Vital’O ya Burundi inasisitiza haiwezi kumuachia
straika wake Laudit Mavugo hadi ilipwe dau la usajili la dola 100,000 (Sh
milioni 206), mchezaji huyo amesema hata kama dili lisipokamilika, hawezi
kurudisha fedha aliyopewa na Simba.
Simba hivi karibuni iliingia mkataba na Mavugo
ili aichezee timu yao lakini kumbe mchezaji huyo ana mkataba wa mwaka mmoja na
klabu hiyo ya Burundi.
Sasa viongozi wa Vital’O baada ya kusuasua kwa
muda mrefu katika kumruhusu Mavugo ajiunge na Simba, wamesema watafanya hivyo
endapo klabu hiyo ya Tanzania itakubali kulipa dola 100,000 (Sh milioni 200)
kuvunja mkataba.
Mavugo aliliambia Championi Jumamosi kutoka
Burundi kuwa, Simba ilimlipa dola 10,000 (Sh milioni 20) ili asaini na
ikamwambia itampa kiasi kingine kama hicho atakapotua nchini.
“Siwezi kurudisha fedha hizo kama dili langu
hilo la kutua Simba litakwama kwani tayari nimeshazitumia kwa ajili ya mambo
yangu ya kimaisha.
“Labda wakitaka wanisubiri hadi nitakapomaliza
mkataba wangu na Vital’O mwakani nitakuja Tanzania kuichezea Simba,” alisema
Mavugo ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Burundi akiwa amefunga mabao 34.
“Hata
hivyo, binafsi napenda sana nije huko kuitumikia Simba, najitahidi kuwashawishi
viongozi wangu ili waweze kumalizana nao. Simba wameniambia kuna kiongozi wao
mmoja anakuja kumalizana na Vital’O ili mambo yaishe.”
Jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara
alisisitiza Mavugo atajiunga na Simba na kuichezea timu hiyo Jumamosi ijayo
katika Simba Day dhidi ya AFC Leopards ya Kenya.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment