Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, leo
Jumamosi anatarajiwa kuzindua rasmi Wiki ya Simba, ikiwa ni maandalizi ya
kuelekea kwenye Tamasha la Simba Day, litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Simba imeandaa tamasha hilo lenye lengo la
kuwatambulisha wachezaji wake wote, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema
katika wiki hii klabu yake itafanya mambo mbalimbali yakiwemo ya kijamii ili
kujiweka karibu na mashabiki wake.
Aliyataja mambo ambayo yatafanyika katika wiki
hii ni pamoja na uzinduzi wa maduka yatakayouza vifaa vya timu hiyo, uzinduzi
wa matawi mapya, kutembelea wazee wa klabu hiyo, wadhamini wa klabu na kufanya
usafi katika miji nchi nzima.
“Kesho (leo) rais atazindua rasmi Wiki ya
Simba, kutakuwa na matukio mengi, katika wiki hii tutafanya mambo mengi ambayo
yataifanya Simba kuwa klabu ya kipekee nchini.
“Katika wiki hii ya Simba, wachezaji
watatembelea shule mbalimbali ili kuwapata wanachama wapya watoto wa Simba na
katika Simba Day tunategemea mchezaji wetu mpya Laudit Mavugo atakuwepo,”
alisema Manara. Simba inatarajiwa kucheza na FC Leopards ya Kenya katika siku
yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment