoji kama yeye tayari ni mchezaji huru au la? Tuwe wakweli bila ya woga wala kufuata mkumbo katika hili, kila kitu kiko wazi, dhuluma imepita hadharani.

Kama angeonewa Messi, lazima tungesimama kidete kupigania haki yake bila ya kumhofia Simba hata mmoja kwa cheo au umaarufu wake. Sasa leo, Simba inadhulumiwa na kundi la watu maarufu kama kamati, tena wakiwa hawana mchango wowote katika maisha ya soka ya Tanzania, halafu tukae kimya bila ya kuwaambia. Kwa kipi? Halafu wewe unakaa kimya kwa sababu zipi pia? Acha woga, fungua mdomo wako tutetee mpira wa Tanzania kwa kuwa mambo kama haya, yataendelea kuuvuruga mpira wetu ambao ni mchanga kila kukicha.


Kamati ya Sinamtwa sasa inataka kutumika kama rungu la kuwamaliza wanyonge, rungu la kuwapiga na kuvunja haki za watu kama ilivyo kwa Dk Ndumbaro ambaye hakuwa na kosa, sasa zamu ya Simba, usishangae kesho itakuwa kwako maana kamati hiyo bado kidogo igeuke kuwa “Mungu wa Mpira wa Tanzania (MMT).”

Linakuja suala la nani alifanya juhudi za kumpata kwa hila? Tayari jana Messi amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Azam FC, siku moja tu baada ya mkataba wake kuvunjwa!

Kwangu Messi ni kijana mtulivu kabisa na muungwana ila inaonekana ameshikwa na watu wanaotaka kutimiza malengo tofauti. Kwani mlolongo wa alichokuwa akiidai Simba kimeonekana kinabadilika kila siku hadi alipofanikiwa kupata upenyo wa kutimiza lengo lake na kuwa huru na baadaye kusajili.

Lazima TFF wajue kama watakuwa nyuma ya hizi kamati zifanye nini ni tatizo. Kama hawako nyuma, halafu wakakaa kimya kwa kuwa zinatumia jina la shirikisho hilo, basi ni tatizo kubwa maradufu.

Vizuri haki ikapewa nafasi, ushkaji, kuridhishana kijinga, tamaa na ubinafsi ukiondoka. Itakuwa rahisi kwetu kupambana na “ukichwa wa mwendawazimu”. Ikibaki hivi, basi soka letu litabaki kuwa la kubahatisha milele.


SOURCE: CHAMPIONI

7 COMMENTS:

  1. Okwi alienda Simba mkakaa kimya, Dk.Ndumbalo akafungiwa mkakaa kimya, Bodi ya ligi ikalazimisha Azam kuonyesha mpira wa Yanga mkakaa kimya, Leo mess anaenda Azam kwa dhuluma bado mnakaa kimya!! Na bado dhuluma na uaharibifu wa soka utazidi kuongezeka kwa wadau kukaa kimya kinafiki

    ReplyDelete
  2. Kweli Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu msemo huu hautafutika mpaka kiyama kitakaposimama, swali najiuliza kama kuna mwenye jibu naomba anijibu Huo mkataba uliovunjwa mpaka Singano akawa huru ni mkataba upi? Wa miaka mitatu uliokuwepo simba au ni wa miaka miwili aliokuwa nao singano?

    ReplyDelete
  3. Umeongea vitu ambavyo vinazidi kuigharimu nchi yetu endapo ukimya utazidi. Katika hili simba kaonewa na ni mpango madhubuti ambao Azam walishauandaa.
    Hainiingii akili ndani ya masaa 30 Mesi awe kakaa na family yake,manager wake, mwanasheria wake na kupata ofa Azam, waupitie mkataba then asaini? Hapa mambo yalisha malizwa kabla ya hukumu, Haina shida Simba itabaki kuwa Simba.
    SIMBA NGUVU MOJA

    ReplyDelete
  4. Ni dhahiri Singano na wakala wake walichezea mkataba.Nasema hivyo kwa sababu tokea mwanzo Simba ilisimama kidete kutetea mkataba wa miaka mitatu kuwa ulikuwa ni halali na walikuwa tayari kulifikisha swala hili mahakamani.kwa hakika TFF mnapotupeleka ni pabaya.....

    ReplyDelete
  5. Were saleh mnafiq tu,kwa kua wewe ni simba ndio unalalama mesi kwenda azam,mbona okwi huku lalama,wewe bwege,acha usimba wako fala we

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic