Wakati uongozi wa Simba ukiendelea kujiandaa kuhusiana na mipango
ya kuipeleka timu hiyo Oman kwenda kuweka kambi ya mwisho ya kujiandaa na msimu
mpya wa Ligi Kuu Bara, mpango huo umepingwa vikali na Kocha Mkuu, Muingereza,
Dylan Kerr.
Chanzo kikubwa cha Kerr kukataa mpango wa kambi hiyo ni kuhusiana
na hali ya hewa ya huko ingawa amekiri kuwa anaweza kupata sehemu na viwanja
vizuri kwa ajili ya kufanyia mazoezi.
Kerr amesema kwamba bado
hajajua wapi wanaweza kwenda kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi hayo lakini
anaangalia pia uwezekano wa kurejea Lushoto, Tanga walikokwenda kuweka kambi ya
awali kabla ya kutua Zanzibar.
Amefafanua kuwa, Oman kuna joto sana na hataweza kuwafua wachezaji
wake ipasavyo na hiyo inaweza kuwasumbua kuelekea msimu ujao na kingine ni
kwamba anahitaji kuwajenga zaidi kisoka wachezaji wake kuliko stamina katika
wiki hizi chache zilizosalia kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara, Septemba 12,
hivyo sehemu ya joto kwa mbinu hizo haiwafai.
“Bado tunaangalia ni wapi pa kwenda kuweka kambi hii ya mwisho
lakini Oman hapana, kule kuna joto sana, ni kweli kule kuna mazingira mazuri
kwa ajili ya mazoezi lakini hali ya hewa ni tatizo. Nahitaji kuwapa zaidi mbinu
za soka kwa sasa na si stamina kwa sana, hivyo Oman kule tutasumbuka.
“Tunaweza kuangalia kama ni kurejea Lushoto au kama tutapata
sehemu nyingine nzuri zaidi kwa ajili ya mafunzo niliyokueleza basi tunaweza
kwenda huko,” alisema Kerr ambaye ameiongoza Simba kwenye mechi saba za
kirafiki hivi karibuni na kushinda zote kwa idadi ya mabao 18 ya kufunga na
manne ya kufungwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment