AZAM FC na Yanga leo zinacheza mchezo wa Ngao
ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, gumzo kubwa katika mchezo
huo ni straika Donald Ngoma na beki Pascal Wawa.
Ngoma, raia wa Zimbabwe, anaonekana kuwa ndiye
atakayeibeba Yanga katika mchezo huo huku Wawa wa Azam akitabiriwa kuwa mtu
atakayeweza kuizuia safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao.
Wawa, raia wa Ivory Coast, ana nguvu, anajua
kumiliki mpira na ukimuendea vibaya hata chenga anakupiga, hivyo kazi itakuwepo
kati yake na Ngoma mwenye nguvu pia na uwezo mkubwa wa kuwalamba chenga mabeki.
Hata hivyo, mchezo huo unaweza kuvurugika zaidi
kwani kuna uwezekano wawili hao wakacheza kwa kukamiana zaidi na kutolewa kwa
kadi nyekundu au mmoja wao kuumia mapema jambo ambalo Hall na Pluijm
wameshalifanyia kazi.
Hata makocha wa timu hizo, Stewart Hall wa Azam
na Hans van Der Pluijm wa Yanga, wanafahamu hali hiyo na kila mmoja amemuandaa
mchezaji wake kupambana ili kupata ushindi ambao ni lazima upatikane hata kwa
njia ya penalti.
REKODI YAO NGAO YA JAMII
Mchezo wa Ngao ya Jamii hukutanisha timu bingwa
na iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Yanga ndiye
bingwa na ya pili ilikuwa Azam.
Hii ni mara ya tatu kwa timu hizi kukutana na
katika mara mbili walizokutana, Yanga ilishinda mechi hizo. Mwaka juzi Yanga
ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Salum Telela na mwaka jana katika mchezo huo,
Wanajangwani walishinda mabao 3-0 yaliyofungwa na Simon Msuva na Geilson Santos
‘Jaja’ aliyefunga mawili.
Wiki chache zilizopita, katika robo fainali ya
Kombe la Kagame, kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga ilifungwa kwa penalti 5-3 baada
ya kutoka suluhu na Azam. Hadi leo tambo kwa mashabiki wa timu hizo zinatawala
mtaani.
Kipigo hicho ni cha pili kwa Yanga ndani ya
miezi mwili iliyopita kwani Mei 6, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara,
Azam ilishinda mabao 2-1.
Mechi ilichezwa katika mvua na ilionekana kama
Yanga ‘iliachia’ ili kuiruhusu Azam ipate pointi tatu za kuiwezesha kushika
nafasi ya pili badala ya Simba.
BUSUNGU AINGILIA KATI
Wakati mashabiki wengi wakisubiri kutazama
‘sinema’ ya Ngoma na Wawa, Yanga ipo makini kwa kuwapa makali zaidi
washambuliaji wake wengine kama Malimi Busungu na Amissi Tambwe.
Busungu ameliambia Championi Jumamosi: “Siogopi
lolote katika mchezo huu, nasikia Azam wana beki imara ila na sisi tuna fowadi
kali inayoweza kuwapenya.”
Hii inamaanisha kwamba, wakati Ngoma na Wawa
wakiwa ‘bize’ na vita yao huku Busungu na Tambwe watakuwa wakifanya vitu vyao
wakipambana na mabeki wengine waliobaki ambao ni Aggrey Morris na Said Morad
kwani kuna uwezekano Hall akawachezesha mabeki watatu wa kati.
AZAM YAJIFICHA, HALL ATAMBIA ULINZI
Jana asubuhi, Azam ilizuia mtu yeyote kutoingia
kwenye uwanja wake wa Azam Complex ili kutobaini mbinu zake za ushindi huku
Kocha Hall akionekana kuwa makini na uchezaji wa pasi fupifupi.
Hall amesema: “Hii ni mechi kubwa, si lazima kila kitu kiwe wazi,
lakini niseme tu kuna marekebisho makubwa niliyofanya baada ya Kagame.
“Naiamini safu yangu ya ulinzi, itafanya vizuri
na kuweza kuizuia safu yoyote ya ushambuliaji, japokuwa katika soka lolote
laweza kutokea, tunachotaka ni kufanya vizuri na kuweka heshima katika mechi
zetu za Ngao ya Jamii.”
YANGA YATULIZA PRESHA
Kocha raia wa Uholanzi, Pluijm amesema
amejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza presha kwa wachezaji wake ili waweze
kufanya vizuri katika mchezo huo.
Pluijm ambaye pia kikosi chake kimefanya
mazoezi ya siri wiki hii kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi, Kurasini
jijini Dar es Salaam, alisema:
“Hii ni mechi kubwa, ni ngumu kutabiri matokeo
yake, mimi nimewaambia wachezaji wangu wapunguze presha ili tushinde mechi hii
na kulinda heshima ya ubingwa tunaoushikilia.
“Hatutaki tuwaze sana kuhusu matokeo
yaliyopita, makosa yote ya mchezo uliopita na kuwasoma wapinzani wetu ni
miongoni mwa vitu tulivyovifanyia kazi.”
ULINZI BOMBA, MAMBO DAKIKA 90 TU
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Baraka Kizuguto, ameliambia gazeti hili kwamba: “Ulinzi ni wa uhakika,
kutakuwa na polisi wengi na walinzi wengine.
“Mchezo huu utaanza saa 10:00 na dakika 90
zikiisha kama timu hazitafungana zitapigwa penalti.”
TFF pia imembadilisha mwamuzi Israel Nkongo na
sasa mchezo huo utachezeshwa na Martin Saanya kwani Nkongo anasumbuliwa na
maumivu ya misuli.
VIKOSI:
Azam: Aishi Manula, Himid Mao, Erasto Nyoni,
Aggrey Morris, Pascal Wawa, Said Morad, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’,
Shomari Kapombe, John Bocco, Kipre Tchetche na Farid Mussa.
Yanga: Ali Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Haji
Mwinyi, Vincent Bossou, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke, Haruna
Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Simon Msuva.
Mohammed Mdose, Said Ally na Khadija Mngwai.
0 COMMENTS:
Post a Comment